Na Hadija Bagasha Pangani
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala ameanza kuvalia njuga vitendo vya ubakaji na ulawiti huku akiliagiza jeshi la polisi Wilayani humo kumfuatilia na kumkamata mtu mmoja kwenye kijiji cha Bushiri ambaye ameripotiwa kwa tuhuma za kuwashawishi watoto wa kiume ili afanye nao vitendo hivyo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku uuzwaji wa pombe majumbani ambao umebainika kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa familia hususani wakati ambao watu wanaanza kulewa.
Kilakala ametoa maagizo hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ccm Wilaya ya Pangani huku akiitaka jamii kuungana kuhakikisha wanafanikiwa kwenye vita dhidi ya ukatili huo kwa watoto.
Mkuu huyo wa Wilaya alitolea mfano mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu kwenye kijiji hicho ambaye mara kadhaa mtu huyo amekuwa akimrubuni kwa kutaka kumlawiti na kwamba ameripoti maeneo kadhaa lakini mtu huyo bado hajachukuliwa hatua.
"Ndugu Mwenyekiti nilikwenda kwenye shule moja ( jina lake limehifadhiwa) hapa Bushiri mtoto mmoja jasiri, tungekuwa na watoto majasiri kama yule hili tatizo lingekwisha kabisa kwa muda mfupi, yule mtoto alizungumza kwa uchungu nadhani alikuwa form 3 au form 4 ameonyesha maigizo akaimba baadae akachukua maiki na kuzungumza kunambia mkuu wa wilaya mimi binafsi nimefanyiwa ukatili wa kijinsia kuna mzee ananitaka mimi kimapenzi hali yakuwa anajua mimi ni mtoto wa kiume, "alisema DC Kilakala
"Nimekwenda kushitaki kijijini nimekwenda kushitaki kwenye kata sijapata msaada nimempongeza yule kijana kwa kuwa jasiri nimempongeza yule kijana kwa kuwa jasiri watoto wetu mpaka wanaharibika ndio tuchukue hatua nimeliagiza jeshi la polisi yule mzee anayetuhumiwa wamuhoji atuambie kazi zile anazifanya na nani na ameshawaharibu watoto wangapi Bushiri ndugu mwenyekiti mambo haya si kana kwamba hayapo yapo tukikaa na watoto wetu tutayajua taratibu, "alisema Kilakala.
Kuhusu uuzaji wa pombe majumbani Kilakala amesema baadhi ya kaya zinazouza pombe watu wanapoanza kulewa wanawabaka watoto wa familia bila mama mzazi au baba mzazi kujua kutokana na kuwa bize na biashara hiyo.
Kufuatia hali hiyo Kilakala amepiga marufuku pombe kuuzwa majumbani na tayari wameshaanza kuyafungia baadhi ya maeneo ambayo walevi hufanya vitendo vya hovyo eneo ambalo wanafunzi wanapita wakitoka mashuleni wa wengine kwenda kuiga na kupelekea mmomonyoko wa maadili.
"Nimemuelekeza afisa biashara kupitia Mkurugenzi maeneo yote yanayoendesha biashara kiholela yafungiwe mpaka hapo yatakapopata leseni lakini tumemwelekeza Mkurugenzi watoto hakuna kurudi shule usiku, masomo gani yanapatikana usiku watoto wanarudi nyumbani saa mbili usiku mpaka saa nne usiku wanatoka wapi nielekeze muda wa masomo uzingatiwe na watoto warudi muda waliopangiwa na mzazi ukiona mtoto hajarudi mpaka saa kumi uanze kuwa na wasiwasi sio mtoto anarudi saa nne usiku unasema hiyo kawaida yake, "alisisitiza Kilakala.
Awali akizungumzia mafanikio waliyoyapata katika Wilaya hiyo Kilakala amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewafanyia maendeleo makubwa ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara.
"Nimshukuru sana Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan katika kutuletea miradi mikubwa ya maendeleo lakini nimshukuru na nimpongeze Mbunge wetu na Waziri wetu wa maji Jumaa Aweso kwa namna anavyopambana kupigania kuchochea kuhakikisha Pangani tunapata miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta zote bila kumsahau Mwenyekiti wetu wa Mkoa Rajab Abrahaman kwa kazi kubwa anayoifanya katika Mkoa Tanga lakini katika kuchochea maendeleo katika wilaya yetu ya Pangani na kuwa chachu ya miradi mikhbwa ya maendeleo inayogusa wananchi moja kwa moja, "alisisitiza DC Kilakala.
0 comments:
Post a Comment