
Elimu hiyo imetolewa kupitia kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kuimarisha mawasiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, kuwapa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya usalama katika jamii.
Akizungumza na wananchi hao, SACP Magomi amewahimiza kuendelea kudumisha amani na utulivu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji ili kuzuia vitendo vya uhalifu na kuhakikisha jamii inaendelea kuishi katika mazingira salama.
Aidha, amewataka wananchi wenye silaha haramu kuzisalimisha katika ofisi za serikali za vijiji au mitaa, ofisi za watendaji wa kata na vituo vya polisi, akisisitiza umuhimu wa kuondoa silaha hizo katika jamii ili kupunguza hatari zinazoweza kuhatarisha maisha na usalama wa watu.
Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuhama na kutafuta maeneo salama kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha katika siku zijazo, kwa mujibu wa tahadhari iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia tahadhari za mamlaka husika na kuchukua hatua mapema ili kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua, yakiwemo mafuriko na uharibifu wa mali.
Kuhusu ulinzi wa mtoto, SACP Magomi amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na mazingira salama ya kujifunzia. Pia, amewahimiza wanafunzi waliohudhuria mkutano huo kusoma kwa bidii, kuzingatia masomo yao na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwafanya waache shule kabla ya kukamilisha masomo yao.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Mwalukwa wamepongeza hatua ya Jeshi la Polisi kuwafuata katika maeneo yao na kuwapa fursa ya kuwasilisha maoni na changamoto zinazowakabili.
Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha pia changamoto ya mgogoro wa ardhi. Hata hivyo, kwa kuwa suala hilo halikuwa changamoto ya moja kwa moja ya kiusalama, lilipokelewa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa mamlaka husika ili liweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Kampeni ya Ongea na Kamanda ni jukwaa muhimu la mawasiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, linalowezesha wananchi kupata elimu ya usalama, kutoa maoni yao na kuwasilisha changamoto kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kudumisha amani na utulivu katika jamii.






.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)







































