Sunday 18 April 2021
SIMBA SC YAICHAPA MWADUI FC 1 - 0 KAMBARAGE
Cosota Yatoa Somo La Hakimiliki Kwa Maprodyuza Wa Muziki
Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki, Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Doreen Sinare atoa elimu kwa Watayarisha wa Muziki nchini (Maprodyuza) kwa kuwaeleza umuhimu wa kusimamia haki zao na kuingia mikataba na wasanii pale wanapokuwa wanafanya kazi zao.
Mtendaji huyo ametoa elimu hiyo katika kikao cha Uzinduzi wa Chama cha Umoja wa Maprodyuza Tanzania (Tanzania Producers and Composers Association) kilichofanyika Aprili 17, 2021 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanya uchaguzi wa viongozi pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kuendesha chama hicho ambacho kimeanzishwa hivi karibuni.
"Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaweka ulinzi katika kazi za Sanaa na usimamizi madhubuti wa Hakimiliki na serikali inataka sekta ya Sanaa ikue na kuendana na kipato na siyo mtu anakuwa na umaarufu wa jina halafu kipato chake kinakuwa hakiendani na umaarufu wake "alisema Bibi Doreen.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo wa TPCA Bibi. Doreen alieleza kuhusu Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ambao unatarajia kuzinduliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na pale utakapozinduliwa utawanufaisha wadau wote wa sekta ya Sanaa na Utamaduni kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu, pamoja na kusaidia kutoa ufadhili wa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kuimarisha ujuzi katika kazi zao.
Kwa upande wa Muanzilishi wa Chama hicho Prodyuza P-Funk Majani alitoa ombi kwa COSOTA la kusambaza sampuli za Mikataba na fomu za Usajili na kutaka Studio zote nyaraka hizo ili mteja anapokwenda kuandaliwa kazi ahakikishe anasaini mkataba na studio pamoja na kujaza fomu ya COSOTA studio, ili ulinzi wa kazi kuanza katika ngazi ya chini.
Aidha, nae mmoja wa Maprodyuza hao Quick Raca atoa maoni kuwa ya kuiomba COSOTA kuwa na mfumo wa kusimamia matumizi ya kazi za wanamuziki kwa kutoa msisisitizo kwa Makampuni yaliyosaini mikataba na wasanii peke yao kwa kazi zinazohusisha haki za "Maproducer" makampuni hayo sasa yaingie mikataba pia na ‘Producers’ ili yaanze kulipa na "producers", na kuanzia sasa utaratibu wote upitie COSOTA vilevile matumizi ya kazi za muziki kwenye mitandao yote ilipwe na wanaotumia, halikadhalika Televisheni na Redio zisipige au kuonyesha kazi ya Muziki kama haijapita kukaguliwa BASATA, Bodi ya Filamu Tanzania na kusajiliwa COSOTA.
Pamoja na hayo Maprodyuza hao waliridhia ushauri wa kuanza kujisajili kwenye chama chao na pia kujisajili COSOTA na kusajili kazi zao COSOTA na kwa taasisi zinazowasimamia pamoja na kuanza kuwa na utaratibu wa kutumia mikataba katika kazi zao.
Halikadhalika Doreen aliahidi kuwa COSOTA itatoa sampuli ya mikataba hiyo bure na zitakabidhiwa TPCA ili kuweza kuwafikishia wadau hao. Pia aliwasisitiza kuwa umoja wao ukiwa imara na wenye manufaa wadau wengi wanaweza kujiunga na kunufaika zaidi.hivyo ni vyema wajenge misingi imara ya kukuza tasnia hiyo kwa lengo la kuweza kunufaika vyema na kazi zao.
Mfumo wa Masoko ya Madini Umeongeza Makusanyo Serikalini
Na Steven Nyamiti, Kahama.
Imeelezwa kuwa, Wizara kupitia Tume ya Madini kupanga bei elekezi ya kuuza madini Nchini umesaidia wauzaji na wanunuzi kuondoa ulanguzi wa bei, na kuchochea wachimbaji kuleta madini yao kwa wingi kwenye masoko ya madini Nchini.
Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini Kahama Fabian Itaru tarehe 17 April, 2021 katika ziara yake na wanahabari kutembelea Masoko ya Madini, Vituo vya ununuzi wa Dhahabu na maeneo ya machimbo ya Dhahabu wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa masoko ya madini kumefanya Dhahabu yote kuingia kwenye mfumo wa soko na malipo halali ya Serikali kukusanywa kwa wakati.
"Kuanzishwa kwa masoko haya kumeongeza mapato kwa Serikali. Ofisi ya madini kipindi cha nyuma ilikuwa inapewa lengo la kukusanya bilioni 45 kwa Mwaka ambapo kabla ya kuanzishwa masoko hayo Mwaka 2016 hatukuwahi kufikia lengo, lakini baada ya kuanzishwa masoko ya madini malengo ya Ofisi ya Madini Kahama kupitia Tume ya Madini yamefikia lengo.Mwaka huu tumepangiwa kukusanya bilioni 79 ambapo hadi sasa tumekusanya bilioni 72 sawa na wastani wa asilimia 91" ameeleza Itaru
Amefafanua kuwa, Makusanyo hayo yametokana na masoko ya Madini, shughuli nyingine za Wachimbaji wadogo, Kodi za leseni zinazolipwa, mrabaha na ada za ukaguzi zitokanazo na uzalishwaji wa Dhahabu Kahama.
Naye, Mjiolojia Samuel Baruti kutoka Tume ya Madini akizungumza Katika kituo cha Ununuzi Madini Mwime Kahama, amewaeleza wanahabari kuwa, huko nyuma hali ilikuwa ngumu Sana kwa wachimbaji wadogo kabla Serikali haijaanzisha utaratibu wa masoko.
Amesema kulikuwa na watu wanafanya biashara mitaani na kujipangia bei tofauti na kipindi hichi ambacho Serikali inapanga bei elekezi ili mchimbaji mdogo aweze kuona faida ya uchimbaji wake.
Ameeleza kuwa, miaka ya nyuma mfaidika mkubwa alikuwa mfanyabiashara wa madini lakini baada ya kuanzisha mfumo wa masoko umefanya wafanyabiashara kukusanyika eneo moja katika soko la madini.
Kwa Upande Meneja wa Umoja wa Kwenye Mashamba Ilindi Mwime Joseph Nalimi, akieleza kwa niaba ya wachimbaji wadogo Mwime ameiomba wizara kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kukopesheka na kupata udhamini wa mabenki, kutengeneza miundombinu ya machimbo ya Mwime, na kupata ripoti ya kijiolojia ya maeneo yao ili waache kuchimba kwa kubahatisha.
Nalimi, ameishukuru ofisi ya madini Mkoa wa Kimadini Kahama kwa kuanzisha vituo vya uuzaji na ununuzi Dhahabu karibu na maeneo ya machimbo ambavyo vimesaidia kupata soko la uhakika la Dhahabu
Waziri Aweso Amtumbua Kigogo Wa Moruwasa
Vigogo waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) Mhandisi Tamimu Katakweba,Afisa Maji wa Bonde la Wami Ruvu Bwana Simon Ngonyani huku akiagiza watumishi wengine waliokuwa vinara wa kueneza chuki na kuleta taharuki badala ya kufanya kazi nao wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Waziri Aweso aliyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo alisema kuwa Mkurugenzi wa Moruwasa pamoja na tuhuma nyingine za kiutumishi lakini alisaini mkataba wa fedha nyingi na wakandarasi bila kushirikisha Wizara na hata bila uwepo wa Katibu Mkuu kinyume na taratibu.
Huku Afisa wa Bonde akisimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya utumishi.
WAZIRI AWESO AWASHA MOTO MOROGORO AMTUMBUA KIGOGO WA MORUWASA
Na Mwandishi,Morogoro
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amewasimamisha kazi vigogo wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Morogoro (Morowasa) ili kupisha uchunguzi wa wa tuhuma ambazo zinawakabili huku akiagiza watumishi wengine kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Vigogo waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) Mhandisi Tamimu Katakweba,Afisa Maji wa Bonde la Wami Ruvu Bwana Simon Ngonyani huku akiagiza watumishi wengine waliokuwa vinara wa kueneza chuki na kuleta taharuki badala ya kufanya kazi nao wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Waziri Aweso aliyasema hayo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo alisema kuwa Mkurugenzi wa Moruwasa pamoja na tuhuma nyingine za kiutumishi lakini alisaini mkataba wa fedha nyingi na wakandarasi bila kushirikisha Wizara na hata bila uwepo wa Katibu Mkuu kinyume na taratibu.
Huku Afisa wa Bonde akisimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya utumishi.
Mwisho.
Rais Samia Afanya Uteuzi Wa Mkuu wa Itifaki na Mkurugenzi Mkuu wa eGA
Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Yusuf Mndolwa kuwa Balozi.
Pamoja na uteuzi huo, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Balozi Mteule Mndolwa kuwa Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol) katika wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Mteule Mndolwa anachukua nafasi iliyoachwa na Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Mteule Mndolwa ataapishwa Jumatatu aprili 19, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Wakati huo huo Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Benedict Ndomba kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Kabla ya uteuzi huo Ndomba alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu na Operesheni wa eGA na anachukua nafasi ya Dkt. Jabir Kuwe ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Uteuzi wa viongozi hao umeanza Aprili 17, 2021.
Vijana 854 wa JKT walioandamana kwenda Ikulu watimuliwa
Mkuu wa majeshi nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema vijana 854 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokiuka taratibu kwa kuanzisha mgomo na kuandamana kwenda Ikulu wakishinikiza kuajiriwa jeshini wamesitishiwa mikataba yao na kurudishwa majumbani.
Mabeyo ameeleza hayo jana Jumamosi Aprili 17, 2021 katika hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mjini Dodoma.
"Aprili 8, 2021 vijana wetu wa JKT wapatao 854 walianzisha mgomo, kukataa kufanya kazi maeneo mengine na kufanya maandamano kwenda Ikulu kwa madai ya kutaka kumuona rais ili wadai kuandikishwa jeshini kama walivyoahidiwa na aliyekuwa rais wa Tanzania, John Magufuli."
"Vijana hao ni kati ya vijana 2400 walioahidiwa kuandikishwa jeshini na walifanya uamuzi huo baada ya jeshi kuamua kuwapunguza katika kazi ya ujenzi wa Ikulu Chamwino baada ya kazi kupungua ili waende kufanya kazi katika maeneo mengine lakini wao wakapinga kwa madai wangekosa kuandikishwa jeshini, " amesema Mabeyo.
Amebainisha kuwa jeshi halikuwa na lengo hilo na limelazimika kusitisha mikataba yao kwa kuwa kosa walilolifanya ni sawa na uasi na hauvumiliki.
Ameeleza kuwa pamoja na kufanya uchunguzi wa kwa nini walifanya hivyo, jeshi limeamua kutafakari upya mpango wa kuchukua vijana wa kujitolea kwa ajili ya kujiunga na JKT.
Waziri aiagiza OSHA kufanya tathmini ya maeneo ya kazi yenye ajali,magonjwa mengi
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi,Vijana,Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kufanya tathmini ya maeneo ya kazi yanayoongoza kwa matukio ya ajali na magonjwa pamoja na kubainisha visababishi vyake ili kuwezesha uandaaji wa mkakati wa kudhibiti visababishi hivyo.
Ametoa agizo hilo alipokuwa akifungua kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kupitia bajeti ya mwaka 2021/2022.
“Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu inaonesha taasisi yenu imekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambayo yametokana na maboresho mbali mbali ambayo yamekuwa yakifanyika na serikali ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo ambazo zilionekana kuwa kero.Hivyo, nawaagiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuweza kufikia lengo letu la kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi na kuleta ustawi wa Taifa letu,” alieleza Mhagama.
Waziri huyo wa Nchi aliwashauri wajumbe wa kikao hicho kufanya majadiliano katika kikao hicho kwa hekima na busara na hatimaye kutoka na maazimio muhimu ambayo yatafanyiwa kazi ili kutimizi malengo ya taasisi.
Aidha, aliitaka taasisi ya OSHA kuendelea kubuni mifumo mbali mbali ya Tehama ambayo itaboresha utoaji wa huduma kwa wadau pamoja na kuweka taratibu za huduma ambazo ni rafiki kwa wadau ili kuendana na maelekezo ya serikali.
Awali wakati akimkaribisha Waziri ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema maboresho ambayo yamekuwa yakifanyika na serikali katika sekta ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo, yamepelekea taasisi hiyo kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza usajili wa maeneo ya kazi kutoka 5,300 hadi 20,000 kwa kipindi kati ya mwaka wa fedha 2014/2015 na 2020/2021.
Kwa upande wao mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa, Fidelis Athuman na Mjumbe wa Baraza hilo, Joyce Mwambungu, wameipongeza serikali na uongozi wa OSHA kwa maboresho ya utendaji ambayo yamekuwa yakifanyika kutokana na ushirikishwaji wa watumishi kupitia vikao vya mara kwa mara vya baraza la wafanyakazi.
Kikao hiki ambacho ni cha pili cha baraza la nne la wafanyakazi wa OSHA pamoja na masuala mengine, kilikuwa na agenda kuu ya kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao (2021/2022).
Mabaraza ya wafanyakazi katika taasisi mbali mbali za umma yapo kwa mujibu wa Sheria Na. 19 ya Mabaraza ya mwaka 2003 ambayo iliundwa kupitia Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 1970. Lengo likiwa ni kuleta ushirikishwaji baina ya menejimenti na watumishi katika kufanya maamuzi yanayohusu utendaji wa taasisi husika.
Utumishi Kusimamia Utekelezaji Ahadi Za Masuala Ya Kiutumishi Kwenye Ilani Ya Ccm Ya Mwaka 2020
Na. James K. Mwanamyoto
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Ofisi yake kusimamia utekelezaji wa ahadi za masuala ya kiutumishi na utawala bora zilizoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 ili kuhakikisha Sekta ya Umma inaimarika na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi yake uliofanyika jijini Dodoma.
Mhe. Ndejembi amelitaka baraza hilo kupitia na kuchambua Ilani kwa kina na kubaini ahadi zinazohusu Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Akihimiza utekelezaji wa Ilani katika Taasisi za Umma, amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza ahadi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Ndejembi amesema, licha ya Watumishi wa Ofisi ya Rais-Utumishi kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza Ilani, lakini wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanabadili mtazamo hasi dhidi yao kwani malalamiko mengi yanayowasilishwa Utumishi yanatokana uzembe wa Watumishi wa Taasisi nyingine.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa baraza, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Bi. Agnes Meena amemuahidi Mhe. Ndejembi kuwa, Utumishi itahakikisha inaishauri vizuri Serikali kutekeleza Ilani na kuongeza kuwa, watumishi wataendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha ofisi kufikia malengo yake.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imefanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, ambapo Taasisi za Umma zinapaswa kukutana kupitia mpango na bajeti itakayowasilishwa Bungeni, kabla Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijapitisha bajeti husika kwa ajili ya utekelezaji.