Saturday 2 January 2021

NFRA Wajipange kununua Mahindi mengi kwa Wakulima – RC Wangabo


Wakati Utekelezaji wa lengo la Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) la kuweka mfumo wa kisasa wa kutunza mazao kufikia asilimia 80. Wakala hao wameshauriwa kujiandaa kununua mahindi mengi Zaidi ili kuwahakikishia wakulima soko la mazao yao katika kipindi cha msimu wa 2020/2021

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa ni vyema NFRA wakaongeza fedha za kununua mahindi na kisha kutafuta soko nje ya nchi hasa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Pamoja na nchi nyingine ili kuwapa fursa wakulima nchini kufanya biashara na NFRA ili kuepuka kuhangaika kutafuta soko la mazao yao.

“Mkoa wa Rukwa tumezalisha tani za mahindi tani 585,000 na matumizi yetu ya ndani ni tani 291,000 kwahiyo tulikuwa tuna ziada ya tani 294,000, sasa ukiangalia kwamba tani 294,000 halafu mahindi yananunuliwa tani 11,000 kwahiyo mahindi mengi yalibaki ndio kikawa kilio cha wakulima wa mkoa wetu wa Rukwa kwahiyo nategemea kwamba ukamilishwaji wa vihenge hivi NFRA itakuwa na uwezo wa kuchukua tani 58,500, hii kwa sisi mkoa wa Rukwa ni sawa na kuingiza na kutoa ili wawauzie watu wengine.”

“Kwahiyo niwaombe NFRA ndio wamekuwa mkombozi sasa kwa wakulima, mjipange vizuri ili kuongeza fedha muweze kununua mahindi mengi kwa wakulima vinginevyo wakulima watakata tamaa na sasa wanaendelea kuzalisha baada ya kuona kwamba hivi vihenge hapa vinakwenda kukamilika kwahiyo uwezo wa NFRA utakuwa mkubwa Zaidi wa kununua mahindi kwa wakulima, ninyi mnao uwezo wa kuona wapi muyapeleke hayo mahindi, ninyi mfanye biashara na nje na sisi tufanye biashara na nyie,” Alisema.

Kwa upande wake Mhandisi Mkazi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Haruna Kalunga amesema kuwa hadi tarehe 28.12.2020mkandarasi ameshatumia muda wake wa miezi 15 sawa na asilimia 83 ya muda aliopewa kwenye mkataba huku utekelezaji ukiwa ni asilimia 80 na hivyo kuufanya mradi kuwa nyuma kwa asilimia 3 na kuongeza kuwa ucheleweshwaji huo umechangiwa na kucheleweshwa kwa msamaha wa kodi wa vifaa vinavyotoka nje ya Tanzania.

Kwa mkoa wa Rukwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Unia Araj kutoka Poland ikisaidiana na Mkandarasi Mzawa Elerai kutokea Arusha kwa thamani ya Dola za marekani 6,019,399.00 ambayo ni asilimia 30 ya mradi mzima unaotekelezwa katika mikoa mitatu Pamoja na Mkoa wa Katavi na Manyara wenye jumla ya thamani yad ola za marekani 20,280,906.00.


Share:

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya Azitaka Taasisi Kujipanga Upya

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutatua kero na malalamiko ya wananchi kwa wakati katika miradi na huduma wanazozitoa.

Akizungumza mkoani Rukwa mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Sumbawanga –  Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112  na upanuzi wa bandari ya Kasanga, Naibu Waziri Kasekenya ameridhishwa na utekelezaji wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi China Railway 15 Group kukamilisha sehemu iliyobaki yenye urefu wa mita 150 katika kipindi cha siku 45.

Aidha, amemtaka Mkandarasi Shanxi Construction Engineering anaetekeleza mradi wa upanuzi wa bandari ya Kasanga kutathmini kazi anayoifanya kama iko katika viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa mkataba kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Hakikisheni kazi za ujenzi wa barabara na upanuzi wa bandari zinakamilika katika kipindi kifupi kuanzia sasa, kwa kuwa muda uliopangwa kimkataba umemalizika”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Meneja wa Bandari ya Kigoma kufika eneo la mradi ndani ya wiki moja kwa ajili ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kutoa ripoti.

Kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga Port na upanuzi wa bandari ya Kasanga ni mkakati wa Serikali wa kuhuisha uchumi katika ukanda wa Magharibi wenye mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na hivyo kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi za Zambia, Burundi na Congo DRC.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius Misungwi, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kuchochea shughuli za kibiashara za Wilaya na kuiomba Serikali kuendelea kuibua fursa za kiuchumi kwenye ukanda huo wenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.

Naibu Waziri Kasekenya yupo katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Ukanda wa mikoa ya Magharibi ambapo pamoja na mambo mengine anakutana na watumishi wa Wizara ili kubadilishana uzoefu.


Share:

Waziri Kalemani Aigiza Tanesco Kuwaombea Ajira Watumishi Walioajiriwa Kwa Mikataba Ya Muda Mfupi Kwa Kipindi Kirefu.


Na Dorina G. Makaya – Shinyanga.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la TANESCO nchi nzima, kuwaombea ajira watumishi walioajiriwa kwa vipindi vifupi na kuitumikia TANESCO kwa muda mrefu.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 30 Mwezi Desemba, alipokuwa akizungumza na watumishi wa TANESCO wa Mkoa wa Shinyanga, katika kikao kazi cha kufahamiana, kusikiliza kero na kutoa maelekezo ya kazi ili kuliwezesha shirika la TANESCO nchini kufanya kazi kama timu moja kwa kasi kwa ubunifu na kwa usahihi ili kufikisha huduma ya umeme kote nchini na kuongeza mapato ya Serikali kutokana na Sekta ya Nishati.

Akizungumza baada ya kusikiliza Kero za Watumishi wa TANESCO mkoa wa shinyanga, Waziri Kalemani ameweka bayana kuwa, watumishi hao wanaoajiriwa kwa vipindi vifupi ndio wanaokutana na wateja moja kwa moja na kujenga taswira ya TANESCO (Visibility) kwa wateja wanaohitaji na kutumia huduma ya umeme hapa nchini.

Amesema, kufanya kazi kama kibarua kwa miaka mingi bila ya kuajiriwa kwa watumishi hao, kunapunguza na pengine kuondoa hari ya kufanya kazi watumishi hao, kuleta mianya ya rushwa na hata kutengeneza vishoka.

Dkt. Kalemani ameeleza kuwa, anaamini kuajiriwa kwa watumishi hao, kutawajengea kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kujituma kwani watahitaji kutunza ajira zao na kuonya kuwa, mtumishi yeyote atakayebainika anaomba rushwa  kutoka kwa wateja na kutumia lugha zisizofaa, huyo atondolewa mara moja na hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi yake.

Akielezea kuhusu umuhimu wa kikao kazi hicho, Waziri Kalemani amefafanua kuwa, ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa kazi, ipo haja ya kuonana na watumishi, kufahamiana, kujionea mazingira halisi ya kazi, kusikiliza kero zao na kuzitolea ufumbuzi na kisha kutoa mwelekeo na maelekezo ya kazi kufikia malengo yaliyowekwa kwenye Sekta ya NIshati.

“Unaweza kuwa unaagiza nataka kazi hii ifanyike leo na kukamilika leo hii hii, na kumbe unayempa maelekezo hayo ni mlemavu na hana uwezo wa kwenda kwa kasi hiyo. Ukaagiza afukuzwe kwa kushindwa kutekeleza kazi husika, lakini kumbe uliyemwagiza ni mlemavu. Hivyo ni muhimu kufahamiana. Amesema Dkt. Kalemani.”

Aidha, Waziri huyo wa Nishati  ameiagiza TANESCO, kuwanunulia pikipiki watumishi walio katika vitengo vya upimaji  kwa ajili ya kufikisha umeme kwa wateja ( surveyors ) ili kuwezesha utendaji kazi kwa haraka na kuwaelekeza watumishi hao kuzitumia pikipiki hizo kwa shughuli za kikazi. “msije mkazigeuza pikipiki hizo kuwa bodaboda!  Tena mziandike SU. Nataka mfanye kazi kwa kasi, kwa ubunifu, na kwa usahihi,  amesema Waziri Kalemani.

Nataka kila ofisi ya TANESCO ninayo kwenda nione kuna ongezeko la mapato, nione kuna ongezeko la wateja sugu kulipa madeni  wanayodaiwa TANESCO.

Waziri Kalemani ameigiza TANESCO na REA kuhakisha vijiji vyote nchini viwe vimeunganishwa na umeme, ifikapo Septemba 2022.

Dkt. Kalemani pia ameiagiza TANESCO kutumia nguzo za zege kwenye maeneo korofi yenye maji (Swamp areas) ili kuepusha gharama za matengenezo zinazotokana na nguzo kuanguka mara kwa mara na wateja kukosa umeme wakati matengenezo yanapokuwa yanafanyika kurejesha umeme. Aidha, Waziri Kalemani ameielekeza TANESCO nchini, kutoza gharama za uunganishwaji wa umeme kwa wateja kwenye vijiji na vitongoji kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kwa wateja wanaotumia njia moja ya umeme isipokuwa katika maeneo ya majiji.


Share:

Halmashauri Zaonywa Wafanyabiashara Kuchanja Mifugo, Mikataba Yao Kuvunjwa


Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutotumia wafanyabiashara kuchanja mifugo na kutaka kuvunjwa kwa mikataba hiyo mara moja.

Waziri Ndaki amebainisha hayo  (31.12.2020) alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Shinyanga ambapo alipokuwa katika josho la kuogeshea mifugo la Kijiji cha Mipa kilichopo Wilaya ya Kishapu mkoani humo kwa ajili ya kushuhudia uogeshaji mifugo na utoaji wa chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, wafugaji wamemlalamikia kuwa baadhi ya ng’ombe kijijini hapo wamekuwa wakivimba na wengine kufa baada ya kupatiwa chanjo.

Waziri Ndaki akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amesema kuanzia sasa chanjo zote nchini zitatolewa na wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa na kugoma kushuhudia zoezi la uchanjaji lililokuwa limeandaliwa baada ya kukasirishwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kutokuwa na takwimu yoyote ya idadi ya ng’ombe waliovimba na wengine kufa baada ya kuchanjwa.

“Halmashauri zetu zote kuanzia sasa hivi ni marufuku kutumia wafanyabiashara kuchanja mifugo yetu, halmashauri zitumie wataalamu wa wizara ambao wamethibitishwa waweze kuchanja mifugo ya wananchi wetu, hao wafanyabiashara kama mmeingia mikataba nao hiyo mikataba ivunjeni haraka iwezekanavyo hatuwezi kuchezea akili za watu namna hii hatuwezi kutuma wafanyabiashara waende kuchanja ng’ombe wanavimba na wanakufa halafu taarifa hatuna.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki katika ziara yake ya siku moja Mkoani Shinyanga amefika katika mnada wa upili wa Mhunze ambao ni moja ya minada inayosimamiwa na wizara na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kumuondoa mara moja kazini mhasibu wa halmashauri hiyo anayefanya kazi katika mnada huo Bw. Athanas Msiba kwa tuhuma za kutokuwa mwaminifu katika kuandika idadi ya mifugo inayoingia na kutoka katika mnada huo hali inayosababisha wizara na halmashauri kukosa mapato stahiki.

“Mkurugenzi huyu Athanas Msiba siyo mwaminifu hafai kukaa hapa tena aondoke sasa hivi ulete mtu mwingine, watu wakipita hapa na mbuzi watano anaandika watatu anaandika kidogo hafai aondoke hapa.” Amesema Mhe. Ndaki

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bw. Emmanuel Johnson amesema amepokea maelekezo hayo na atayafanyia kazi kwa kuihusisha pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ili ifanye ufuatiliaji kwa kuwa serikali haiko tayari kuwa na watu wenye tabia ya namna hiyo.

Akiwa katika mnada huo Waziri Ndaki amepata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wafugaji ikiwemo ya kuzuiwa kuondoa mifugo mnadani kabla ya saa 12 jioni hali inayohatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa fisi wengi kwenye maeneo ya mashamba wakati wa kurudi nyumbani majira ya jioni hali iliyomlazimu Waziri Ndaki kuutaka uongozi wa mnada utafute utaratibu wa kuwaruhusu wafanyabiashara kuondoka kabla ya muda huo wakiwa wamemaliza shughuli zao.

“Mtu amemaliza biashara yake mkagueni vizuri kwenye mlango wa kutokea aende zake akimaliza hapa akikaa saa mbili aondoke, akikaa dakika 15 aondoke ili mradi amemaliza shughuli zake siyo unawaleta unawafungia humu haka kamekuwa kajela kadogo? Hapana hiyo.” Amefafanua Waziri Ndaki

Akiwa Mkoani Shinyanga Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul, ametembelea ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika Manispaa ya Shinyanga unaogharimu Shilingi Bilioni 5.5 ambapo tayari zimelipwa Shilingi Bilioni 5.1 na umefikia asilimia 97 hadi kukamilika kwake.

Mara baada ya kukamilika machinjio hayo Mwezi Februari Mwaka 2021, yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 mbuzi na kondoo 1,000 kwa siku.

Siku moja kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga, Waziri Ndaki akiwa na Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul walifika katika shamba la mifugo la serikali Shishiyu Holding Ground lililopo katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu, ambapo Waziri Ndaki amesema shamba hilo lenye ekari 10,240 halina tija kwa sasa kwa kuwa limebaki pori na hakuna mifugo.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi inataka maeneo yote ya mashamba ya serikali ya mifugo ambayo yapo chini ya wizara kuyaweka chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), ili NARCO washughulike nayo kwa sababu ni chombo pekee cha wizara kinachokubaliwa kufanya biashara ya kupangisha maeneo kwenye mashamba ya wizara.

Waziri Ndaki amefikia hatua hiyo baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuomba ekari 1,500 ili kuendeleza shamba hilo kwa ajili ya kunenepesha mifugo ikiwemo kuotesha malisho pamoja na kuelimisha wananchi namna ya kufuga mbegu bora za mifugo, ambapo Waziri Ndaki amesema atatoa maamuzi ya ombi lao haraka iwezekanavyo.

Amefafanua kuwa haina maana wizara kuwa na maeneo makubwa katika mashamba yake ambayo hayatumiki huku wafugaji wakiwa hawana maeneo ya malisho yao hivyo ni bora kuyapangisha ili serikali iweze kupata mapato kupitia mashamba hayo.


Share:

Naibu Waziri Mabula Awashukia Wakurugenzi Halmashauri Kuzitelekeza Idara Za Ardhi


Na Munir Shemweta, WANMM KIBAHA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelea ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu baadhi ya wakurugenzi wa halamashauri kwa kushindwa kuzihudumia idara za ardhi katika halmashauri zao na kuzifanya idara hizo kufanya kazi katika mazingira magumu.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, uongozi wa mkoa wa Pwani na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo tarehe 31 Desemba 2020 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Pwani, Dkt Mabula alisema kuna baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa wakorofi na kuziona idara za ardhi kama siyo sehemu ya idara zao na kuziacha bila kuzihudumia.

Alisema, baada ya kutoka waraka uliohamisha Maafisa Ardhi kurudi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuna baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri waliamua kujivua kuzihudumia idara hizo kwa kisingizio kuwa idara hizo sasa haziko chini yao na zimerejeshwa Wizarani.

Dkt Mabula alisema, waraka uliotolewa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa  ulieleza wazi kuwa wajibu wa Wizara ya Ardhi kwa watumishi wa sekta hiyo utakuwa kwenye  masuala ya sera, ajira na nidhamu lakini usimamizi utaendelea kubaki kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, majukumu ya kupanga miji ni ya halmashauri za miji , manispaa na majiji hivyo wakurugenzi wa halmashauri bado wana wajibu wa kuzihudumia idara hizo ili ziweze kupanga miji vizuri pamoja na kutoa huduma zinazohusiana na masuala ya ardhi.

‘’Hawa ni watumishi wenu kama walivyo wale wa idara nyingine za afya, elimu nk hivyo mnapaswa kuwahudumia vizuri ikiwemo kuwapatia vitendea kazi ili waweze kufanya kazi vizuri’’ alisema Dkt Mabula.

Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kubadilika na kuanza kuzihudumia idara za ardhi vizuri kwa kuzipangia idara hizo bajeti ya kutosha pamoja vitendea kazi kama magari na vifaa vya kupimia ili ziweze  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akigeukia suala la ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi, Naibu Waziri Mabula aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuziwezesha idara za ardhi ili ziweze kufuatilia madeni ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mkoa wa Pwani pekee unadai bilioni 32, 762,665,972 za kodi ya pango la ardhi kutoka kwa wadaiwa mbalimbali na kusisitiza kuwa kama  idara za ardhi zitawezeshwa vizuri zinaweza kukusanya mapato mengi  yatakayosaidia utekelezaji  miradi mbalimbali kama vile ya afya, elimu na miundombinu ukilinganisha na idara nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masamia alisema, pamoja na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kukusanya kodi bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika suala hilo kutokana na hadi kufikia Desemba 31, 2020 ni Bilioni 61 ndizo zilizokusanywa na kutaka juhudi za makusanywa kuongezwa katika kila halmashauri. Malengo ya Wizara katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni bilioni 200.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki uliopo wilayani Kibaha mkoani Pwani mradi unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo , Dkt Mabula alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa miradi mbalimbali iliyokabidhiwa na kulitaka kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kujenga imani kwa wateja.


Share:

Chukueni Hatua Kali Kwa Wanaoharibu Miundombinu Ya Barabara – Kasekenya


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezitaka Mamlaka mkoani Rukwa kusimamia kikamilifu Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 inayozuia shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi ili kulinda barabara na madaraja katika bonde la mto Rukwa.

Amesema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Ntendo – Muze Kilometa 37 na barabara ya Kasansa – Kilyamatundu Kilometa 175 ambazo zimeathiriwa na mafuriko ya mvua kutokana na shughuli za kibinadamu za ukataji miti, kilimo na ufugaji katika safu za milima ya ukanda wa bonde hilo.

“Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji hakikisheni tabia ya uharibifu wa mazingira zinazofanywa na wananchi zinakomeshwa maramoja ili kulinda hifadhi za misitu na miundombinu ya barabara na madaraja”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amesema zaidi ya shilingi Bilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha barabara hizo zilizoko katika bonde la mto Rukwa ambalo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula zinakarabatiwa ili kupitika wakati wote wa mwaka na kutoathiri uchumi wa wakazi wa mkoa huo.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Rukwa,  Mhandisi Jotrevas August, amesema zaidi ya madaraja madogo 19 yamebomolewa na mvua hizo zinazoendelea kunyesha katika ukanda huo na hivyo Wakala umejipanga kuhakikisha kuwa ujenzi wake unaendelea ili kutoathiri huduma ya usafiri katika barabara hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dakta. Khalfan Haule, amemhakikishia Naibu Waziri kwamba kwa kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji watahakikisha miundombinu ya barabara na madaraja inayojengwa inalindwa ili ikamilike kwa wakati.

Naibu Waziri Kasekenya yuko katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.


Share:

Serikali Kuweka Mazingira Wezeshi Ya Kuendeleza Vijana Wabunifu Wa Tehama


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali itaweka mazingira wezeshi ya kuendeleza vijana wabunifu wa TEHAMA nchini

Ndkt. Ndugulile ameyasema hayo jana  wakati wa ziara yake ya kutembelea Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Ndaki ya TEHAMA ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COICT) zilizopo Dar es Salaam

Amesema kuwa vijana wanabuni mifumo mbali mbali ya TEHAMA ya kutatua changamoto za wananchi ila wanakosa mazingira wezeshi ya kuendeleza na kukuza bunifu zao kama vile kupatiwa muda maalumu wa kuingiza sokoni bunifu zao kwa kufanya majaribio ya bunifu hizo kukubalika kwa wananchi bila kulazimika kulipia gharama za usajili, kupata masoko, malipo ya kodi na leseni kuendana na matakwa ya uendeshaji wa kampuni na biashara nchini

Amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuendeleza wabunifu wa TEHAMA ili waweze kutengeneza mifumo kuendana na mahitaji ya wananchi badala ya kuendelea kununua mifumo hiyo kwa gharama kubwa kutoka nje ya nchi ambapo Serikali inatumia fedha nyingi kununua mifumo ya TEHAMA

Amefafanua kuwa utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA hapa nchini utaongeza wigo wa matumizi ya intaneti na huduma za mawasiliano na itajibu changamoto za wananchi na ametoa rai kwa watanzania kujenga imani ya kutumia teknolojia rahisi zinazobuniwa na vijana wa ndani ya nchi bila kujali umri, uzoefu au majina ya kampuni zao

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema kuwa vijana haom wameanzisha kampuni zaidi ya 20 za mifumo ya TEHAMA na tayari mifumo hiyo inasaidia kukusanya kodi kwenye halmashauri; kuwawezesha vijana kusoma VETA kwa njia ya mtandao na TIGO kuweza kuhifadhi taarifa za wateja wake

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, utafiti na ubunifu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Benadetha Kiliani na Mkuu wa Ndaki ya TEHAMA ya Chuo hicho, Dkt. Mussa Kisaka wamesema kuwa Chuo kiko tayari kushirikiana na Wizara ili kuendeleza vijana wabunifu na watafiti wa TEHAMA nchini

Akizungumza kwa niaba ya vijana wabunifu wa TEHAMA, Geofrey Magila ameiomba Serikali kuwawezesha wakubalike na kuaminika na wapewe kazi badala ya kampuni zao kufanya kazi kwa kutumia mgongo na majina ya kampuni nyingine kwa kuwa kampuni zao ni changa na hazina mtaji wa kutosha kuingia kwenye ushindani wa zabuni zinazotangazwa zinazohusu mifumo ya TEHAMA

“Tulipata kazi kutoka kampuni ya AIS ya simu za mkononi ya Malyasia yenye wateja zaidi ya milioni 50 ambao walituamini na tuliwatengenezea mifumo ya kulinda taarifa za wateja wao, ndipo baadae baadhi ya kampuni za ndani ya nchi zikaanza kutuamini,” amesema Magila

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari




Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi January 2



Share:

Friday 1 January 2021

AJIFUNGUA KANISANI KWENYE MKESHA WA MWAKA MPYA 2021 MWANZA

Na Daniel Makaka - Mwananchi
 Priska Isaya (33) makazi wa kijiji cha Kanyala wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza amejifungua mtoto wa kike akiwa anahudhuria ibada ya mwaka kwenye Kanisa ya AICT jana. 

Akizungumzia tukio hilo kanisani hapo, mchungaji wa kanisa hilo Isaka Yasini amesema mwanamke huyo alifikia kanisa kuhudhuria ibada hiyo huku ikiwa ni mara yaka ya kwanza. 

Amesema alipokuwa akiongoza ibaada hiyo alimuona mama huyu akiwa amekaa chini na alipofika kumuuliza alimwambia anaumwa uchungu.

Asema wakiwa kwenye harakati za kuona namna ya kumpeka zahanati kupata hudumua mama huyu ilichukuwa dakika tano ajifungulia kanisani na hali yake inaendelea vizuri.

Mmoja wa wanawake waliomsaidia Priska aliyejitambulisha kwa jina la Kefreni Barnaba amesema alitumia dakika tatu kufuata uzi duka liliko karibu na kanisa hilo kwa ajili ya kumufunga kitovu mtoto aliyezaliwa .

Amesema kutokana na tukio hilo Mungu ana makusudi yake hivyo tunapaswa kumshukuru kwa kila kila Jambo na kuwataka wananchi kusali kwa bidii. 

Akisimulia tukioa hilo Priska amesema kuwa yeye baada ya kupata ujauzito mume aliyempa alimkimbia na kwa sasa hajulikani aliko.

Baaada kuona hivyo aliishi maisha ya kutangatanga akiwa kisiwa cha Kasalazi kilichopo katika ziwa Victoria, huku akiomba msaada kwa wasamaria mema kutokana na maisha magumu aliyokuwa nayo baada ya kukimbia na mume.

Mwanamke huyo aliyesema amebadilisha jina lake kutoka Hadija Abubakari na kutumia jina la Priska Isaya amesema Desemba 31, 2000 alivuka kutoka kisiwa cha Kasalazi kilichopo ziwa Victoria na kwenda Kijiji cha Kanyala.

Amesema akiwa huko alikwenda kanisani lengo lilikuwa kuomba msaada na alipofika uchungu ulianza kuuma na kujifunza akiwa kanisani.

"Nyumbani kwetu ni Kagera Wilaya ya Muleba ndiko aliko mama yangu, baba yangu aliishafariki,” amesema Priska. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyala Gacha Paul amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa mchungaji alifika kanisani hapo na kuwashukuru wote waliotoa msaada kwa mtu huyo ambapo waliokoa maisha yake na kuitaka jamii kuwasaidia kwa kila jambo.

Kwa sasa Priska amehifadhiwa kwa mama Kefrini Barnaba akipatiwa hudumu huku waumini wa kanisa hilo.


Share:

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA MHE. NDEJEMBI APONGEZA MCHANGO WA TASAF KATIKA KUPAMBANA NA UMASKINI NCHINI



‘’Karibu kwetu Mhe.Naibu Waziri Deogratus Ndejembi’’…. hivi ndivyo Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus mwamanga anavyomkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipotembelea ofisi za Mfuko huo mjini Dodoma.
***
Na Estom Sanga- Dodoma 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF umeendelea kuwa kichocheo muhimu katika kupiga vita umaskini nchini na hivyo kuutaka Uongozi wa Mfuko huo kuboresha zaidi huduma zake ili ziwafikie wananchi wanaozihitaji kwa ufanisi zaidi. 

Mhe.Ndejembi amesema kutokana na mchango wake muhimu katika kupiga vita dhidi ya umaskini , Serikali imeendelea kuuamini Mfuko huo na kuupa fursa ya kupata fedha ili uweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi. 

Ametoa rai hiyo mjini Dodoma alipotembelea ofisi za TASAF na kukutana na Watumishi wa Mfuko huo walioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake , Ladislaus Mwamanga akiwa katika ziara ya kujitambulisha na kuona utendaji kazi wa taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Magufuli mwanzoni mwa mwezi uliopita. 

Aidha Mhe. Ndejembi ameuagiza Uongozi wa TASAF kufanya tathmini za huduma zitolewazo na mfuko huo mara kwa mara ili kujiridhisha ikiwa Walengwa wake wanatumia vizuri fursa zitolewazo na pale inapobainika kuwa Walengwa wanakiuka misingi ya kuanzishwa kwake hatua madhubuti zichukuliwe mara moja. 

Akitoa taarifa ya utendaji kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga ameeleza namna Mfuko huo ulivyosaidia jitihada za Serikali za kuwahudumia wananchi hususani wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri . Amesema kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Walengwa wamefanikiwa kuboresha makazi yao, kusomesha watoto , kupata huduma za Afya kwa uhakika baada ya kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii,kuanzisha miradi ya kiuchumi na kujiongezea kipato. 

Bwana Mwamanga pia amesema kuanzia mwaka huu TASAF itaanza kutekeleza maagizo ya Rais Mhe. Dr. John Pombe Magufuli ya kuwafikia wananchi watakaokidhi vigezo vya umaskini uliokithiri katika mitaa, vijiji na shehia kote nchini. 

Adha Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha Mfuko huo kupata fedha za ndani na Wafadhili jambo ambalo amesema limeupa nguvu zaidi ya kuwafikia Walengwa nchini kote kwa wakati na kuwa sekta za elimu, afya na maji pia zitapewa msukumo katika utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF. 

Kuhusu uhakiki wa Walengwa Mwamanga amesema suala hilo ni endelevu na limekuwa likitekelezwa kila baada ya miezi miwili ili kuondoa uwezekano wa kunufaisha watu ambao hawajakidhi vigezo vya Mpango.
Picha ya juu na chini Mhe. Ndejembi akiwa katika picha na baadhi ya Watumishi wa TASAF mjini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Mfuko huo.


Share:

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AWATAKA WAZAZI, MAAFISA USTAWI KUWA KARIBU NA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

 


 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (aliyevaa miwani) akikabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu, Halmashauri ya Ikungi, mkoani Singida.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa kituo hicho Padre Tom Ryan, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.

 Dk. Jingu akifurahi kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa kituo hicho.
 Dk. John Jingu (kushoto) akisalimiana na Diwani wa Siuyu Celestine Yunde, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.
Dk. John Jingu (kulia) akizungumza na watendaji mbalimbali walioshiriki katika hafla hiyo ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.

Na Dotto Mwaibale,  Singida

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu, amewataka wazazi wanaoishi na watoto wenye changamoto za ulemavu wa aina mbalimbali kuwathamini sanjari na kuwapa matunzo stahiki katika malezi na makuzi yao.

Jingu aliyasema hayo alipotembelea na kutoa zawadi za bidhaa mbalimbali na chakula kwa watoto wa Kituo cha Walemavu Siuyu, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani hapa juzi

“Wazazi wawathamini watoto bila kujali hali zao. Kuna baadhi wanawaleta watoto kwenye vituo na kisha kuwatelekeza…hii haikubaliki ni lazima tuzingatie haki za msingi za malezi na makuzi ya watoto hususani watoto hawa wenye ulemavu,” alisema Jingu.

Aidha, aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuongeza kasi ya kuhakikisha wanawatangamanisha watoto na wazazi wao-sambamba na jamii katika muktadha wa kubadili fikra, mtazamo ili kuleta ustawi wa watoto hususan wale wenye aina mbalimbali za ulemavu katika ngazi zote bila kubagua.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, kituo hicho cha Siuyu ni miongoni mwa vituo vyenye sifa stahiki za utoaji wa huduma za malezi kwa watoto, ikiwemo usalama wa kutosha sambamba na walimu waliosomea elimu maalumu ya watoto wenye ulemavu, huku akiwataka viongozi wa vituo vingine nchini kuzingatia matakwa ya kisheria katika uendeshaji wa huduma za usajili wa vituo vyao.

“Moja ya majukumu yetu ni kuvisajili na kuhakikisha vituo hivi vinafanya kazi sawasawa. Hivyo nimekuja hapa kutembelea kituo hiki kwa lengo la kukagua lakini nimeona pia nitoe zawadi kwa watoto hawa ambazo ni bidhaa na chakula,” alisema Jingu.

Hata hivyo, Diwani wa Kata hiyo, Selestine Yunde, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kutembelea kituo hicho huku akimsihi kuangalia namna ya uwezekano wa serikali kuanza kutenga bajeti za kuhudumia vituo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Padre Tom Ryan, alisema ziara ya viongozi wa serikali akiwamo Jingu hutafsiri faraja, ustawi na kuchagiza ustawi na furaha kwa watoto hawa. “Tunaona fahari kwa kutiwa moyo na hamasa kupitia zawadi hizi,” alisema.

Huku mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Raymond Daudi, mbali ya kushukuru, aliomba mamlaka ndani ya serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wenye ulemavu, hususan wahitimu wa darasa la saba kwa kuwatengenezea mazingira ya kujipatia kipato badala ya kuwaacha bila ya msaada wowote.

Awali, akisoma taarifa ya kituo hicho, Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Paul Sangalali, alisema kituo hicho cha Siuyu, kilichopo wilaya ya Ikungi mkoani hapa kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Ulaya na Marekani na kilifunguliwa Februari 2007 na aliyekuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Desderis Rwoma.

Hata hivyo, Sangalali alisema mbali ya mafanikio yaliyopo, kituo kinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhitaji wa baiskeli kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa viungo, uhitaji wa chakula, sabuni, mashuka na fedha kwa ajili ya nauli ya kuwarudisha watoto nyumbani wakati wa likizo.

“Pia miundombinu yake sio rafiki sana hasa pale watoto wanapokuwa wakielekea shule ya msingi Siuyu, na kuna ushirikiano hafifu kwa wazazi kuchangia shilingi laki moja za huduma kwa kila mwaka…lakini watoto wanapokuwa likizo nyumbani hawapati mazoezi kwa wazazi hivyo wakirudi kituoni walimu hulazimika kuanza upya kufundisha,” alisema Sangalali. 

Share:

Breaking : BENARD MEMBE AIPIGA CHINI ACT WAZALENDO


Aliyekuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo na mshauri wa Chama hicho, Bernad Membe leo Januari 1,2021 ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi zake zote ndani ya chama hicho.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 ametangaza uamuzi huo leo akiwa nyumbani kwake kijijini Rondo Chiponda, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi ambapo amesema hajafanya uamuzi huo kwa shinikizo lolote na kwamba kwa sasa atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali yanayoihusu nchi ya Tanzania na kupigania demokrasia ya kweli.

Mwanadiplomasia huyo alitangaza kuhamia Chama cha ACT Wazalendo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2020 baada ya kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), tarehe 10 Julai 2020.

Membe alifukuzwa kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya CCM, pamoja na kuonywa mara kadhaa, pasina kubadilika.

Baada ya kuhamia ACT Wazalengo, Membe alitangaza kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Akijiunga ACT Wazalengo Membe alisema ; “Kwa hiari yangu nimeamua kujiunga katika familia kubwa ya ACT Wazalendo inayotaka mabadiliko yenye lengo la kuwanufaisha Watanzania wengi hasa wakulima, wafanyabiashara, watumishi wa serikali, wafanyakazi mbalimbali na wote wanaoitakia kheri Tanzania yetu. Nataka kupigania mabadiliko ya kweli ya hii nchi kupitia ACT na azma yangu itatimia".

Hata hivyo kuliibuka migogoro ndani ya chama hicho baada ya Viongozi wa ACT Kutangaza kumuunga mkono Mgombea Urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu licha ya Membe kuwa mgombea Urais kupitia ACT Wazalendo.

Ijumaa Oktoba 16, 2020 Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alitangaza kumpigia kura mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni mjini Kigoma.

Mbali na Zitto, Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kutangaza kuwa chama hicho kitamuunga mkono Lissu katika Urais ambapo pia Lissu pia aliwahi kutangaza kuwa Chadema itamuunga mkono Maalim Seif katika urais wa Zanzibar.

Hata hivyo Membe alisisitiza kuwa yeye ni mgombea halali wa Urais kupitia ACT Wazalendo.

“Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa”,alisema.
Share:

Picha : KATAMBI ASHEREHEKEA SIKUKUU YA MWAKA MPYA 2021 NA WATOTO WENYE UALBINO BUHANGIJA...ATUMA SALAMU ZA JPM NA KUTOA ZAWADI


Katikati ni Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Buhangija kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. 

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) amesherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021 kwa kuwatembelea na kuwapatia zawadi watoto wenye ualbino wanaolelewa katika kituo cha Buhangija Mjini Shinyanga. 

Mhe. Katambi ametembelea watoto hao leo Ijumaa Januari 1, 2020 akiambatana na Katibu wa Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mkama Nyamwesa, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakari Gulam na Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya ya Shinyanga Mjini, Raphael Nyandi. 

Miongoni mwa zawadi zilizotolewa na Mhe. Katambi kwa watoto ni pamoja na unga wa ngano, sukari, madaftari, kalamu,chumvi, sabuni na juisi huku akiwapa motisha walimu walezi wa watoto hao. 

Akizungumza, Katambi amesema lengo la ziara yake katika kituo cha kulelea watoto cha Buhangija ni kuwapa salamu za Mwaka Mpya 2021 kutoka kwa viongozi Wakuu wa nchi wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. 

“Lengo la mimi kufika hapa ni kuwapa watoto salamu za Mwaka mpya 2021 za Rais wetu Mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa”, amesema Katambi. 

Amesema lengo jingine ni kufuatilia maendeleo ya kituo cha kulelea watoto cha Buhangija, kutatua changamoto za kituo hicho na kuwapa watoto zawadi mbalimbali za Mwaka Mpya 2021 na kuwapa motisha walimu walezi wa wanafunzi hao. 

Mhe. Katambi amebainisha kuwa Serikali inatoa kipaumbele na kuyajali makundi maalumu ya watu (wenye uhitaji maalumu) katika jamii wakiwemo watoto wenye ulemavu, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. 

Katika hatua nyingine, Katambi ametoa wito kwa wadau na wananchi kwa ujumla wajitokeze kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji kama vile mafuta maalumu kwa ajili ya watoto wenye ualbino, nguo na chakula akidai kuwa hiyo ndiyo Sadaka, Sala na Dua ya kweli kwa Mungu yenye majibu ya neema. 

Mmoja wa watoto hao kwa niaba ya wenzake, Kwandu Masunga amemshukuru Mhe. Katambi kwa kusherehekea nao Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021 na kuwaomba wadau wengine kutembelea kituo hicho kwani wanafarijika na kufurahi wanapopata wageni. 

Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha Kulelea watoto cha Buhangija, Mwalimu Suleiman Kipanya amesema kituo hicho sasa kina jumla ya watoto 225 ambapo kati yao wenye ualbino ni 131, wasiosikia (viziwi) 74 na wasioona 20.
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akizungumza katika kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu cha Buhangija Mjini Shinyanga leo Ijumaa Januari Mosi ,2020 kwa ajili ya kuwapa zawadi ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakari Gulam, mtoto Kwandu Masunga na Katibu wa Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mkama Nyamwesa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa kituo cha Buhangija, Selemani Kipanya. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akizungumza katika kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu cha Buhangija Mjini Shinyanga leo Ijumaa Januari Mosi ,2020 kwa ajili ya kuwapa zawadi ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. 
Mtoto Kwandu Masunga akimshukuru Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) kwa kutembelea kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu cha Buhangija Mjini Shinyanga leo Ijumaa Januari Mosi ,2020 na  kuwapa zawadi ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. 
Muonekano wa sehemu ya zawadi za Mwaka Mpya 2021 zilizotolewa na Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) leo Ijumaa Januari Mosi ,2020 kwa ajili ya watoto katika kituo cha Buhangija ili kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. 
Katikati ni Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Buhangija kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa kituo cha Buhangija Selemani Kipanya. Wa kwanza kulia ni Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Raphael Nyandi akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakari Mukadam.
Katikati ni Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Buhangija kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa kituo cha Buhangija Selemani Kipanya. Wa kwanza kulia ni Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Raphael Nyandi akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakari Mukadam.
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) na msafara wake akipiga picha ya kumbukumbu na watoto na walimu katika kituo cha Buhangija.
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) na msafara wake akipiga picha ya kumbukumbu na watoto na walimu katika kituo cha Buhangija.
Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM) akipiga stori na mmoja wa watoto katika kituo cha Buhangija huku amembeba wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021 leo Januari 1,2021.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa January 1, 2020



Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger