Thursday 2 July 2020

DKT. NCHIMBI AMPA TANO RAIS KWA KUIINGIZA TANZANIA UCHUMI WA KATI


 Mkuu wa MKoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifunga  mafunzo maalum ya  siku sita kwa wadau zaidi ya 300 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini  yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa  la watu wanaoishi na  virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge” unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2019-2024, unaofadhiliwa na  Shirika la Marekani  la  Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara. kushoto Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa, Kulia Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA  Pantaleo Shoki


Na John Mapepele

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amempongeza Rais Magufuli kwa kuvunja rekodi ya  maendeleo kabla ya mwaka 2025 na kuifanya Tanzania kuingia kwenye nchi za uchumi wa kati duniani Julai Mosi mwaka huu.  

Huku akiwahimiza watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini  kufanya kazi kwa  bidii bila kuwa na hofu sambamba na kumtanguliza Mungu na kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano ili  ku kuinua hali za maisha na kuongeza pato la taifa kwa ujumla



Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo katika Mji Mdogo wa Manyoni mkoani  Singida alipokuwa akifunga  mafunzo maalum ya  siku sita kwa wadau zaidi ya mia 3 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini  yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa  la watu wanaoishi na  virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge”.

Mradi huo unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2019-2024,unaofadhiliwa  na  Shirika la Marekani  la  Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara.



Amesema kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imepiga hatua kubwa ya kupiga vita unyanyapaa dhidi ya watu wanaishi na virusi vya UKIMWI na kwamba watu wote wana haki na fursa sawa  mbele ya Serikali yao hivyo hakuna sababu ya  wao kuendelea kujinyanyapaa  wenyewe  na badala yake wawe walimu wa kuwaelimisha wengine kwenda kupima na kutambua hali zao  na kuendelea kuchapa kazi ili kuinua uchumi wan chi yetu.



“Kubwa ndugu zangu hapa ni  kumtanguliza  Mungu mbele, kutoa hofu na  kuachana  na mambo yote ambayo yanapelekea  kudhoofu kwa afya zetu kama vile unywaji wa pombe  hata kama wake zetu wanapika  kwa ajili ya biashara na badala yake tutumie juisi lishe za matunda ya asili kama vile  Sasati, Ubuyu na Ukwaju” amesisitiza Dkt. Nchimbi



Umewaelekeza  Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Singida kuangalia namna  ya kuja na mikakati madhubuti ya kiuendelevu ya kuwakopesha wanaoishi na UKIMWI  ili kuwaletea maendeleo huku akisisitiza kuwa  Mkoa wake utaendelea kutekeleza mikakati iliyojiwekea ya kuinua maisha  ya wanainchi wake ikiwa ni pamoja na mkakati wa kuwavusha salama mama na mtoto.



Aidha ameweka msimamo wake wa kutokuonesha nia yeyote ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu huku akiwaonya watu ambao wamekuwa wakianza kudanganya kuwa atagombea ambapo alisisitiza kuwa nafasi hiyo ya ukuu wa Mkoa aliyopewa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ni ya heshima kubwa.





“Naomba niliseme  hili, na tayari nimeshalisema mara kadhaa  hata hivi karibuni nilipokuwa nyumbani kwangu, kijijini Matufa,  Babati Manyara nilipo hudhuria mazishi ya mtoto wa Kaka yangu aliyefariki kwa ajali ya Pikipiki kwamba nilikwenda kuungana na familia yangu katika msiba wa kijana wetu na si vinginevyo. Ninaridhika sana na nafasi hii niliyo nayo ya ukuu wa Mkoa" alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na umati wa  wadau wa mafunzo hayo



Baadhi ya waombolezaji wamesikika kupongeza msimamo wa kiongozi huyo, huku wakisema  kuwa Msimamo huo unapaswa kuigwa na viongozi wengine  kwa kuwa umejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi badala ya kuwa na tamaa za madaraka.



“Binafsi nampongeza sana Mama Nchimbi  kwani kwa muda wote amekuwa aking’ang’ana na kuwaunganisha watu wote bila kujali dini wala rangi kwa, hata sisi leo ametutia moyo sana kiasi kwamba  baada ya kutoka hapa tumekuwa na nguvu mpya  ya kuchapa kazi na kushirikiana na Serikali yetu ya  kujiletea maendeleo Zaidi ili tutoke katika nchi za uchumi wa kati na kwenda katika nchi tajiri duniani na tuna imani kubwa chini ya Rais wetu Magufuli tutafika” amesema Amina  Huredi ambaye ni Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Singida



Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA  Pantaleo Shoki  amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumhakikishia kuwa  wataendelea kushikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mradi huo yanatimia kama yalivyopangwa.


Shoki  amesema Mradi  unalenga kufikia Mkakati wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI(UNAIDS) wa 95-95-95 yaani  asilimia 95 ya watu wote wanaoishi na maambukizi ya VVU wawe wamepima na kugundua afya zao,asilimia 95 ya watu wote waliopimwa na kukutwa na maambukizi wawe wameanza tiba na asilimia 95 walio kwenye tiba wawe wamefubaza virusi hivyo ifikapo 2030
Share:

WATANZANIA 44 WALIOKWAMA AFRIKA KUSINI KWA LOCKDOWN WAREJEA NCHINI TANZANIA

Na Mwandishi Maalumu
Leo Julai 1, 2020 Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi kwa mara ingine amesimamia zoezi la usafirishaji wa dharura (repatriation) ya Watanzania pamoja na raia kadhaa wa nchi hiyo waliokwama nchini humo kutokana na "Lockdown" na kusitishwa safari za ndege inayoendelea huko.

Balozi Milanzi amesimamia zoezi hilo lililohusu usafirishwaji wa jumla ya abiria 60, ikiwa ni Watanzania 44 na raia wa Afrika Kusini 16, ambao wanarudi kufanya kazi kwenye makampuni na taasisi za nchi hiyo baada ya kukwama huko kwa miezi kadhaa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania nchini humo, abiria hao wamesafirishwa kwa ndege ya kukodi ya kampuni ya Precision Air, hilo likiwa na zoezi la nne kufanyika nchini humo tokea ugonjwa wa COVID 19 uikumbe dunia na kupelekea nchi nyingi duniani, ikiwemo Afrika Kusini, kusimamisha kila kitu ikiwemo safari za kuondoka nchini mwao.

Tayari Tanzania imeshafungua anga lake na kuruhusu utalii pamoja na safari za ndege za kimataifa viendelee kama kawaida, ambapo tayari mamia ya watalii wameendelea kumimimika nchini, huku wengine wakitarajiwa kuwasili kwa wingi baada ya mashirika ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari zao.

 
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi akiagana na Watanzania pamoja na rais wa Afrika Kusini wakati aliposimamia zoezi la kuwasafirisha kwa dharuran katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa O.R. Tambo jijini Johannesburg leo. Chini ni taswira mbalimbali za abiria hao wakielekea kupanda ndege kurejea Tanzania leo. 
Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO ALHAMIS JULAI 2,2020


















Share:

Wednesday 1 July 2020

RC MTAKA AONGOZA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA KIBASO ALIYEKUWA MWALIMU KWAYA YA SDA KURASINI



Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Picha inayomuonesha Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini marehemu mwalimu Samson Kibaso akipiga gitaa enzi za uhai wake.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso likishushwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso likishushwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kulia) akiteta jambo na Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark Malekana katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiimba na pamoja na baaadhi ya waimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini kabla ya mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya hiyo mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark Malekana akitoa mahubiri katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
***
Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewaongoza mamia ya waomboleaji kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mara, Mwanza, Simiyu na nchi jirani ya Kenya katika mazishi ya aliyekuwa mwalimu na mwimbaji wa Kwaya ya Kanisa la Wadventista Wasabato (SDA) Kurasini, Mwl.Samson Kibaso ambaye pia ni mtunzi wa wimbo wa Jumiya ya Afrika Mashariki.

Mazishi hayo yamefanyika Juni 30, 2020 katika Kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara na kuhudhuriwa na viongozi wa Kitaifa wa Kanisa la SDA, Wachungaji kutoka konferensi mbalimbali za Kanisa hilo pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .

Akizungumza na waombolezaji, Mtaka amesema Mwalimu Samson Kibaso amefanya kazi kubwa ambayo imeacha alama ya utumishi wake si tu katika Kanisa la Waadvenista Wasabato(SDA) bali hata katika madhehebu mengine ambayo amefanya kazi nayo kupitia kazi yake ya utunzi wa nyimbo.

“Yapo maandiko yanasema hubirini kwa sauti ya kuimba, kupitia yeye (Kibaso) ameongoa wengi, amegusa wengi, tuna wachungaji ambao wangeweza kufa ndani ya kanisa wanaofahamika kimataifa lakini wasingetoka watu Kenya wakaja hapa; wote tunajua kuna shida ya kusafiri lakini kuna watu kutoka Kenya wakasema lazima wafike kuona safari ya mwisho ya huyu mtu mwema,” alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema atakuwa tayari kushiriki katika mambo ambayo Kanisa litayafanya kwa kumuenzi Mwalimu Samson Kibaso huku akibainisha kuwa heshima aliyopewa Mwalimu Kibaso inabeba taswira ya namna kazi ya Kwaya ya Kurasini inavyopokelewa na watu.

Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuthamini elimu kwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili wapate elimu huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo inaweza kuwawafanya wakashindana na watu kutoka maeneo mengine.

Akitoa mahubiri kabla ya mazishi ya Mwalimu Kibaso, Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark Malekana amemzungumzia Kibaso kuwa alikuwa na mchango mkubwa kwa kanisa, mtu mnyenyekevu pamoja na kipaji alichokuwa nacho, hivyo akatoa wito kwa waimbaji na walimu wengine kuacha kiburi na kutumia vipaji vyao kwa utukufu wa Mungu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mwita Waitara ametoa pole kwa familia, kwaya ya Kurasini na Kanisa la SDA na kubainisha kuwa anatambua kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Samson Kibaso hivyo atakuwa tayari kushirikiana na familia, kwaya na kanisa katika kuenzi kazi zake.

Nao wanakwaya wa Kwaya ya SDA Kurasini wamesema wamempoteza, nguli wa muziki, mwalimu mahiri wa uimbaji na rafiki yao, huku wakiahidi kumuenzi kwa kuendelea kumuimbia Mungu ili kupitia uimbaji wao watu waendelee kumuona Mungu.

Mwalimu Samson Kibaso alizaliwa mwaka 1956 na amekuwa mwalimu wa kwaya ya SDA Kurasini tangu mwaka 1985, ambapo pamoja na kuwa mwalimu katika Kwaya ya SDA Kurasini Kibaso pia amefundisha kwaya ya madhehebu mbalimbali kama KKKT, Anglican na Moravian.

Pia alitunga na kufundisha nyimbo za taasisi mbalimbali ikiwemo muhimili wa mahakama pamoja na kutunga wimbo wa jumuiya ya Afrika Mashariki ambao mpaka sasa umekuwa ukiimbwa katika nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo.

Share:

TAMWA YAFURAHISHWA UTHUBUTU WA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI UCHAGUZI MKUU 2020 ZANZIBAR

Share:

Breaking : TAKUKURU SHINYANGA YAMKAMATA KADA WA CCM AKIGAWA RUSHWA YA MASHUKA, NDALA KWA WAJUMBE WA UWT

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa akionesha mashuka kitenge kimoja, ndala zinazodaiwa kuwa za  Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga alizotaka kuzigawa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake CCM  (UWT). 

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 
Wakati joto la uchaguzi likiendelea kushika kasi,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga linamshikilia Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa CCM, Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT). 

Kwa Mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari ilitolewa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa leo Jumatano Julai 1,2020 Asha Mwandu Makwaiya alikamatwa Juni 28,2020. 

“TAKUKURU katika ufuatiliaji wa vitendo vya Rushwa kuelekeza kipindi hiki cha uchaguzi ilimkamata Bi. Asha Mwandu Makwaiya ambaye ni mkazi wa Majengo Mapya Shinyanga Mjini na Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa akiwa nyumbani kwa Elizabeth Donald Itete ‘Mama Buzwizwi’ ambaye ni Katibu wa UWT tawi la Mshikamano pamoja na wajumbe wengine 10 ambao ni viongozi wa UWT kata ya Ngokolo”,amesema Mussa. 

“Bi. Aisha Mwandu Makwaiya alitaka kugawa mashuka 10, kitenge kimoja, ndala 11 kwa wajumbe 11 wa umoja wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) kata ya Ngokolo kama kishawishi cha yeye kuchaguliwa au kuchaguliwa kwa aliyemtuma”,ameongeza Mussa. 

Aidha amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU kama ambavyo wamekuwa wakifanya ili kuhakikisha kuwa kero ya rushwa katika mkoa wa Shinyanga inaondolewa mkoani Shinyanga hasa katika kipindi hiki cha michakato ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Share:

RAIS MAGUFULI AWASHUKURU WALIOMDHAMINI, ASEMA ANA DENI KUBWA

Na Richard Mwaikenda,Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM), Dk. John Magufuli amewashukuru sana wote waliojitokeza kumdhamini kwa kujaza fomu za kuomba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2020, kupitia chama hicho.

Shukrani hizo alizitoa mara baada ya kurejesha fomu Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma, ambapo kwa kitendo hicho cha kudhaminiwa na zaidi ya wanachama milioni moja wa Tanzania Bara na Visiwani, amesema kinamfanya awe na deni kubwa kwao.

Pia, Dk. Magufuli aliwapongeza Wenyeviti wa CCM wa mikoa yote 32 kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kufanikisha udhamini huo mkubwa, licha ya kupata lawama nyingi kwa waliojitokeza kudhamini lakini walikosa fursa hiyo.

Aliwaomba wanachama waliokuwa na nia hiyo, wasivunjike moyo bali udhamini huo wauweke kwenye kura endapo mikutano husika ya chama itampitisha kuwa mgombea urais wa Tanzania kupita chama hicho, ili akapambane na wagombea wa vyama vingine.

Pia aliwaomba wanachama wa vyama vingine wampigie kura wakati wa kinyang’anyiro hicho, ili awatumikie Watanzania kutimiza malengo waliyojiwekea pamoja na kukamilisha miradi mbalimbali waliyoianza katika Serikali ya Awmu ya Tano inayoongozwa na yeye, ikiwemo ya Reli ya Kisasa ya Mwendo Kasi (SGR), Mradi mkubwa wa umeme wa Mwalimu Nyerere Rufiji na miradi mingine mingi.

Kabla ya kurejesha fomu, lilifanyika tukio la wenyeviti wa mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani kukabidhi fomu za waliomdhamini kutoka katika mikoa hiyo. Pi wenyeviti wa Jumuiya za chama hicho; Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Umoja wa Wazazi Tanzania na Umoja wa Vijana (UVCCM), walikabidhi fomu za waliomdhamini Dk. Magufuli.


Share:

ZITTO KABWE NA WENZAKE 07 WARIPOTI POLISI LINDI , WATAKIWA KUREJEA TENA JULAI 20

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo , Zitto Kabwe na viongozi wengine saba wa Chama hicho wameripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mkoani Lindi kama walivyohitajika.

Zitto pamoja na viongozi wengine akiwemo Mbunge wa Kilwa Kusini aliyemaliza muda wake, Suleiman Bungara walikamatwa na Polisi Wilayani Kilwa Juni 23, 2020 kwa kile ambacho Polisi walikiita ‘kuhatarisha amani’.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu wa Kamati ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo, Janeth Rithe, viongozi hao wametakiwa kuripoti tena Polisi Lindi Julai 20, 2020.


Share:

BILIONI 13 ZATUMIKA KUBORESHA MIRADI YA ELIMU KIGOMA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Kasulu mkoani Kigoma yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 13.


Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kasulu, Chuo cha Ualimu Kabanga na jengo la Utawala la shule ya Sekondari Grand.

Akizungumzia maendeleo​ ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga mara baada ya kukagua, Waziri Ndalichako amesema chuo hicho kinajengewa upya miundombinu yote​ baada ya ile ya awali kuchakaa sana na kushindwa kukarabatiwa.
Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya​ chuo hicho unagharimu zaidi ya bilioni 10, na kuwa utakapokamilika utabadili taswira ya mji huo kwa kuwa majengo yanayojengwa ni ya kisasa na imara ambayo yatadumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala na utengenezaji wa mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Grand, Profesa Ndalichako amesema umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 534 na kwamba utakapokamilika utaongeza morali ya walimu​ kufundisha na kusaidia wanafunzi waliopo katika shule hiyo.
Mradi mwingine uliotembelewa na Waziri wa Elimu ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Kasulu ambao upo katika hatua za mwisho ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.97. Jumla ya majengo 15 yatajengwa​ na kitachukua wanafunzi 320 watakaokuwa wakilala chuoni hapo.
Waziri Ndalicahko amewataka wananchi wa wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali katika Halmashauri hiyo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa ama kujiajiri ili kujiletea maendeleo binafsi na ya mkoa wa Kigoma.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia​ kwa namna ilivyojikita katika kupanua wigo wa elimu. Amesema kuwa katika wilaya yake kuna maeneo ambayo ni ya wafugaji na watoto hawakuwa wakienda shule lakini kwa sasa zimejengwa shule shikizi katika maeneo hayo ya mbali hivyo kuwezesha watoto kusoma na kuleta matokeo chanya.
Kanali Anange amesema baada ya Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila ada kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hivyo kupelekea Serikali kupanua​ miundombinu katika ngazi zote za elimu ili kuwezesha fursa za masomo kwa wanafunzi ikiwemo na kuongeza walimu.​

Aliongeza kuwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu itawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira bora.
Naye Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu (TESP), Ignas Chonya amesema ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Kabanga awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Oktoba 2020 na chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 400 kwa wakati mmoja na kwamba chuo kinatarajiwa kuanza mafunzo mwaka huu.


Share:

RAIS MAGUFULI AMPONGEZA DK. LAZARUS CHAKWERA KWA KUCHAGULIWA KUWA RAIS MPYA WA MALAWI


Rais  Magufuli amempongeza Dk. Lazarus Chakwera  kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Malawi. 




Kupitia ukurasa wake wa Twitter; Rais Magufuli amesema, “Nakupongeza Dkt. Lazarus Chakwera kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Malawi.

“Kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote, naahidi kuendeleza uhusiano wetu wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema hususani katika masuala ya uchumi na ustawi wa jamii. Hongera sana Mhe. Rais,” amesema.

Chakwera amechaguliwa na Wamalawi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 23 Juni 2020 kwa kupata asilimia 58 akimshinda Rais aliyekuwa madarakani Peter Mutharika.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya ule wa awali wa Mei 2019 kufutwa na mahakama Februari 2020 baada ya kubaini ulikuwa na dosari.


Share:

WAZIRI UMMY ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA MTWARA


Na WAJMW-Mtwara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mikoa ya kusini iliyopo mkoani Mtwara na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

Waziri Ummy ameonekana kuridhidhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia asilimia 80 na inagharimu Shilingi Bilioni 15.8 mpaka kukamilika kwake.

"Kukamilika kwa Hospitali hii kutasaidia kupunguza rufaa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwenda kutafuta huduma za kibingwa Muhimbili, MOI au JKCI, huduma zote zitakua zinapatikana hapa". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuona huduma zinaanza kutolewa katika Hospitali hiyo kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwani ilikua ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipopita mwaka 2015 kuomba kura na Hospitali hiyo ipo kwenye utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

"Hatutaki watu wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla muende Dar Es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za CT-Scan, huduma za madaktari bingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, mishipa ya fahamu, Madaktari wa watoto na uzazi. Huduma zote hizi zitapatikana hapa mara baada ya ujenzi wa Hospitali hii kukamilika". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya sekta ya Afya mkoani Mtwara ni nzuri ambapo katika kipindi cha miaka mitano Hospitali mpya za Wilaya tatu zimejengwa ambazo ni Nanguluwe, Nanyamba pamoja na Masasi. Aidha, vituo vya Afya vinane vimejengwa katika Mkoa huo katika kipindi hicho na kufanya idadi kufikia vituo 23 kutoka 15 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani.

Share:

TARURA YAWAJENGEA DARAJA WANANCHI WILAYANI MVOMERO

Na. Erick Mwanakulya, Morogoro.

Wakazi wa Kijiji cha Digoma, kata ya Diongoya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujenga daraja la kudumu katika mto Mjonga litakalounganisha Kijiji hicho na maeneo mengine ya Wilaya ya Mvomero.




Wakizungumza katika mahojiano maalum wakazi hao wameipongeza TARURA kwa kujenga daraja hilo litakalotumiwa na watembea kwa miguu pia litapitisha na baadhi ya vyombo vya usafiri kama pikipiki na bajaji.

“Kivuko kikikamilika kitatuondolea kero ya muda mrefu kwani maji yanapojaa tunapata shida sana kupata huduma za kijamii hivyo kukamilika kwa daraja hili kutapunguza kero zetu za muda mrefu”, alisema Leonard Michael Mkazi wa Kata ya Diongoya.                                                                         

Wakazi hao wamesema kuwa kwa sasa wanatumia shilingi 1000 hadi 2000 kuvuka kwenda upande mwingine kwa kutumia mtumbwi, hivyo kukamilika kwa daraja hilo kutawasaidia sana katika usafirishaji wa mazao yao kwenda sokoni.

Naye, Mtendaji wa Kijiji cha Digoma, Ndg. Omari Nyilika alisema kuwa Daraja la Mto Mjonga ni kiunganishi cha Vijiji vya Digoma na Digalama, hivyo ukamilikaji wa daraja hilo utawasaidia wakazi hao katika shughuli zao za kijamii na kuboresha uchumi wao kwani wanategemea zao la Hiliki pamoja na Kokoa.

“Tunaishukuru sana TARURA kwa kutujengea daraja hili kwani Kijiji chetu hakikuwa na mawasiliano kwa muda mrefu kiasi kilichopelekea wananchi kupata shida kuvuka kwenda upande wa pili kufanya shughuli zao za kimaendeleo, lakini kwa jitihada za TARURA kivuko cha kudumu kimejengwa ili   kutatua kero hiyo ya muda mrefu’’, alisema Mtendaji huyo.

Naye, Meneja wa TARURA Halmashauri Wilaya ya Mvomero, Mhandisi William Lameck alisema ujenzi wa Daraja hilo umekuja baada ya mawasiliano kukatika hasa kipindi cha masika na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama na kushindwa kufanya kazi zao kwa kuwa wakazi wa Kata ya Diongoya uchumi wao mkubwa unategemea mazao ya kokoa pamoja na hiliki ili kujipatia kipato.

Ujenzi wa daraja la Mto Mjonga lenye urefu wa mita 42 umefikia asilimia 80 kukamilika na utagharimu shilingi milioni 68.1, ambapo kukamilika kwake kutawezesha wananchi kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger