Monday 29 June 2020

Ufaransa Yaipatia Tanzania Sh, Bilioni 592.57 Kutekeleza Miradi Ya Umeme Na Maji.

Na Farida Ramadhani na Ramadhani Kissimba, Dar es Salaam
Serikali ya ufaransa kupitia shirika la Maendeleo ya nchi hiyo (AFD) imeipatia Tanzania Euro milioni 230 sawa na shilingi bilioni 592.57 zikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya  kutekeleza miradi mitatu ya kipaumbele ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, alisema miradi iliyokusudiwa kutekelezwa kupitia fedha hizo ni Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA), uliopatiwa Euro milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 257.64) na utasambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.

Mradi mwingine utakaonufaika na mkopo huo ni Mradi wa Umeme wa Kuunganisha Tanzania na Zambia unaojulikana kama “Tanzania – Zambia Interconnector Project” ambao utagharimu Euro milioni 100 (sawa na shilingi bilioni 257.64) kwa ajili ya kuchangia uunganishaji wa Mashirika ya Umeme ya Kusini mwa Afrika kwa pamoja yanayojulikana kama “Southern African Power Pool” na Mashirika ya Umeme ya Afrika Mashariki kwa pamoja yanayojulikana kama “Eastern African Power Pool” na  Kazi za Nyongeza kwenye Mradi wa Maji Safi na Maji Taka katika miji inayozunguka Ziwa Victoria ambazo zitagharimu Euro milioni 30 (sawa na shilingi bilioni 77.29) na itahusisha maeneo ya Buhongwa, Kisesa na Buswelu katika jijini la Mwanza.

Pia Bw. James alimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa, uhusiano ambao umefanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta za maji na nishati.

Bw. James aliongeza kuwa miradi yote mitatu ambayo imesainiwa mikataba yake  inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025, ambayo inaongoza juhudi za kuleta maendeleo nchini hadi mwaka 2025 na kwa sasa inatekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21.

‘’Malengo ya Dira yetu ni kuinua, kuratibu na kuelekeza juhudi za Watanzania, fikra na rasilimali za Taifa kwenye sekta muhimu ambazo zitawezesha nchi kufikia maendeleo na kuhimili ushindani mkubwa wa kiuchumi unaotarajiwa’’. Alisema Bw.James.

Alilishukuru Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa kuwa licha ya kuisaidia Tanzania kiasi cha Euro milioni 230 wameonyesha nia ya kutoa mikopo mingine yenye masharti nafuu na misaada ambayo inafikia jumla ya Euro milioni 721.7, sawa na shilingi trilioni 1.86 ambazo zitatumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo program ya Maendeleo ya umeme  jua, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, Uboreshaji wa Huduma za Kifedha kwa ajili ya Kilimo, Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam (BRT Awamu ya Tano), Mradi wa Usafi wa Mazingira jijini Dar es Salaam, Mradi wa Nishati wa Kuunganisha Tanzania na Uganda na Mradi wa Nishati wa Kuunganisha Tanzania na Zambia.

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo aliwashukuru wahisani hao na kusema kuwa baada ya kukamilika kwa mchako mrefu wa makubaliano kati ya Tanzania na Ufaransa na kupatikana kwa fedha hizo, Wizara yake itatekeleza mara moja miradi hiyo na kuwahakikishia wananchi kuwa miradi hiyo itakamilika kwa wakati uliopangwa.

Profesa Mkumbo aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuwa mstari wa mbele kwa kuthamini rasimali za Tanzania hivyo kuamua maji ya ziwa Victoria kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Awali Mheshimiwa Frederic Clavier, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania alisema mkopo uliosainiwa pamoja na mambo mengine una madhumuni ya kusaidia uendelelezaji wa mradi wa umeme vijijini na utatekelezwa katika Mikoa kumi na sita na kukamilika kwake kutasaidia kuwaunganishia umeme familia zipatazo 90,000.

Mwisho


Share:

Prof. Palamagamba Kabudi 'Autaka Ubunge' Kilosa

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi amesema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa jimbo la kilosa iwapo watamhitaji kwenda kufanya hivyo.

Kabudi ameonyesha nia hiyo leo tarehe 29 Juni 2020 wilayani Kilosa, wakati akihutubia katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa mahandaki manne yenye urefu wa kilomita 2.7 ya reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutupora.

Licha ya kwamba hakutaja hadharani nia ya kugombea ubunge Kilosa, Profesa Kabudi amesema, kama atapata kibali kutoka kwa Mungu, hatakataa kuwa mtumishi wa wananchi wa Kilosa.

 
“Mimi ni kijana wenu, mzaliwa wa hapa na niwaambie kuwa mkinihitaji kuwatumikia niko tayari” amesema Kabudi.


Share:

Iran Yatoa Waranti Ya kukamatwa Rais wa Marekani Donald Trump

Iran imetoa waranti wa kukamatwa Rais wa Marekani Donald Trump na wanajeshi 35 wa Marekani, ikiwa ni pamoja na maafisa kutoka taifa hilo kwa kuhusika na kifo cha Jenerali Qassem Soleimani.

Iran pia imeomba msaada wa polisi ya kimataifa ya Interpol kuhusu faili hiyo, ofisi ya mashitaka ya Tehran imetangaza leo Jumatatu, kulinganan nashirika la habari la FARS.

Jenerali Qassem Soleimani alikuwa mkuu wa kikosi cha Quds, kitengo cha Walinzi wa Mapinduzi wa Irani, aliuawa mwezi Januari mwaka huu katika shambulio la anga la Marekani nchini Iraq kwa ombi la haraka la rais Donald Trump.

Waranti huo umemuhusisha Trump kwa "mauaji" na "hatua ya ugaidi," amebaini mwendesha mashtaka wa Tehran Ali Alqasimehr, akinukuliwa na shirika la habari la FARS.

Ameongeza kuwa Iran imeomba polisi ya kimataifa, Interpol, kutoa "notisi nyekundu" dhidi ya Donald Trump na wengine ambao Tehran inaona kuwa walihusika katika kifo cha Qassem Soleimani.

Washington inamshutumu Qassem Soleimani kwa kupanga njama za kufanya mashambulizi dhidi ya kambi za muungano wa kijeshi unaoongowza na Marekani nchini Iraq.

Akiwa mkuu wa kikosi cha Quds Soleimani alisimamia operesheni za kijeshi nje ya Iran na kuingia kweny euhasama na Marekani wakati wa vita vya Iraq akionekana kuwa mfadhili wa makundi ya wanamgambo wa kishia.

Marekani ilikilaumu kikosi cha Quds kwa shambulizi la Karbala lililowauwa wanajeshi wake watano pamoja na kutoa mafunzo na watengenezaji mabomu yaliyiotumika kuvilenga vikosi vyake.

Mwaka 2007 Marekani na Umoja wa Mataifa walimjumuisha Soleimani katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo lakini aliendelea kusafiri maeneo mbali mbali duniani.

Umaarufu wake uliimarika zaidi wakati wa vita vya Syria na kutanuka kwa kundi linalojiita dola la kiislam. Iran ilimtuma Soleimani mara kadhaa nchini Syria kuongoza mashambulzi dhidi ya kundi la IS na makundi yanayopinga utawala wa Bashr Al Assad.

Jenerali huyo alipata mafanikio makubwa kwenye mapambano ya ardhini na alikuwa alama ya ushindi katika vita dhidi ya IS na kuendelea kulipa nuru jina lake.

-RFI


Share:

Msanii Vitali Maembe ajiunga ACT -Wazalendo na Kutangaza Nia ya Kugombea Ubunge

Mwanamuziki  Vitalis Maembe amejiunga na Chama cha ACT-Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu
 

Maembe  amejiunga na chama hicho leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 na kukabidhiwa kadi na Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa chama hicho, makao makuu ya ACT-Wazalendo, Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Maembe amesema ACT-Wazalendo ni chama chenye sifa anazozihitaji kama vile yeye anavyojipambanua kwenye muziki wake.


Akimkabidhi kadi ya uanachama Jana jijini Dar es Salaam , Ado amemuhakikishia Maembe kuwa ACT Wazalendo litakuwa jukwaa sahihi kwake kuendeleza mapambano ya kudai haki.

Amesema, zaidi ya haki ataendelea kupinga rushwa na kupigania umoja wa Afrika kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote kupitia sanaa.

Mbali na kuchukua kadi hiyo lakini pia Maembe aliyewahi kuimba nyimbo ya “Sumu ya teja”, “vuma” ametangaza nia ya kugombea Ubunge kwenye Jimbo la Bagamoyo.


Share:

CHADEMA Yatangaza Ratiba Kwa Wagombea wa Urais, Ubunge na Udiwani Kupitia Chama Hicho

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua zoezi la uchukuaji fomu za kugombea Urais wa Tanzania, ubunge na udiwani, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020

Ratiba hiyo imetolewa leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020 na Reginald Munisi, Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema, wakati anazungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Munisi amesema, zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ya urais wa Tanzania, litafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 19 Julai 2020.

Amesema katika mchakato wa kumpata mgombea Urais wa Tanzania ndani ya Chama, mtia nia au wakala wake Julai 4,mwaka huu Chama hicho kitafungua mlango wa mtia nia au wakala wake kuchukua fomu za kugombea urais wa Tanzania kupitia Chama hicho.

Amesema fomu hizo za urais zitatolewa Makao Makuu ya Ofisi ya Chama hicho na kila mgombea atatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 100 kwa kila Kanda.

“Tunakanda 10 za CHADEMA Tanzania, nane zipo Bara na visiwani zipo kanda mbili, hivyo wagombea watapita na kuomba wadhamini katika kanda hizo na wadhamini hao hawapaswi kuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Taifa,”alisema na kuongeza kuwa;

“Mgombea wa nafasi hiyo au wakala wake atatakiwa kuwasilisha fomu za kuomba uteuzi Julai 19 mwaka huu na kuambatanisha viambatanisho vyote vilivyotajwa katika fomu na stakabadhi ya malipo ya fomu kwa Katibu Mkuu wa Chama,”amesema Munisi.

Aidha amesema Jula 22, mwaka huu Katibu Mkuu wa Chama hicho atawasilisha taarifa kuhusu mchakato huo kwa kamati kuu ya chama ambapo Kamati hiyo itapendekeza jina au majina ya wagombea kwenda Baraza Kuu na Mkutano Mkuu kwa ajili ya mapendekezo ya uteuzi wa mwisho .

Akizungumzia upande wa nafasi ya ubunge, amesema wagombea wa ubunge watatakiwa kujaza fomu za kuomba uteuzi wa kugombea nafasi hiyo ndani ya Chama.

Alisema fomu zao zitatolewa Julai 4, mwaka huu hadi Julai 10 kwa Tanzania Bara na Visiwani ambapo zitapatikana katika mtandao wa chama na Ofisi za Majimbo ya Chama hicho.

“Kamati Kuu ya Chama itafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge Julai 30 hadi 31 mwaka huu,ambapo wagombea wataitwa na kuhojiwa juu ya uanachama wao na sera zao,”alisema na kuongeza

“Hatua ya pili majina yatakayoteuliwa yatapelekwa katika kura ya maoni kwa Mkutano Mkuu wa Majimbo kisha kurudishwa katika kamati tendaji ya Kanda na kufanya mapendekezo ya nani anafaa,”Amesema

Akizungumzia nafasi za Udiwani Munisi amesema utafiti wa kuwapata wagombea wa udiwani (Tanzania bara)utaendeshwa kwa kuzingatia sheria ya Chama huku kila mgombea akiitwa mbele ya kamati ya Utendaji kueleza taarifa zake.

Amesema fomu zao zitaanza kutolewa Julai 11, mwaka huu katika Ofisi za kata za Chama na kurudisha fomu Julai 17,mwaka huu nao watapigiwa kura ya maoni na Kamati ya Utendaji ya Jimbo ambayo itakaa na kufanya uthibitisho wa wagombea udiwani .


Share:

KAMPUNI YA FINTECH YAZINDUA APP ITAKAYOSAIDIA KUTOA USHAURI KATIKA MASUALA YA KIFEDHA

Kampuni ya Fintech imezindua App mpya ambayo itakayokuwa ikitoa ushauri wa kifedha kwa mtu binafsi kulingana na mapato na matumizi yake, kutumia akili bandia (Artificial Intelligence) ambayo ni teknolojia ya hali ya juu.

App ya Mipango, inayojihusisha na masuala ya kifedha, itasaidia Watanzania kuwa na uelewa mzuri juu ya matumizi yao, mapato yao na kupata nafasi ya kuangalia bajeti binafsi, kujiwekea malengo ya maendeleo na kisha app hii kukusimamia ili kufanikisha malengo hayo. Ikiwalenga watanzania wa rika zote na kisomo chochote, Mipango app inapatikana kwa lugha ya Kiswahili huku elimu ya fedha ilikitolewa kwa lugha rahisi Zaidi. 

Kwa mujibu wa mmoja wa Waanzilishi wa Mipango, Bi. Lilian Makoi: “Kua na elimu ya kifedha ni moja ya nguzo ya kukua na maendeleo nchini. Zaidi ya  asilimia hamsini (50%) ya  watu wazima wa Watanzania hawajui kiasi au jinisi wametumia  fedha zao wiki iliyopita, na hawana malengo ya kifedha. Tabia hiyo inaingiza watu kwenye madeni mabaya, ambayo inaongoza kupelekea kuwa masikini.”

“Tumeamua kuzindua App hii kwa lengo la kutoa fursa ya kubadilisha maisha ya raia wetu wanayoishi kila siku na kuwa na mahusiano mazuri na fedha zao. Program hii itamsadia mteja kupokea ushauri wa kifedha bure, kufuatilia kipato chake, kufuatilia matumizi yake yote yanavyokwenda, kusimamia mikopo na madeni na pia kupata fursa za uwekezaji kuendana na kipato chake,” alisema Lilian. 

Aliongeza: “Pia tunatarajia kupata zaidi ya watu milioni moja ambao watapakua  App hii ndani ya miezi 12 ya mwanzo.  Mwaka 2017 taasisi ya Finacial Sector Deepeing (FSDT), walifanya utafiti wa sekta ya fedha katika miji mbalimbali na kujua kuna watu zaidi ya milioni 27 walikuwa watumiaji hai wa simu Tanzania na 48.7% kati ya hao ni watuamiji wa simu za mkononi zenye kuweshwa huduma za mtandao (Smart Phones). Kati ya watumiaji hawa wa simu, milioni 9 ndio wenye vyanzo vya mapato. Hii ilitupelekea kuamini kwamba kuzindua App hii itakuwa na manufaa zaidi kwa raia wa nchi hii.”

Katika miji mingine kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, asilimia 43 ya Watanzania walitunza fedha zao nyumbani kwa njia ya mtandao au kwa benki au kwa watu wa karibu wa familia.

Mwanzilishi mwingine wa Mipango Fintech, Agness Mollel alisisitiza: “Fikra zetu kwa baadaye ni kuwashawishi vijana wengi Zaidi kua na Mipango binafsi ya kifedha na kuwawezehsa kufikia malengo yao kwa kutumia fursa za kuwekeza zinazowafaa nchini. 

Lengo letu ni kuwa wezesha watu katika maeneo yote na wenye umri tofauti kkua na Mipango ya kifedha na matumizi mazuri kwa mafanikio yao binafsi,”.

“App hii itakuwa ikitambulisha kitu kipya kila mwezi, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wateja wetu kununua hisa na fursa za uwekezaji, kutunza kumbukumbu za ulio wakopesha na kupata ushauri wa kila matumizi unayoyafanya kulingana na uwezo wako halisi wa kifedha.” Ofisa Mkuu wa Teknolojia wa kampuni hiyo, Nicholaus Ngolongolo, alisisitiza. 

“Uzinduzi huu una vipengele vitatu ambavyo ni kutengeneza wasifu wako wa kifedha, kutengeneza bajeti ya mwezi na kurekodi mapato na gharama za kila mwezi/ siku ambazo zitakuwa zikifuatiliwa kulingana na bajeti yako ili kukusaidia kuishi ndani ya bajeti yako!” alimalizia Mwanzilishi wa nne Chris Rabi.

Uvumbuzi mpya wa huduma hii kwenye simu za mkononi unaletwa na Kampuni ya Mipango Fintech ambayo itabadilisha Watanzania jinsi ya kuishi kwa malengo na usimamizi wa fedha zao binafsi na kuwezesha kufikia malengo yao ya maendeleo.  Hii ni hatua ya kwanza ila tunategemea kuendelea kutambulisha vipengele vingine vingi Zaidi na Zaidi.

Kuhusu Mipango Fintech 
Mipango ni huduma binafsi ya fedha ambayo inamwezesha mtumiaji kutunza fedha, matumizi, malengo ya fedha, bajeti na kuwekeza kupitia fursa za kifedha. Mtumiaji wa Mipango app anaweza kupata uelewa zaidi juu ya kuzimiliki fedha zake kwa uhuru zaidi.
Share:

CUF YAMSIMAMISHA UONGOZI MAKAMU MWENYEKITI WA CHAMA HICHO ZANZIBAR

Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF) limemsimamisha Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar, Abbas Juma Muhunzi kwa kukiuka maadili ya uongozi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwaUmma CUF, Mohamed Ngulangwa inaeleza kuwa, kwa kuzingatia Ibara za 83(1) (b) na 94(1) zinazolipa Baraza Kuu la uongozi la Taifa mamlaka na muongozo katika kushughulikia masuala ya kinidhamu kwa viongozi wakuu.

Baada ya wajumbe kupokea tuhuma dhidi ya Muhunzi na kufanya mjadala wa kina, Baraza hilo lilitoa nafasi kwa mlalamikiwa kujitetea ambapo alikiri kufanya makosa yaliyoelekezwa kwake na akakiachia kikao kuamua dhidi yake.

Wajumbe katika kikao hicho waliamua kupiga kura za kumsimamisha uongozi ambapo wajumbe 42 walitaka Muhunzi asimamishwe huku wajumbe 7 wakipinga kumsimamisha na wajumbe 6 hawakuunga mkono wala kupinga kusimamishwa kwa Muhunzi.

Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, maamuzi ya kumsimamisha Muhunzi yanastahili kufikishwa kwenye mkutano mkuu kwa maamuzi ya mwisho ndani ya siku 90 kuanzia leo.


Share:

Rais Magufuli Ampa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi Siku 7

Rais Magufuli  amempa siku saba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amkabidhi  hati ya shamba lenye ukubwa wa hekta 5,000, linalomilikiwa raia wa kigeni wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro. 
 
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 29 Juni 2020, baada ya kupokea malalamiko ya mgogoro wa ardhi, kutoka kwa wananchi wa Kibamba, wilayani Kilosa.

Amemuagiza Waziri Lukuvi aliyekuwepo kwenye msafara wake kumkabidhi hati ya shamba hilo, ili aligawe upya, kisha  sehemu yake wapewe wananchi wa Kibamba, kwa ajili ya kumaliza changamoto ya mgogoro wa ardhi.

Rais Magufuli amesema katika uongozi wake, atahakikisha analinda maslahi ya wananchi wanyonge, pamoja na kuwadhibiti wenye nguvu ambao wamekuwa wanadhurumu haki za wanyonge.

“Mnakodishiwa mashamba sababu hati ni za wakubwa, nataka nilale nao hao wakubwa, nimesema siku saba waziri pamoja na mkuu wa mkoa ataleta hati, yale mashamba yakufuta, sababu kwa mujibu wa sheria ardhi iko chini ya rais, na mimi nitaenda na watu wanyonge,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka wananchi wa Kibamba, kutumia vyema mashamba watakayopewa.

“Naweza futa nusu au kutokana na mapendekezo nitakayopewa nitayagawa kwenu. Mjipange vizuri kugawiwa kwenu isije kuwa chanzo cha kupigana, mtumie uongozi mlio nao kila mmoja apate kipande, kutakuwa sehemu ya wafugaji na wakulima sababu wote tunategemeana,” amesema Rais Magufuli.


Share:

MGODI WA BARRICK BULYANHULU WATOA ZAWADI YA NG’OMBE, FEDHA KWA WANAFUNZI WALIMU NA WAZAZI NA SHULE ZILIZOFAULISHA KIDATO CHA NNE NYANG’HWALE

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Twiga Minerals Corporation hapa nchini, umekabidhi zawadi zenye thamani ya shilingi milioni Tisa na elfu Hamsini kwa Wanafunzi, Wazazi, Walimu na Shule zilizofaulisha wanafunzi kwenye mtihani wa Kidato cha Nne Wiyalani Nyang’hwale.

Zawadi hizo zimekabidhiwa Jumamosi 27 Juni 2020 na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Fabian Yinza wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ya kuhitimisha mwaka wa kwanza wa mradi wa kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne wilayani humo unaojulikana kama PIP (Performance Improvement Program).

Akikabidhi zawadi hizo Kaimu Mkuu wa Wilaya alibainisha kwamba mradi huo ulibuniwa mwaka jana 2019 na ulitekelezwa kwa awamu tatu kwenye shule zote 10 za Sekondari wilayani humo kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu na wadau mbalimbali.

“Wanafunzi 200 walishiriki kwenye mradi huu na kufanya mtihani wa taifa mwaka jana 2019, na kwa mara kwanza wilaya imefanikiwa kupata wanafunzi 20 wenye daraja la kwanza akiwemo msichana mmoja mwenye daraja la kwanza kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa wilaya hii kwa hivyo tunawashukuru sana Barrick Bulyanhulu tumepata matokeo chanya” ,alisema Mhe. Fabian Yinza.

“Hongereni sana wanafunzi mliofaulu, wazazi, walimu pamoja na wadhamini Barrick Bulyanhulu kwa juhudi na ushirikiano mliounyesha hadi kufikiwa kwa mafanikio hayo, nawasihi sana zawadi mtakazopewa leo na Kampuni ya Barrick Bulyanhulu uwe ni motisha wa kusonga mbele, na kuhamasisha wengine kufanya vizuri zaidi kwenye suala la elimu ili tupate wataalam watakaofanya kazi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa na serikali na wadau hapa nchini na Wilayani Nyang’hwale kama vile hospitali, vituo vya afya, zahanati, shule na viwanda”,alisema.

Kaimu Meneja wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Bi. Zuwena Senkondo alitaja makundi saba ya zawadi za kutambua waliofaulu na waliofanikisha ufaulu huo ikiwa sehemu ya motisha kwenye mradi huo wa PIP kwa mara kwanza.

“Kundi la kwanza la zawadi ni la wanafunzi wavulana wanne waliofaulu daraja la kwanza kwa pointi 12 hadi 13 ambapo wawili wenye point 12 tunawazawadia shilingi laki tano kila mmoja, na watatu wenye point 13 wanawazawadia laki tatu kila mmoja, Kundi la pili ni la wanafunzi saba wasichana waliofaulu daraja la kwanza na la pili, ambapo mwenye daraja la kwanza amezawadiwa fedha taslimu shilingi laki tano, na wengine wenye daraja la pili shilingi laki mbili kila mmoja.

Kundi la tatu ni la wazazi watano ambao watoto wao walifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza, ambapo kila mzazi amezawadiwa Ng’ombe jike mmoja mwenye thamani ya shilingi laki tano, Kundi la nne ni walimu waliofaulisha vizuri zaidi kwenye masomo yao kwa alama A, na B wanazawadiwa kiasi cha shilingi laki moja hadi laki moja na ishirini na tano elfu kila mmoja kulingana na walivyofaulisha. Kundi la tano ni walimu 14 ambao wamefaulisha alama A kwenye masomo yao ambapo masomo ya sanaa walimu wanazawadiwa shilingi elfu hamsini kwa kila alama A na masomo ya sayansi shilingi elfu sabini na tano kwa kila alama A.


Kundi la sita ni zawadi ya shule moja iliyofaulisha kwa kuzingatia uwiano wa jinsia ambayo ni Shule ya Sekondari ya Shabaka iliyozawadiwa kiasi cha shilingi laki tano. Na kundi la saba ni la shule zilizofaulisha wanafunzi wengi kwa daraja la kwanza hadi la tatu ambazo ni Sekondari ya Nyang’hwale iliyofaulisha jumla ya wanafunzi hamsini, Sekondari ya Bukwimba iliyofaulisha wanafunzi 46 na Sekondari ya Kafita iliyofaulisha wanafunzi 38.

Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale David Rwazo, alisema muasisi wa Mradi wa PIP ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Hamim Gwiyama ambaye kwa sasa ni Marehemu.

 “Tutamuenzi kiongozi huyu aliyekuwa mzalendo na mpenda elimu, tutahakikisha kwamba tunatimiza malengo ya program hii ambayo ni kuongoza matokeo ya kidato cha nne kimkoa na kushika nafasi bora za kitaifa, kwa mwaka huu wa kwanza tulilenga kupata wanafunzi 100 wenye daraja la kwanza hata hivyo tumefanikiwa kupata wanafunzi ishirini na hii ni ishara kwamba inawezekana, hasa baada ya kuona kwamba pia tumefaulisha msichana wa kwanza kwenye wilaya hii kwa daraja la kwanza jambo ambalo limefungua ukurasa mpya katika halmashauri yetu ya Nyang’hwale”,alisema.

Akitoa taarifa ya Idara ya Elimu Sekondari ya mradi wa PIP katika Halmashauri ya Nyang’hwale Afisa Elimu Vielelezo na Takwimu Mwl Felician James, alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kupitia mpango wake wa uwekezaji kwenye jamii (CSR), ulinunua vitabu 900 vya mazoezi ya masomo yote vilivyogawiwa katika shule zote 10, ili kuhakikisha wanafunzi wote wa kidato cha nne wanakuwa na vitabu vya masomo yote ili kujiandaa vyema na mitihani yao.

“Awamu ya pili ya mradi ilihusisha kambi ya mwezi mmoja ya wanafunzi 200 wa kidato cha nne ndani ya wilaya hiyo iliyofanyika na kuwawezesha wanafunzi kushiriki masomo ya ziada yaliyofundishwa na walimu wabobezi wa masomo mbalimbali wilayani humo, na awamu ya tatu ilihusisha walimu kupambanua changamoto za kwenye masomo mbalimbali za wanafunzi na kuwapatia masomo ya ziada na mtihani wa kujipima”, Alisema Afisa Elimu Vielelezo na Takwimu Mwl Felician.

Wakizungumza baada ya kupatiwa zawadi wanafunzi, wazazi, walimu na wakuu wa shule waliushukuru uongozi wa wilaya na halmashauri kwa kushirikiana na Barrick kutambua mafanikio yaliyopatikana.

“Walimu wamejitolea sana kunisaidia ili niweze kufaulu mtihani kwa kutufundisha bila kukata tamaa hadi muda wao wa ziada nawashukuru wazazi pia kwa kunipa nafasi ya kusoma pia wafadhili wa Barrick waliotupa chakula tukawa tunasoma tukiwa tumeshiba vizuri, nitajitahidi nisome kwa bidii nitakapoingia kidato cha tano ili niendelee kupata elimu zaidi.” Alisema Zainab Majaliwa ambaye ni mwanafunzi wa kwanza wa kike kupata daraja la kwanza wilayani humo akitokea katika Shule ya Sekondari ya Msalala.

“Ninaomba uongozi wa Mgodi uje unitembelee Ngo’ombe niliyezawadiwa leo naenda kumtumza azae na kunisaida kumsomesha mwanangu hadi afikie malengo”, alisema Charles Katemi mzazi wa Simon Charles aliyepata daraja la kwanza.

“Kila Sekondari ilipangiwa kufaulisha wanafunzi 10 wa daraja la kwanza sisi Kafita tumefanikiwa kupata wanafunzi watano wenye daraja la kwanza, lakini pia Mwalimu wetu mmoja amengoza kwa kupata zawadi kwa kufaulisha wanafunzi 3 wenye alama A katika somo la Bailojia, hivyo tunaamini tutafanya vizuri zaidi mwaka huu” alisema Mwalimu Mkuu wa Kafita Mwl. Felista Kamati.



“Shule yetu ya Sekondari ya Nyang’hwale imeongoza kiwilaya kwa kuwa nawanafunzi 50 waliofaulu kati ya daraja la kwanza hadi la tatu, na mimi nimepata zawadi kwa kufaulisha alama nzuri kwenye somo la History, tunashukuru sana mwanzilishi wa wazo hili, wadhamini wa mradi huu na viongozi wetu kwenye halmashauri yetu.” Alisema Mwl Steven Gumba Ombogo.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Mhe. Fabian Yinza akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Msalala wilayani Nyang’hwale mkoani Geita ya kuhitimisha mwaka wa kwanza wa mradi wa kuboresha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne wilayani humo unaojulikana kama PIP (Performance Improvement Program).
Kaimu Meneja wa Maendeleo ya Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Bi. Zuwena Senkondo akitaja makundi saba ya zawadi za kutambua waliofaulu na waliofanikisha ufaulu huo ikiwa sehemu ya motisha kwenye mradi huo wa PIP kwa mara kwanza.



Share:

Wataalam 16,000 Sekta Ya Kilimo Wafundishwa

Wizara ya Kilimo imesema mafanikio makubwa yamepatikana nchini katika kuzalisha wataalam wa Kilimo kupitia vyuo vyake na kufanya sekta ya Kilimo kuchangia asilimia 28.2 ya pato la Taifa.

Kauli imetolewa leo (29.06.2020) mjini Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofungua kikao kazi cha siku mbili cha Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATIs) chini ya wizara hiyo.

Kusaya alisema anatambua kuwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya kati ni kiwanda cha kuzalisha wataalam wenye sifa zinazohitajika katika soko la ajira au ajira binafsi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

“Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vimetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na wataalam wa kutosha wenye weledi wa kusimamia sekta ya Kilimo ambapo jumla ya wataalam 16,570 walihitimu mafunzo yao kwenye vyuo vya mafunzo ya Kilimo nchini kati ya mwaka 2009 hadi 2018” alisema Kusaya

Katibu Mkuu Kusaya aliongeza kusema sekta ya kilimo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambapo sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2.

Ili kuendelea kuwa na vyuo bora na vyenye tija Katibu Mkuu Kusaya ameagiza wakuu wa vyuo vyote Kumi na Nne (14) chini ya Wizara ya Kilimo kuweka msisitizo katika kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kufundisha wanafunzi kwa vitendo zaidi ili kujenga umahili.

“ Sisi ndio vyuo vya kilimo lazima tuoneshe  kuwa tunafanya kilimo cha kisasa. Itakuwa jambo la ajabu kukuta chuo hakina shamba darasa bora la kufundishia wanafunzi” alisisitiza Kusaya.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amevipongeza vyuo vya kilimo nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya kufundisha wanafunzi na wakulima mbinu bora na za kisasa za kukuza sekta ya kilimo.

“Nawapongeza sana na ningependa kuona mnaongeza kasi katika juhudi hizo na pia kuwajengea uwezo wanafunzi  katika maarifa na ujuzi wa  kilimo biashara kwa vitendo ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na kuiwezesha Tanzania kupata malighafi kwa urahisi zaidi kwa ajili ya viwanda vinavyozunguka maeneo yenu” alipongeza Katibu Mkuu huyo.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimelenga kuweka mipango imara ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi viwango vinavyohitajika kwenye soko la ajira na kujiajiri. Hivyo wakuu wa vyuo hivyo watajadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mwisho
Imetolewa na :
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo


Share:

LIVE: Ziara Ya Rais Magufuli Mkoani Morogoro

LIVE: Ziara Ya Mhe.rais  Magufuli Mkoani Morogoro


Share:

Nimeisambaratisha CHADEMA Ukonga, sasa nahamia Tarime Vijijini- Mwita Waitara

Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kuwa mpaka sasa hivi amekwishamaliza kazi kubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam ya kukisambaratisha Chama cha CHADEMA, na kwa sasa  ameweka wazi kwa mara nyingine kuwa atakwenda kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara kupitia chama hicho.

Waitara amesisitiza kuwa haondoki Ukonga kwa sababu anamkimbia mtu, bali amekamilisha kazi ya kukisambaratisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hivyo anakwenda Tarime Vijijini ambako ndipo anapotokea, kufanya kazi hiyo.

“Wala hakuna mtu ninayemkimbia, jimbo langu [Ukonga] lipo salama ndani na nje ya chama. Nimeshafanya kazi ya kuwasambaratisha CHADEMA hapa wameshapoteana. Walikuwa na Meya wa Jiji, hayupo, walikuwa na Meya Ilala, hayupo, walikuwa na Meya wa Ubungo, hayupo. Nishamaliza kazi Dar es Salaam, naenda kukamilisha kazi sehemu nyingine,” amesema Waitara.

Kiongozi huyo ambaye alihamia CCM akitokea CHADEMA Julai 2018 amesema kuwa Julai 14 mwaka huu atachukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge Jimbo la Tarime Vijijini, na kwamba suala hilo sio siri.


Share:

LIVE: Rais Magufuli Akiweka Jiwe La Msingi Wa Ujenzi Wa Mahandaki Ya Reli Ya SGR

Live: Rais  Magufuli Akiweka Jiwe La Msingi Wa Ujenzi Wa Mahandaki Ya Reli Ya SGR


Share:

China nayo yageukia mitishamba kutibu corona

Wakati wanasayansi wakipambana kutengeneza chanjo ya virusi vya corona, China nayo imetengeneza dawa ya asili inayojulikana kama 'Traditional Chinese medicine (TCM)' ili kutibu ugonjwa wa corona.

Gazeti moja lililozinduliwa na serikali ya China lilidai kuwa 92% ya wagonjwa wa corona wa nchi hiyo walitibiwa na dawa hiyo. TCM ni dawa ya kale zaidi duniani ambayo imetengenezwa kwa mitishamba.

Dawa hiyo ni maarufu sana nchini China licha ya kwamba ilizua mjadala kuhusu matumizi yake mtandaoni.

Wataalamu wanasema China inajaribu kuisambaza dawa hiyo ya TCM ndani ya nchi na nje ya nchi lakini wataalamu wa afya bado hawaamini uwezo wake wa kutibu.

Wizara ya afya ya China imeweka kitengo maalum cha TCM pamoja na muongozo wa kukabiliana na virusi vya corona, wakati televisheni ya taifa ilidai kuwadawa hiyo ilifanya kazi katika mlipuko wa miaka ya nyuma kama Sars mwaka 2003.


Share:

New Mv Victoria Hapa Kazi Tu Yatia Nanga Rasmi Katika Bandari Ya Bukoba.

Na Avitus Benedicto Kyaruzi, Bukoba Kagera.
Hatimaye meli ya New Mv Victoria Hapa Kazi Tu iliyokuwa imesitisha huduma za usafiri katika ziwa victoria kati ya Mwanza na Kagera  imetia nanga katika bandari ya Bukoba ikitumia muda wa takribani saa sita tofauti na saa 12 za awali..

 
 Meli hiyo iliyokuwa ikijulikana kama MV Victoria imepokelewa jana  katika bandari ya Bukoba majira ya saa 10 jioni june 28 mwaka huu na imeelezwa kuwa ilianza safari zake katika bandari ya Mwanza majira ya saa 3 asubuhi na kwamba  ilisitisha huduma  kati ya mwanza na Bukoba  takribani miaka sita iliyopita.
 
Mgeni rasmi alikuwa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama cha Mapinduzi (CCM)  Humphrey Polepole, ambaye alisafiri na meli hiyo kutoka Mwanza hadi Bukoba na emeeleza  ujio wa meli hiyo ilivyo kielelezo tosha cha utekelezaji wa ahadi ya CCM na maono ya Rais John Pombe Magufuli kwa maendeleo ya watanzania,.
 
Pole pole amesema ameagizwa na Rais Magufuli kuwatangazia wakazi wa kanda ya ziwa kuwa gharama za kusafilisha mizigo zitakuwa ndogo kulinganisha na hapo awali ambapo tani moja itasafirishwa kwa sh elfu 27 tofauti na ilivyokuwa awali ya sh 120,000 kwa mzigo wa tani moja
 
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kagera Bregidia General Marco Gaguti amesema  kuwa ujio wa meli hiyo utafunguia fursa za kibiashara baina ya Kagera na mikoa jirani pamoja na nchi zinazozunguka mkoa wa kagera
 
Ukarabati wa meli hiyo umegharimu zaidi ya sh bilioni 22 na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria na mizigo yenye tani 100 na gharama za usafiri kati ya mwanza na Bukoba pamoja na tarehe ya kuanza rasmi safari itatangazwa baada ya siku 14 kuanzia sasa.


Share:

Rais Magufuli akagua ujenzi wa reli ya kati (standard gauge railway) sehemu ya Dar es Salaam - Morogoro

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana  tarehe 28 Juni, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kwa sehemu ya kwanza ya Dar es Salaam – Morogoro na kuelezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa.

Rais Magufuli alisafiri kwa gari kandokando ya reli hiyo kuanzia Kisarawe hado Soga Mkoani Pwani na kisha akapanda kiberenge kilichopita katika reli hiyo mpya kuanzia Soga hadi Kikongo kabla ya kuendelea na safari yake kwa gari kuelekea Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa alimueleza Rais Magufuli kuwa kazi ya ujenzi wa sehemu ya kwanza ya reli hiyo imefikia asilimia 82 ambapo Watanzania 13,000 wamenufaika na ajira na inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu (2020).

Akizungumza na wananchi wa Soga na Kikongo, Rais Magufuli amewapongeza kwa kupata mradi huo na ametaka waendelee kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili waweze kunufaika zaidi na mradi huo.

Aidha, Rais Magufuli alisikiliza kero za wananchi hao ambapo aliendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya uboreshaji wa Shule ya Msingi Soga na kufanikiwa kukusanya shilingi 68,535,000/- zikiwemo shilingi Milioni 5 alizochangia yeye mwenyewe, na amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kufika Kijijini hapo ili kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mmiliki wa shamba kubwa lililopo kijijini hapo ambalo halilimwi.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha anatatua tatizo la maji linalokikabili kijiji cha Soga.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kutekeleza mradi huo ambao utagharimu shilingi Trilioni 7.02 kwa sehemu ya kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Mkoani Dodoma, pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika Bwawa la Nyerere ili kukuza uchumi wa Watanzania na kuinua kipato cha wananchi na hivyo amewataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo.

Akiwa Mlandizi, Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi na kumuagiza Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso kuhakikisha Wizara ya Maji inatatua tatizo la maji la Mitaa ya Mbwawa Shule na Mbwawa Mkoleni na pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami ya Mafia – Mzenga – Vikumbulu ili kuunganisha Mlandizi na reli.

Rais Magufuli amewasili Mjini Morogoro na leo  ataendelea na ziara yake Mkoani hapa ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa (standard gauge) sehemu ya Morogoro – Makutupora, kuzindua barabara ya lami ya Rudewa – Kilosa na atafanya mkutano wa hadhara katika eneo Mkadage Wilayani Kilosa.

Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu (2020) huku wakikumbuka kudumisha amani, umoja na mshikamano pamoja na kuwachagua viongozi watakaowafaa.


Share:

Ufugaji wa nguruwe : Gharama na Faida Zake

 Utangulizi
Nguruwe ni mnyama amabaye hutumika kama chakula / mboga na pia ni zao la biashara kwa mfugaji, mjasirimali na mfanyabiashara.
 
NGURUWE HUTEGEMEA SANA MAMBO YAFATAYO
1 . Banda imara na rafiki kwake
2. Usafi ni muhimu sana katika banda la Nguruwe
3 Mchaganyo bora wa chakula
4. Tiba bora na kinga
5. Maji na Lishe ( access ya vyakula Muhimu kwake )
 
CHANGAMOTO
KATIKA UFUGAJI WA NGURUWE KUNACHAGAMOTO ZAKE LAKINI ZAWEZA KUTATULIWA KWA KUFATA MAMBO KADHAA.
Katika ufugaji wa nguruwe kunachagamoto ya vifo vya nguruwe wachanga ambao hupunguza faida ya biashara ya nguruwe kwa kupunguza idadi ya nguruwe wazima wa kuuzwa lakini utunzaji mzuri wa nguruwe wachanga huepusha vifo vinavyotokana na shida kama:
 
Matatizo ya kupumua
Ni kifo kinachosababishwa na mama anapomlalia nguruwe mchanga.chagamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kuwatenga au kuwa na mabanda makubwa ya kulelea watoto.
 
Baridi
Nguruwe wachanga huathiriwa na baridi haswa katika majuma mawili au matatu ya mwanzo. Hii ni kwa kuwa wana kiwango kidogo cha utando wa mafuta wa kuwakinga.
 
Unashuriwa kuwaweka katika hali ya joto, wape matandiko na utumie vipasha joto kama vile kuwasha globu za joto kama utakuwa umewaweka kwenye mabanda ya kuta au nyumba yenye sakafu baridi.
 
Namna bora utunzaji wa nguruwe wachanga
Nguruwe moja wa kike ana uwezo wa kuzaa watoto 12. Namna ifuatayo itasaidia kupunguza idadi ya vifo vya nguruwe wachanga:
1.Pale nguruwe awapo na kidonda nyunyizia dawa ya ayodini 5% kwenye kovu ili kuzuia kuambukizwa kwa magonjwa.
2.Wawekee matandiko (nyasi kavu au maganda ya miti) mahali pa mapumziko ili wapate joto au utumie globu za joto.
3Wadunge sindano ya madini ya chuma (iron) siku ya tatu baada ya kuzaliwa ili kuzuia upungufu wa damu.
3. Yalainishe meno ya vichaga kabla ya masaa 24 ili kuzuia uharibifu wa matiti wakati wanaponyonya.
4. Watie vibandiko au utoboe masikio ili uwatambue na uhifadhi rekodi zao kama kuna umuhimu kama vile wafanyavyo wafugaji wa ng’ombe.
5. Wapime uzani wanapozaliwa na uhifadhi rekodi hiyo itakusaidia kujua ukuaji wao na maendeleo yao
6. Wahasi wale wa kiume juma la tatu, wale ambao hawafai katika kuendeleza kizazi kwa kutumia mtindo wazi (open method) kama unaona inafaa.
7. Wapatie dawa ya kuzuia minyoo pia zipo dawa za asili kama unga wa mkaa na majivu pia zipo za kitaalamu, wasiliana na wataalamu wa mifugo
8.Waachishe kunyonya katika juma la nane au wafikapo kilo 14 hadi 20 hii itasaidia kujitegemea na kukua kwa haraka.
 
Nguruwe Walioachishwa Kunyonya
1.Walioachishwa kunyonya wawekwe makundi ya 10 hadi 12 kulingana na uzito au ukubwa wao kwenye eneo ambalo watajitosheleza.
2.Watenganishe wakubwa kwa wadogo ili kuzuia kupigana.
3.Wakati wa kuwaachisha kunyonya mwondoe mama yao kutoka kwa watoto ili kupunguza usumbufu.
4Watoto wa nguruwe wa mama tofauti wasiwekwe pamoja maana hii husababisha mapigano kati yao na
5.Unapowachanganya watoto wa mama tofauti wapake mafuta ya gari yaliyotumika kwenye ngozi yao au mafuta ya kula ili kuiondoa harufu ya kutambulika ili wasipigane
 
FAIDA YA UFUGAJI WA NGURUWE
Faida kuu ya nguruwe ni zao la chakula lakini pia ni zao la kukuongezea kipato ukiwa kama mjasirimali / mfanyabiashara.
Lengo langu nikueleza namna unavyoweza kufuga na kutupa faida, Steps zifatazo ni muhimu kuzigatia.
 
JIPE MTAJI WA MILLION 4 / 3.5 KWA NGURUWE 50
UANDAAJI WA BADA WEKA MAKADILIO YA LAKI TANO (800,000/=) .
Hapo nazugumzia banda lenye heru U yenye mstatili ikiwa na kitako kirefu
Eneo lenye ukubwa wa mita 50 kwa 50 litafaa zaidi ili kuhakikisha usalama wa nguruwe wako na ukuaji bora.
1. Tafuta mabati used kwa bei ya 5000 mfano mabati 20 ya futi 10 /10 = 100,000/=
2. Tafuta mabazi ya futi 10 kwa 2000 kila moja utapata mabazi pic 100 = 200,000/=
3. Tafuta miti ya nguzo na kechi ya 1000 na 2000 miti ya 1000*70 na 2000*3 = 120,000/=
4. Tafuta chagalawe / moramu trip 10*3000 =30000/=
5. Cement mifuko kwa ajiri ya sakafu na mashimo ya kulishia 5 *18000 = 90,000/=
6. Misumari ya aina 4, nch 6 kg5,nch 3 kg5 nch 5 kg10 na nch4 kg10, Bawaba na komeo =100,000/=
7. Malipo ya fundi 75000 fundi uashi na 75000 fundi seremala =150,000
JUMLA HAPO INAKUWA 790,000/= MAKADILIO INAKUWA 800,000/=
 
UNUNUZI WA NGURUWE WA KUANZIA .
Nguruwe wadogo wadogo ni vinzuri zaidi kuanza nao kwa sababu watakuzalia watoto wengi na kwa muda mrefu . Chukua mfano MILLION 2.5 . Nguruwe wadogo wa dogo wanauzwa 50000 au 40000 inategemeana na mahala na maelewano . Milioni 2.5 inakupa vitoto 50 au 55 . Hivyo unawexa kuwa na vitoto jike 50 na vidume 5. baadaye ukaongeza madume matano ya kuazima au kukondi kwa ajiri ya kupandishia
 
MAANDALIZI YA CHAKULA
Mchaganyiko wa chakula cha nguruwe na gharama zake tunaweza ukadilia kujitosheleza kwa laki tatu kwa mwenzi mmoja kwa nguruwe hao 50, kwa 300,000/= , ambapo itajumuisha tiba / kinga, lishe, vyakula vya nguruwe vinaweza kuwa pumba ya mpunga ile laini,pumba ya mahindi, mashundu, mabaki ya magada ya vianzi amba mabaki ya chakula yaliyosalama
 
MALIPO YA MSIMAMIZI NA ENEO LA KUWEKEZA
Katika kipengele hiki makadilio ya juu ama ya chini kwa msimamizi wa kazi yako waweza mlipa 100,000/= ama chini yake pia kwa mwenye eneo huwa nimaelewano tu aunaweza pata kwa fair au kukakodi kwa laki tatu, 300,000/= kwa mika miwili.
 
HIVYO JUMLA YOTE YA GHARAMA ZA UAZISHAJI UWEKEZAJI WA NGURUWE 50 ZITAKUGHARIMU MILLION 4 AMA MILLION 3.5 KWA MAANA KUWA HAPO JUU NIMETUMIA MAKADILIO YA JUU NA UKIINGIA KWENYE UHALISIA KAMA MJASIRIMALI LAZIMA IPUNGUE NA KUFIKIA 3.5

KIPATO AU FAIDA YA UFUGAJI NGURUWE
Nguruwe wanafaida ya haraka na nimradi wa uhakika kabisa, ukipitiia mchanganuo hapo juu wa nguruwe 50 utatupa faida kama ifatavyo
 
Nguruwe huzaa Mara mbili kwa mwaka na huzaa watoto zaidi ya watanoyaani huzaa watoto 12 ama nane .
Basi chukua nguruwe 50 * vitoto 5 yaani ufanye kuwa nguruwe wako 50 wakupatie vitoto vitano vya uhakika
Nguruwe 50*5 = 250 ukijumlisha na wale 50 wa mtaji umakuwa nao 300 . Chukua zao la nguruwe la 250 na uza kwa 200000 kwa kila nguruwe yaan bei ya kawaida kabisa. Utapata Million 50.

Hivyo zao la kwanza ndani ya robo tatu ya mwaka inakutegenezea million 50 pia na mienzi sita ijayo inakupa tena 50 na zaidi ili kukamilisha uzao wa pili hii inkupa uhakika wa kutegeneza million 100 za uakakika ndani ya mwaka mmoja na nusu ama miaka miwili ukijipa timeframe work lakini kumbuka hapo tumefanya kwa hesabu ya uzao wa chini kabisa ambapo tumeangalia na hasara ya vifo kama vifo visipotokea na uzao ukawa mkubwa utakuwa na uhakika wa kutegeneza million 150 kwa miaka miwili.

Kwenye hesabu ya kuwale unaweza kuwaza sana kuwa itaongezeka na kukughalimu sana jibu ni hapana mpka kufikia kuuza hawatokugharimu zaidi ya million 7 je million 7 kwenye million 150 ni kitu kisicho nafaida ?
 
NB . jambo lolote linahitaji umakini naa dhamira ya dhati pia kushirikisha wataalamu na wenye uzoefu ili kufikia leng Ewe ndugu kila kitu kinawezekana UTAYARI WAKO / UTHUBUTU WAKO, UAMINIFU .NA MAAMZI YAKO.
 


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger