Friday, 27 March 2020

KENYA YAANZA KUTEKELEZA AMRI YA WATU KUONDOKA MTAANI KUANZIA SAA MOJA USIKU KUKABILIANA NA CORONA

Amri ya kutotoka nje Nchini Kenya kuanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri imeanza kutekelezwa mwendo wa saa moja huku huku wafanyakazi wa huduma muhimu pekee wakiruhusiwa kuwa nje usiku hali itakayosaidia kupunguza utangamano baina ya watu na mikusanyiko mikubwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Serikali ya Kenya imewaonya Wakenya dhidi ya kukiuka amri ya Rais ya kutotoka nje kuanzia mwendo wa saa moja jioni ambapo  maafisa wa polisi watakuwa wakifanya misako mitaani na kuwakamata wananchi watakaokuwa wakirandaranda kuanzia mwendo wa saa moja jioni. 

Mwendo wa saa kumi na mbili Wakenya wengi wameonekana wakiharakisha kuelekea nyumbani hatua iliyosababisha msongamano katika barabara kadhaa huku wale waliokuwa wakitumia magari ya umma wakionekana kusubiri katika vituo vya magari hayo licha ya muda kuyoyoma.

Hata hivyo wengine wao walikata kauli na kuanza kutembea kwa miguu wakihofia kukamatwa na maafisa wa polisi.

Mjini Mombasa na Eldoret mpango huo ulianza kwa mkosi baada ya maafisa wa polisi kukabiliaNa na wakazi saa mbili kabla ya amri hiyo kuanza kutekelezwa.

Katika mtafaruku huo waandishi wa habari pia hawakusazwa huku baadhi yao wakichapwa na polisi kwa kujaribu kurekodi katika kamera zao yaliyokuwa yakijiri.
Share:

Mke na Mume Watiwa Mbaroni Kwa Kutoa Taarifa za Uongo Kuhusu Corona

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linawashikilia watu wawili ambao ni mume na mke kwa tuhuma na kueneza taarifa za uongo kwa wananchi kuhusu ugonjwa COVID-19(Corona) na kwamba watafikishwa mahakamani wakati wowote.

Akizungumza leo  Machi 27 mwaka 2020 ,Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema watu hao wamekamatwa Machi 20 mwaka huu saa saba mchana  wakiwa kwenye daladala aina ya Toyota DCM namba T 119 DKS iliyokuwa ikitokea Muhimbili.


“Tunawashikilia watuhumiwa wawili Boniphace Mwita na Mkewe Rosemary wakazi wa Tabata,DSM kwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu corona wakiwa kwenye daladala ambapo walianza kupotosha, kukejeli na kutania kwa kusema Serikali inapotosha Wananchi kwamba kuna corona”-Amesema Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa kutokana na kejeli na uzushi wa watu hao abiria waliokuwepo ndani ya daladala hiyo walikasirishwa na kuchukua hatua za kuwaweka chini ya ulinzi na  kuitaka daladala hiyo ipelekwe Kituo cha Polisi na sasa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya hatua inayofuata ya kuwapeleka mahakamani.

“Baada ya Mwita na Mkewe kusema Serikali inapotosha kuhusu corona na haina fedha ndio maana imefunga shule na vyuo kwa kisingizio cha corona, abiria ktk daladala iliwakera wakawaweka chini ya ulinzi wakamuamuru Dereva apeleke gari Polisi, tunao, tutawapeleka Mahakamani”-Mambosasa


Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi limeshachukua maelezo ya watuhumiwa hao na jarada tayari wameshapeleka kwa Wakili wa Serikali kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.


Share:

China Yasitisha Kwa Muda Wageni Kuingia Nchini Huko ili kukabiliana na Corona

China imetangaza kuzuia wageni wote kuingia nchini humo hata kama wana viza au vibali, lengo likiwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

China pia imeagiza ndege za nchi hiyo na zile za kigeni kufanya safari moja tu kwa wiki na hazitakiwi kujaza watu kwa zaidi ya asilimia 75.

Taarifa kutoka China zimeeleza kuwa kulikuwa na wagonjwa 55 nchini humo siku ya Alhamisi, kati yao 54 walikuwa ni wa kutoka nje ya nchi hiyo.




Share:

RC Tabora Awataka Wananchi Kutoa Taarifa Za Wageni Wasiowafahamu

NA TIGANYA VINCENT,TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa huo kutoa taarifa za wageni wasiofahamika walikopotoka pindi wanaonekana katika maeneo yao ili kuepuka kuambukizwa  homa kali ya mapafu inayoenezwa  na kirusi kipya aina ya  Corona.

Alisema Mkoa huo ni mkubwa na unapatakana na mikoa inayopakana na Nchi za jirani na upo uwezekano wa wageni kuingia kwa kutumia njia za panya na hivyo kuhatarisha afya za wakazi wa Tabora.

Mwanri alitoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa timu ya Mkoa wa Tabora ya kudhibiti janga la Corona lisiingie mkoani humo.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kuchuka taadhari dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoenezwa  na kirusi kipya aina ya Korona kwa kunawa mikono mara kwa mara.

Aidha Mwanri aliwataka wananchi kususia maduka yote ambayo wamiliki wake watakutwa hawaweka vitakasa mikono ama ndoo kwa ajili ya wateja kunawa kabla ya kununua bidhaa.

Mwanri alisema wamiliki wa aina hiyo wana nia mbaya na Watanzania na wanapingana na maagizo ya viongozi wa Kitaifa na wataalamu ya kuwataka wananchi kuna mikono kama kinga ya janga la Corona.

Amevitaka vyombo vya habari na Redio zilizomo mkoani humo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na janga la corona ili Mkoa huo uendelee kuwa salama.

MWISHO


Share:

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akutwa na virusi vya corona

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amekutwa na maambukizi ya Corona baada ya kufanyiwa vipimo, imesema ofisi yake Downing Street.
 
Johnson alichukuliwa vipimo vya ugonjwa huo ambao umeua zaidi ya watu elfu kumi duniani, baada ya kupata dalili kadhaa za ugonjwa wa corona.

“Nimekuwa na dalili ndogo za coronavirus, ambazo ni viwango vya juu vya joto la mwili na kikohozi ambacho hakikomi ,” Bwana Johnson amesema katika video aliyoituma kweinye ukurasa wake Twitter.

Johnson atajitenga binafsi – katika makao yake ya kikazi ya Downing Street, baada ya kupimwa na kupataikana na virusi hivyo na muhusumu wa huduma za afya nchini Uingereza katika ofisi yake al maarufu No 10.

Waziri Mkuu huyo wa Uingereza amesema kuwa ataendelea kulingoza taifa kutoka nyumbani baada ya kupatikana na Covid-19.


Share:

DOWNLOAD - PAKUA APP YA MALUNDE 1 BLOG ...TUWE TUNAKUTUMIA HABARI ZOTE BURE MOJA KWA MOJA KWENYE SIMU YAKO

Kuwa wa Kwanza kupata habari na matukio yanayojiri Tanzania na dunia kwa ujumla kwa kupakua/ kudownload App ya Malunde 1 blog tukuhabarishe masaa 24.


Tembea na dunia kiganjani mwako sasa.

Pakua App mpya ya Malunde 1 blog imeboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasomaji wetu. Hii ndiyo mpya kabisa,ina alama hii ↡↡
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Ni rahisi sana : Ingia Play store kisha Andika Malunde 1 blog halafu bonyeza Install

https://bit.ly/2Qb7qyF

Tafadhali fuata maelekezo hapo juu... Usikubali kukosa habari kizembe..Pakua app yetu Mpya ya Malunde1 blog Sasa
Share:

Breaking : AJENTI WA BASI LA KISIBO AFARIKI DUNIA KWA KUKANYAGWA TAIRI AKIDANDIA BASI SHINYANGA

Wakala/Ajenti wa Basi la Kisibo Athuman Hamad (38) lenye namba za usajili T192 DBZ linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam amefariki dunia kwa kugongwa na basi hilo wakati basi likitoka katika Stand kuu ya mabasi mkoa wa Shinyanga.

Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Machi 26,2020 majira ya saa mbili na dakika 20 asubuhi wakati Wakala huyo akidandia basi hilo na kisha kuanguka na kukanyagwa na basi akafariki dunia hapo hapo.

Mashuhuda waliozungumza na Malunde 1 blog wanasema Athuman Hamad ni Wakala wa Basi la Kisibo alikuwa anatokea Mwanza na basi hilo alipofika Shinyanga alishuka basi lilipoanza kuondoka akawa anakimbilia hilo basi ambalo lilikuwa linatoka getini akadondoka chini akakanyagwa na tairi za basi hilo.

"Huyo Wakala huwa huwa wanasindikiza magari hayo kwa ajili ya kukusanya pesa, walipofika stendi wakasimama kupakia abiria. Wamepakia abiria walipomaliza basi likaanza kuondoka,yeye alikuwa nje ya basi sasa wakati anakimbilia hilo basi ambalo lilikuwa linatoka getini likikata kona,mlango wa basi ukacheza,akadondoka chini akakanyagwa na tairi za basi hilo.
 
Mwili wa marehemu Athuman Hamad ukiwa chini baada ya kukanyagwa na basi

Mwili wa marehemu Athuman Hamad ukiingizwa kwenye gari la polisi

Share:

Afrika Kusini yapiga marufuku raia wake kutoka nje Ili Kukabiliana Na Virusi Vya Corona

Afrika Kusini imeanza kutekeleza leo amri ya watu kubakia majumbani mwao chini ya uangalizi wa jeshi, na kujiunga na nchi nyingine za Afrika zinazoweka hatua kali za watu kutotoka nje na kufunga shughuli nyingi katika jitihada za kusitisha kusambaa kwa virusi vya corona.

Watu milioni 60 nchini Afrika Kusini watalazimika kukaa nyumbani kwa siku 21.

Afrika Kusini ina visa 927 vya maambukizi ya virusi vinavyo sababisha ugonjwa hatari wa Covid-19 (Corona).

Hatua hizo zilitangazwa Jumatatu jioni na Rais Cyril Ramaphosa, ambaye alisema anataka kuzuia mlipuko wa janga la Covid-19 na kuepuka janga la kiafya.
 

"Kaeni nyumbani.... Baa, migahawa, maeneo ya starehe, mbuga, makanisa vimefungwa. Hakuna gari inyopaswa kutembea katika mitaa ya nchi hiyo.

"Maafisa pekee wanaofanya kazi katika sekta muhimu ndo ambao wanaruhusiwa kwenda kazini: hospitali, maduka ya dawa, maduka makubwa, maduka ya chakula. Watu wanaofanya kazi katika sekta za maji na umeme wanaweza pia kwenda kazi. Wafanya kazi katika sekta ya migodi ya makaa ya mawe, wataendelea kuripoti kazini.

"Ni marufuku mtu kutoka nje, barabarani, kwenda sehemu anakotaka," ameonya Waziri wa Polisi Mbeki Cele.


Share:

Marekani Yaongoza katika idadi ya Maambukizi ya Virusi Vya Corona Duniani

Marekani imeipiku China na Italia na kuwa nchi inayoongoza duniani katika maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa takwimu zilitotolewa na watafiti wa Chuo Kikuu cha John Hopkins, ni kuwa Marekani inaongoza kwa visa 83,000, ikifuatwa na China na zaidi ya 81,000 na Italia ikiwa na zaidi ya 80,000.

Kumekuwa na zaidi ya vifo 8,200 nchini Italia, ambayo ni kitovu cha mlipuko wa COVID-19 barani Ulaya, na zaidi ya 3,100 nchini China, ambako virusi hivyo vilianzia, na zaidi ya vifo 1,200 nchini Marekani. 

Wakati huo huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamewapa mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro wiki mbili kutayarisha mpango imara wa kukabiliana na athari za kiuchumi zinazokana na janga la virusi vya corona.

 Viongozi wa nchi 27 wanachama walifanya mkutano kwa njia ya video jana na kushindwa kufikia msimamo wa pamoja kuhusu mgogoro huo.

Credit:DW


Share:

SERIKALI YA CHINA YASITISHA VISA ZOTE ZA KUINGIA NCHINI CHINA NA HATI ZA UKAZI


Visa
Ubalozi wa Tanzania nchini China umeeleza kuwa kuanzia Machi 28, Serikali ya China imesitisha VISA zote za kuingia nchini China na Hati za Ukazi (residence permit), na kwamba Watanzania wenye VISA na wanafunzi wenye hati za ukazi wasitishe mipango ya kurejea China hadi itakapotangazwa.

Taarifa hiyo imechapishwa leo Machi 27, 2020, kupitia ukurasa wa twitter wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo, hatua hii ikiwa ni kuendelea kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa hatari unaosababishwa na Virusi vya Corona.

"Katika kudhibiti kuenea kwa COVID-19, kuanzia Machi 28, 2020 Serikali ya China imesitisha VISA zote za kuingia nchini China na Hati za Ukazi (residence permit), Watanzania wenye VISA na wanafunzi wenye hati za ukazi wasitishe mipango ya kurejea China hadi itakapotangazwa tena" imeeleza taarifa hiyo.
Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa March 27



















Share:

Papa Francis apimwa Corona

Kiongozi wa Kansa Katoliki Duniani, Papa Francis amepimwa virusi vya corona (covid-19) na kuthibitika kuwa hajaambukizwa.

Papa Francis alipimwa virusi hivyo baada ya mmoja wa wachungaji anayeishi katika katika makazi yake kugundulika kuwa na corona.

Vyombo vya habari nchini Italia viliripoti kuwa mchungaji huyo ambaye ni ofisa wa sekretarieti ya jimbo aligundulika kuwa na virusi vya corona na kuzua hofu kuwa huenda Papa Francis naye ameambukizwa.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya  Vatican, mchungaji huyo alikuwa mmoja wa washiriki wa karibu wa papa na sasa amelazwa katika Hospitalini ya Roma wakati idadi ya walioambukizwa katika jimbo hilo ikifikia watano.


Share:

Burundi Yakanusha Taarifa Inayosambaa Mitandaoni Kwamba Haina Vifaa Vya Kupima Corona

Burundi imedai watu wanaotumia mtandao wa internet kusema nchi hiyo haina vifaa vvya kugundua virusi vya corona kuwa ni waongo.

Kwenye taarifa iliyotolewa jana jioni, msemaji wa serikali ya Burundi Prosper Ntahorwamiye amesema nchi hiyo ina vifaa vya kutosha na vyenye ufanisi vya kugundua virusi vya corona. 

Ametolea mfano ushahidi kuwa mwalimu kutoka shule inayomilikiwa na Wafaransa aliyeshukiwa kuwa na virusi hivyo amepimwa, lakini matokeo yameonesha kuwa hana virusi.

Serikali ya Burundi imeonya dhidi ya vitendo vya kupotosha ukweli na kutafsiri vibaya maamuzi yaliyotolewa na serikali. 

Msemaji huyo amesema serikali ina madaraka ya kuchukua hatua mwafaka dhidi ya watu wanaotoa kauli zisizo za kweli.

Wakati huohuo, serikali ya Burundi imeshukuru China kwa kutoa vifaa vya kuisaidia kukabiliana na uwezekano wa mlipuko wa virusi vya Corona nchini humo.

Credit: CRI


Share:

Kenya yathibitisha kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Corona

Mgonjwa wa kwanza mwenye maambukizi ya virusi vya corona (covid-19) nchini Kenya amefariki katika Hospitali ya Aga Khan.

Taarifa hiyo  imethibitishwa na Waziri wa Afya nchini humo, Mutahi Kagwe ambaye amesema mgonjwa huyo ni mwanaume aliyekuwa na umri wa miaka 66 na alikuwa amelazwa Katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU).

“Mwanaume huyo pia alikuwa na ugonjwa wa sukari na alikuja nchini Machi 13, 2020 kutoka Afrika Kusini akipitia Swaziland,” imesema taarifa hiyo.

Kenya hadi sasa imeripoti kesi za Corona 31 tangu kutangaza mgonjwa wa kwanza Machi 13, 2020.


Share:

Maandalizi Ya Kukabiliana Na Corona Songwe Yafikia Hatua Nzuri

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameibanisha Kuwa maandalizi ya kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe yapo vizuri huku akizielekeza Halmashauri za Wilaya kukamilisha baadhi ya mapungufu yaliyopo.

Brig. Jen. Mwangela ameyasema hayo jana akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa mara baada ya kukamilisha ukaguzi wa utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona katika Halmashauri  za Mbozi, Ileje na Halmashauri ya Mji Tunduma.

Amesema watalaamu wa Afya ambao watawahudumia wagonjwa wa Corona endapo watatokea Mkoani Songwe tayari wana mafunzo na Uelewa wa majukumu yao huku Vituo vilivyo teuliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na washukiwa vimezingatia maelekezo ya Wizara ya Afya.

Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa amebaini baadhi ya vituo vya kutolea huduma kwa wagonjwa na Washukiwa wa Corona vina mapungufu kadhaa ikiwemo uhaba wa maji, umeme na baadhi ya vifaa tiba na kinga ambapo ameziagiza Halmashauri husika kukamilisha mahitaji hayo haraka sana.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa elimu ya Kujikinga na Virusi vya Corona kwa wasafiri, madereva na wafanyakazi wengine wa Mabasi katika maeneo mbalimbali huku akiwasisitiza kuchukua hatua za tahadhari kwa kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya Lazima.

Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi George Salala amewaagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha hawajazi abiria kuliko uwezo wa gari kwakuwa ni kutengeneza mkusanyiko usio wa lazima huku akisema hatua kali zitachukuliwa kwa watako kaidi.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Salala ametoa angalizo kwa abiria pia kutokubali kupanda mabasi au usafiri endapo watakuta umejaa kwani mikusanyiko kama hiyo ni mojawapo ya njia ya kusambaza ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Amesema wamiliki wa mabasi wanapaswa kuweka maji ya kunawa yenye dawa katika mabasi yao ili kuwakinga madereva wao na kuwakinga abiria dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwakuwa ili kufanikisha kutosambaa kwa ugonjwa huo inatakiwa jamii yote ishirikiane.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema mpaka sasa maandalizi ya Utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa Mkoa wa Songwe yamefikia asilimia 50 huku mapungufu yaliyobainishwa yatakamilishwa ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

Dkt Nyembea ameongeza kuwa kufuatia agizo la Serikali la kuwaweka karantini siku 14 watu wote walio toka nchi zenye maambukizi Zaidi ya Virusi vya Corona hadi sasa wamewaweka watu sita karantini waliotumia mpaka wa Tunduma kutokea nchi ya Afrika Kusini.


Share:

Uongozi Wa Wizara Ya Maliasili Na Utalii Wakutana Na Baraza La Wafugaji Ngorongoro Kujadili Fedha Za Miradi Ya Maendeleo.

Waziri wa  Maliasili  na  Utalii, Dkt.  Hamisi Kigwangalla, jana amekutana na viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro, Viongozi wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, kujadili utaratibu wa usimamizi wa fedha zinazotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa ajili ya Baraza la Wafugajji na miradi inayotekelezwa katika Tarafa ya Ngorongoro .

Fedha hizo sasa zitapelekwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro  kutekeleza shughuli zilezile zilizokuwa zinatekelezwa na Baraza la Wafugaji Ngorongoro.

Mkutano huo uliofanyika  kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Swagaswaga, umehudhuriwa na Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utaliii Mhe. Constantine  Kanyasu, Mbunge wa Ngorongoro  na Naibu Waziri wa Elimu,  Sayansi, na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda ,  Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Mfaume Taka na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Maurus Msuha.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Prof. Abiud Kaswamila, Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Freddy Manongi, Meneja wa Maendeleo  ya Jamii wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,  Bw. Fedes Mdala.  na Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro,  Bw. Edward Maura.


Share:

Thursday, 26 March 2020

Waziri Mkuu: Kamati Za Maafa Ziungane Na Waratibu Wa Kukabiliana Na Corona

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za Maafa katika ngazi za mikoa na wilaya ziungane na waratibu wa kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) waliopo katika maeneo yao.

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza Watanzania waendelee kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wanajiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na hata wakienda kwenye maeneo ya kutolea huduma kama sokoni, vituo vya mabasi wapeane nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 26, 2020) wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Kitaifa cha Kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. Kikao hicho kimehusisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipeleke wataalamu katika maeneo yenye mahitaji makubwa kama kwenye viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandarini.

“Lengo letu ni kuhakikisha nchi inabaki salama hivyo Watanzania tuendelee kuwa na tahadhari ya kutosambaa kwa ugonjwa huu na pale tunapokwenda kwenye maeneo ya kutolea huduma tujipe nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.”

Waziri Mkuu amesema kamati hiyo inatakiwa ifuatilie na isimamie vizuri ili kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapimwa na wanafuatilia ili kujua historia zao za safari katika kipindi cha siku 14, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi hayo yasisambae kwa jamii.

Amesema watu wote waliopewa dhamana ya kuratibu zoezi la kupeleka watu walioko kwenye karantini, wahakikishe wahusika wanafika kwenye hoteli walizozichagua. Pia Serikali inafanya utaratibu wa kutenga maeneo ambayo watu watakuwa wanakaa bila gharama na yatakuwa na huduma zote muhimu.

Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona, ambapo amevitaka viendelee na utaratibu huo kwani utasaidia wananchi kupata elimu na kuweza kujikinga na maabukizi hayo.

Machi 23, 2020, Waziri Mkuu aliunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).

Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo inaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wengine ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Pia, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika kikao cha leo, Waziri Mkuu ameongeza wajumbe wawili ili waongeze nguvu katika kukabiliana na virusi vua corona ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger