Taarifa ya Mtaka aliyoiandika jana kwenye moja ya mitandao ya kijamii ilisema ameagiza wateule wote wa Idara ya Elimu
mkoani Simiyu wafanyiwe uchambuzi wa historia zao (vetting).
mkoani Simiyu wafanyiwe uchambuzi wa historia zao (vetting).
“Watumishi hao watafanyiwa uchambuzi huo ambao umezoeleka kufanyika kwa watumishi wa umma wa ngazi kubwa, ili kuona kama wanakidhi mahitaji ya ukuu wa shule au uratibu wa Simiyu tunayoitaka,” taarifa ya Mtaka ilisema.
“Nimeagiza wateuliwa wote katika madaraka ya kielimu mkoani kwetu wafanyiwe ‘vetting’ juu ya mienendo na tabia zao, (na) vyombo vyetu vya usalama vitakuwa msaada katika hili.”
Lengo la mkakati huo, Mtaka alisema ili kuweka walimu, wanafunzi, shule na pesa za serikali kwenye mikono ya watu salama.
Mkuu wa mkoa huyo alieleza amefikia uamuzi huo baada ya kuona mwalimu mkuu wa miaka ya 1990-2015 si mwalimu mkuu wa leo.
Mwalimu mkuu au Mkuu wa Shule wa leo, alisema Mtaka, anapokea fedha ya serikali moja kwa moja kutoka hazina.
“Kwa maana nyingine, mkuu wa shule wa leo ni afisa mashuri katika eneo lake,” alisema Mtaka na kuongeza: “Hivyo pesa hizi zinazokuja shuleni tungehitaji kuona zinakuta mwalimu mwenye weledi, uwezo, elimu stahiki na nidhamu ya kiutumishi.”
Mkuu wa mkoa huyo alisema anakusudia, kwa pamoja na wasaidizi wake, kufanya maamuzi yenye kulenga mabadiliko chanya ya kielimu ili miaka michache ijayo, Simiyu uwe miongoni mwa mikoa itakayotamba na kuheshimika kielimu.
Mbali na mchujo kwa walimu wakuu na wakuu wa shule, Mtaka ameainisha mikakati mingine mitatu ili kuiwezesha Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa itakayotamba na kuheshimika kielimu.
Mikakati hiyo ni pamoja na kubadili fikra za wakuu hao kwamba kila takwimu inayoombwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ni kwa ajili ya kupelekewa fedha, hivyo kuwapo kwa udanganyifu katika ripoti zao.
Mataka pia amekusudia kuwafanya wakuu wa elimu mkoani humo kuacha kufanya kazi kwa mazoea licha ya kuwa wakuu hao mkoani Simiyu ni kati ya wenye hali nzuri kimapato kutokana na kuwapo kwa mradi wa kielimu ujulikanao kama EQUIP-T.
“Tatu-nimewaagiza wakurugenzi na ofisi ya katibu Tawala Mkoa kutambua walimu wote ambao wamejiendeleza ngazi ya stashahada, shahada na shahada za uzamili ili waweze pia kupewa nafasi hizi za kiuongozi katika elimu kwenye shule, kata na hata wilayani kwa zile zilizo ndani ya mamlaka yetu kama mkoa.”
SH. BILIONI 137
Serikali imetenga Sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharimia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani, kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi Desemba 20 mwaka jana.
Utoaji elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne ni ahadi ya Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, ambapo Serikali hutoa Sh. bilioni 19 kila mwezi ambazo hupelekwa na Hazina kwa kila mkuu wa shule kulingana na idadi ya wanafunzi shuleni.
Jitihada za kumpata RC Mtaka kufafanua zaidi mkakati wake huo hazikufanikiwa jana kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa