VUGUVUGU la watangaza nia ndani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchuana kuwania nafasi ya kuteuliwa
kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa rais,
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu linazidi kuwa kubwa kila
kukicha.
Idadi ya makada wa chama hicho
wanaowania nafasi hiyo, inazidi kuongezeka ambapo mpaka sasa, zaidi ya
makada 40 wamejitokeza kwenye makao makuu ya chama hicho, Dodoma na
kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Licha ya utitiri huo wa wagombea, mtu
anayetakiwa ni mmoja tu na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo
wanavyozidi kuibuka watu wanaobadili kabisa upepo wa kisiasa ndani ya
chama hicho, wengine wakipewa nafasi kubwa huku wengine wakionekana kuwa
‘mamluki’ katika safari hiyo ya kuelekea Ikulu .
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Ngoyai
Lowassa, ni kada ambaye mpaka sasa, nguvu zake za ushawishi miongoni mwa
wananchi na wanachama wa chama hicho zimejipambanua pengine kuliko
mgombea mwingine yeyote, huku akipewa nafasi kubwa ya kurithi kiti
kitakachoachwa wazi na swahiba wake wa siku nyingi, Rais Jakaya Mrisho
Kikwete.
Hata hivyo, licha ya dalili zote za
awali kuonesha kwamba Lowassa ana nafasi kubwa ya kuteuliwa na chama
hicho, hasa kutokana na jinsi anavyokubalika miongoni mwa wananchi,
akifunga mitaa kila anapokwenda kuomba udhamini mikoani, duru za kisiasa
ndani ya chama hicho, zinaonesha kwamba uwezekano wa mbunge huyo wa
Monduli kupenya ni mgumu kutokana na sababu kadha wa kadha.
Kwa mujibu wa Profesa mmoja wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam ambaye alizungumza kwa sharti la kutoandikwa
jina lake gazetini, mfumo usio rasmi utakaotumiwa na Kamati Kuu (CC) ya
chama hicho kuwachuja wagombea hao ili kumpata mmoja atakayekiwakilisha
chama, unaonesha ‘kutokuwa rafiki’ kwa Lowassa.
MFUMO UTAKAOTUMIKA
“Unajua chama tawala kinatumia mfumo wa
‘X, 5, 3, 1’, yaani maana yake ni kwamba watajitokeza watangaza nia
wengi ambao idadi yao haina kikomo (X) ambao sekretarieti kuu ya chama
itayapitia majina yote kisha kuyapeleka kwenye Kamati Kuu (CC) ambayo
itayachuja majina hayo kwa kuzingatia vigezo 13 vilivyowekwa na chama
ili kupata majina ya wagombea watano watakaopelekwa kwenye Halmashauri
Kuu.
“Majina hayo matano yatachujwa na
Halmashauri Kuu ili kupata majina matatu ambayo yatapelekwa kwenye
mkutano mkuu wa chama utakaopitisha jina moja kwa hiyo kanuni ya ‘X, 5,
3, 1’ itakuwa imetimia,” alisema profesa huyo.
UGUMU UNAANZIA HAPA
Profesa huyo aliliambia Uwazi Mizengwe kwamba ugumu kwa Lowassa kupenya kwenye mchujo huo, unatokana na sababu zifuatazo:
“Unajua hiki ninachowaambia siyo rasmi
lakini ndiyo utaratibu utakaotumika na kama hamuamini mtajionea wenyewe.
Katika majina matano yatakayopitishwa na Kamati Kuu, uwezekano mkubwa
ni kwamba chama kitazingatia mambo kadhaa.
“La kwanza ni suala la
Muungano, ili kuulinda muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara,
lazima nafasi mbili kati ya tano za watakaopitishwa, zitatoka kwa
wagombea wa Zanzibar ambapo mpaka sasa, uwezekano mkubwa unaonesha
Makamu wa Rais, Mohamed Ghalib Bilal na Jaji Mstaafu, Augustino Ramadhan
ndiyo wanaopewa nafasi.
“Pili chama kitazingatia suala la jinsia
ambapo lazima katika nafasi hizo tano, moja itaenda kwa mwanamke.
Habari za chini kwa chini zinaonesha Dk. Asha Rose Migiro ndiye mwenye
nafasi kubwa ya kupita kwa kigezo cha jinsia, kwa hiyo katika zile
nafasi tano, zinakuwa zimesalia nafasi mbili.
“Waziri mkuu ndiye mtendaji mkuu wa
serikali, kwa lugha nyingine lazima awe ni mtu anayekubalika ndani ya
chama kabla ya kupewa wadhifa huo mkubwa wa kumsaidia rais. Mizengo
Pinda amekuwa waziri mkuu wa kipindi kirefu katika utawala wa Rais
Kikwete tangu Lowassa alipojiuzulu.
“Kwa kuwa naye amechukua fomu, haitakuwa
rahisi kwa wajumbe wa kamati Kuu ‘kumchinjia baharini’. Haipo rasmi
lakini uwezekano mkubwa ni kwamba anaweza kubebwa na wadhifa wake ingawa
suala la upendeleo ndani ya chama huwa halipewi kipaumbele.
“Kama ikitokea hivyo, maana yake, tayari
kutakuwa na majina manne; Bilal, Jaji Augustino, Dk. Migiro na Pinda.
Katika ile hesabu ya majina matano yanayotakiwa, inabakia nafasi ya mtu
mmoja tu ambayo ndiyo hiyo itakayogombaniwa na akina Lowassa, Membe,
Dk.Magufuli, Profesa Mwandosya, Wasira, Makamba na makada wengine wote
waliosalia. Unafikiri itakuwa rahisi kwa Lowassa kupenya?” alisema
profesa huyo.
UPEPO WA KISIASA ULIVYO
Licha ya ufafanuzi huo jadidi kutoka kwa mtaalamu huyo wa siasa, Uwazi Mizengwe
lilienda mbele zaidi na kupima upepo wa kisiasa ulivyo miongoni mwa
watangaza nia. Katika uchunguzi huo uliofanywa na gazeti hili,
imebainika kwamba mpaka sasa hakuna mtangaza nia ambaye amekuwa gumzo
kama ilivyo kwa Lowassa.
“Jamaa anakubalika sana, tuacheni utani.
Yaani tangu siku ya kwanza alipotangaza nia pale Arusha, sote tuliona
jinsi alivyokusanya umati mkubwa wa watu ambao haujawahi kutokea na
hakuna mtangaza nia mwingine aliyevunja rekodi hiyo.
“Yote tisa, kumi ni ziara za mikoani
kusaka wadhamini zinazofanywa na Lowassa. Yaani kila mkoa anaokanyaga,
anapokelewa na maelfu ya wananchi na wanachama wa chama hicho. Maeneo
yote aliyopita ameacha gumzo. Hiyo ni ishara kwamba Lowassa anakubalika
sana,” alisema Profesa huyo, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
“Kama CCM wataamua kufumba macho na
kutozingatia kigezo cha kukubalika, basi wanaweza kulikata jina la
Lowassa lakini kama wataangalia mgombea anayeuzika kama Rais Kikwete
alivyosema kwenye maadhimisho ya miaka 37 ya CCM kule Songea, ipo wazi
kwamba Lowassa atapenya kwenye hatua zote za mchujo,” Ismail Mabula,
mtaalamu wa siasa kutoka taasisi moja isiyo ya kiserikali iitwayo Free
Political Forum, yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam aliliambia Uwazi Mizengwe.
CCM WANASEMAJE?
Uwazi Mizengwe
halikuishia hapo, liliwatafuta viongozi wa CCM na kutaka kujua
wanazungumziaje mchakato huo. Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama
hicho (jina limehifadhiwa) alipoulizwa kuhusu mchakato wa mchujo
utakavyokuwa, alisema sifa na vigezo anavyotakiwa kuwa navyo mgombea
vipo wazi na kwamba chama hicho kitasimamia kwa umakini utaratibu na
kanuni.
Alisema CCM haitachuja wagombea nje ya
kanuni na kwamba mgombea asiyekuwa na vigezo hatabakizwa kwa sababu ya
cheo chake, hasa viongozi wa serikali kwani ni wadogo kuliko viongozi wa
chama.
“Suala la kuteuliwa kutoka Kamati Kuu
kwenda Halmashauri Kuu haliangalii vyeo, ukisema Waziri Mkuu na Makamu
wa Rais wataingia kwa vyeo vyao utakosea kwa sababu kichama hao ni watu
wadogo, kama utakumbuka katika uchaguzi wa mwaka 2005, John Malecela
alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama lakini jina lake lilikatwa mapema.
“Vigezo 13 wanavyotakiwa kuwa navyo
wagombea vipo wazi, tunasubiri muda tu ili tuanze kazi ya kuwachuja
wagombea kumpata mmoja anayestahili kupeperusha bendera ya chama,”
alisema ofisa huyo mwandamizi wa chama.
Kwa mujibu wa ratiba, mchakato wa
kuchukua fomu utafikia mwisho Julai 2, mwaka huu kisha vitafuata vikao
mbalimbali vya uchujaji wa majina ya wagombea kwa kuanza na kikao cha
Kamati ya Usalama na Maadili, Julai 8.
Kikao hicho kitafuatiwa na kikao cha
Kamati Kuu (CC), Julai 9 kisha Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu
utakaofanyika Julai 12 na 13, mwaka huu ambapo hapo ndipo jina la
mgombea mmoja atakayechaguliwa litakapotangazwa
0 comments:
Post a Comment