MREMBO aliyewahi kuwa na uhusiano na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Faiza Ally, mwanzoni mwa wiki hii aliamriwa na Mahakama ya Manzese/Sinza, amkabidhi mtoto kwa
baba yake (Sugu) ambaye aliiomba mahakama hiyo imruhusu apewe mtoto huyo kwa madai kuwa mama yake huyo anamlea kinyume na maadili.
Sugu aliileza mahakama kuwa mrembo huyo hana maadili kwani amekuwa akijipiga na kumpiga picha za nusu utupu mtoto na kuziweka mitandaoni kitu ambacho aliamini kitamsababishia akose maadili.
Mara baada ya hukumu hiyo kutolewa, Mikito Nusunusu ilimtafuta Faiza na kutaka kujua ameipokeaje pamoja na historia nzima ya yeye kukutana na mzazi mwenzake huyo, shuka na mtiririko wa maswali na majibu:
Alianza lini kuvaa mavazi ya nusu utupu?
“Jamani haya mavazi wanayosema navaa uchi sijaanza kuvaa leo ni tangu utotoni, hakuna ambaye hajui kitu hicho kwa kuwa hata mama yangu alikuwa akinishonea sketi ya shule ndefu mimi naenda kwa fundi kuikata.”
Alikutana vipi na Sugu?
“Nilikutana naye kwenye Mtandao wa Facebook na alikuwa akiniona nikiwa katika mavazi hayohayo ambayo yeye anadai ni ya kuvunja maadili na alinitongoza nakumbuka nilikuwa Zanzibar kwenye hoteli moja inaitwa Lagema, ambapo nilitupia picha zangu zilezile ndipo alipovutiwa nazo akarusha nyavu.”
Hakumpa masharti ya nguo anazopenda?
“Yeye aliniambia kuwa kama ‘package’ amepata iliyokamilika kuanzia mavazi yangu ninayovaa mpaka ‘tatoo’ nilizochora hivyo alinikubali kwa jinsi nilivyo.”
Anazungumziaje kuvaa nguo fupi?
“Jamani ninachoamini mimi nguo siyo kila kitu katika maisha ya mtu, mimi ni mama wa tofauti kwa mtoto wangu hilo hata Sugu mwenyewe analijua kabisa, nimeanza kumfundisha mtoto wangu kusoma kabla hata hajaanza shule na si mtu wa kujirusha kama wanavyofikiria.”
Kumbe vimini vilianzia kwenye filamu
“Kabla sijawa na Sugu, nilikuwa na filamu yangu inaitwa Jesca, nafikiri ndiyo muigizaji wa kwanza kuvaa bikini na kutembea hadharani lakini yote hiyo ni kutokana na mazoea, hata Sugu aliiona filamu hiyo, hakuona kama ni ukosefu wa maadili.”
Alitinga ‘swimming’ akiwa na mama mkwe
“Nakumbuka mimi na mama yake Sugu tulishawahi kwenda ufukweni nikiwa na mtoto wangu na nilikuwa nimevaa nguo za kuogelea na wala haikuwa tatizo na siyo mama hata nikiwa naye mara nyingi navaa hivyo, nashangaa sasa anasema navunja maadili.”
Sugu alimkuta akiwa na maisha mazuri?
“Wakati nimeanza kuwa na Sugu hakuwa hata na kibanda alikuwa amepanga na nilimuambia kuwa hadhi yake hapaswi kuwa hivyo, tulinunua kiwanja na tukajenga nyumba Mbeya tena kwa kuisimamia huku akikiri kuwa alimshukuru Mungu kunikutanisha naye.”
Unawaambia nini Watanzania?
“Nawaomba sana Watanzania wasitumie nguo niliyovaa siku ile (kwenye Tuzo za Kili 2015) iliyoniacha wazi kwa bahati mbaya kuwa fimbo ya kunichapia, nina vitu vingi sana nimefanya kwa jamii yangu, kama kuwatembelea wagonjwa, kufanya usafi mahospitalini na hata kutembelea watoto yatima mbona hivyo havionekani?”
Vipi maisha yake bila Sasha?
“Bila Sasha kwangu hakuna maisha kabisa ni bora kufa kuliko kukaa mbali na mtoto wangu kwa kuwa ndiye kila kitu kwangu na wala siwezi kupata usingizi mpaka mtoto wangu atakaporudi mikononi mwangu, nimeshaanza process za kukata rufaa.”
Kumbe sugu alimtambulisha Bilicanas
“Sugu alinitambulisha katika Ukumbi wa Bilicanas tena mbele ya kadamnasi kuwa mimi ni mchumba wake tena nikiwa nimevaa nguo fupi kabisa, hapo pia hakuniona?”
Nini chanzo cha kugombana?
“Wala hakuna ugomvi mkubwa, nafikiri tu upendo ulianza kupungua kwa kuwa niliondoka Mbeya kwenda kumsaidia mama yangu kuhama, yeye alikuwa hataki niondoke hiyo ndiyo sababu kubwa.”
0 comments:
Post a Comment