Nawasikitikia Watanzania wenzangu waliokaa mkao wa kula wakisubiri Katiba mpya.
Nasikia wengine wanafunga na kuomba ili Katiba ipatikane, wengine wamejawa tu na matumaini.
Ya Mungu mengi, inawezekana Katiba Mpya ikapatikana, lakini kwa mwendo huu, tayari matumaini yametoweka.
Kinachoendelea bungeni kwa sasa kimeanzia mbali. Mtoto wa nyoka ni nyoka, usijidanganye ukamsogezea kidole.
Wengi walijaa matumaini mwishoni mwa mwaka 2011 baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.
Ilikuwa ni ajabu kwani suala hilo halikuwepo
kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010, tofauti na vyama vya upinzani
kama vile, CUF na Chadema.
Kabla ya tangazo la Rais Kikwete aliyekuwa Waziri
wa Sheria na Katiba, Celina Kombani alipoulizwa kuhusu mchakato huo,
aliruka kimanga akisema hautakuwepo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema naye aliwakaripia waandishi wa habari Ikulu mjini Dar es Salaam
walipomuuliza kuhusu mchakato huo.
Maana yake CCM na serikali yake hawakuwa tayari na
mabadiliko ya Katiba asilani, lakini kwa mshangao, Rais Kikwete
akatangaza mchakato huo.
Pengine aliusoma upepo wa siasa, akaona aweke
kando woga wa CCM na kuichukua hoja ya Katiba mpya katika muda ambao
hakukuwa na maandalizi ya kutosha kubeba mzigo huo mkubwa.
Baada ya hapo Tume ya Mabadiliko ya Katiba (TMK)
ikaundwa. Makamishna wakateuliwa na kulipwa mishahara na masurufu ili tu
watayarishe rasimu bora ya Katiba.
Tayari rasimu ya kwanza na ya pili zimetolewa na
mambo yamebadilika kabisa. Kisa tu, rasimu imetaja muundo wa Muungano wa
serikali tatu, ambao CCM hawautaki; ukweli unauma.
0 comments:
Post a Comment