WATU 18
wamekufa papo hapo wakiwemo askari Polisi wanne katika ajali ya
barabarani, wakati basi linalomilikiwa na Kampuni ya Sumry, lilipopamia
watu hao wakati wakimsitiri mtembea kwa miguu, aliyekufa kwa kugongwa na
gari lisilofahamika.
Ajali
hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Utaho, kilometa 20
nje ya Mji wa Singida katika Barabara Kuu ya Singida Dodoma.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi Mwandamizi, Geofrey
Kamwela, alisema jana kuwa mbali na askari hao, wengine waliokufa papo
hapo ni viongozi watatu wa kijiji hicho na wananchi wanaowaongoza na
wengine wanne ambao hawajatambulika.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kamwela, askari waliokufa katika ajali hiyo ni Koplo
Boniface Magubika, PC Jumanne Mwakihaba, PC Novatus Tarimo na PC Michael
Mwakihaba na wote wanatoka katika kituo kimoja cha kazi.
Viongozi
wa Kitongoji na Kijiji cha Utaho waliokufa ni Ramadhan Mjengi, ambaye ni
Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Paul Hamis, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji na
Ernest Salanga ambaye ni Mwenyekiti Kitongoji.
Wananchi
wanaowaongoza katika kijiji hicho waliokufa ni Saidi Rajabu, Ushirika
Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na
Issaha Hussein.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kamwela, miili ya watu wengine wanne haikuwa rahisi
kutambulika mara moja na wote wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa
mjini Singida.
Kamanda
Kamwela alisema ajali hiyo ilisababishwa na basi la abiria lenye usajili
namba T.799 BET aina ya Nissan, mali ya Kampuni hiyo ya Sumry,
inayomilikiwa na Mohamed Abdallah wa Sumbawanga, lililokuwa likienda
jijini Dar es Salaam likitokea Kigoma.
Alisema
kuwa basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Paul Njilo, mkazi wa Dar es
Salaam, liliwagonga waenda kwa miguu hao waliokuwa wamekusanyika kando
ya barabara wakisaidiana na askari Polisi kuondoa mwili wa marehemu
Gerald Zephania, aliyekuwa amegongwa na lori lisilofahamika juzi saa
moja usiku.
Katika
ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, watu wengine wanane
walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Puma ya mjini
Singida.
Habari
kutoka eneo la tukio zinasema kilichosababisha ajali hiyo huenda ni
kuegeshwa vibaya kwa gari la Polisi, wakati likipakia mwili wa marehemu
Gerald, aliyekuwa amegongwa na lori mapema kabla ya basi hilo kufika
hapo. Inadaiwa gari la Polisi liliziba barabara.
Akizungumzia
ajali hiyo katika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam jana, Kamishna
Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alitoa pole kwa
wananchi wote waliofiwa na ndugu zao na kuwaombea majeruhi kupona
haraka.
Alisema
Askari wa Usalama Barabarani hawatakuwa na muhali na dereva yeyote
atakayekwenda kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani. Kutokana na hilo,
ametoa mwito kwa madereva kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
usalama barabarni, ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Polisi
iko imara kuchukua hatua zozote za kisheria, kwani kuna baadhi ya watoa
huduma wa usafiri hugoma pale wanapotaka kuchukuliwa hatua kwa sababu
mbalimbali matokeo yake ni uvunjaji wa sheria kwa makusudi,” alisema.
Alisema
Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali wa dereva wa basi hilo ambaye
alitoroka ili kufikishwa mahakamani, na kuwaomba wananchi kuendelea
kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa aina yeyote ile, ili
wakamatwe na kufikishwa mahakamani. Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida
na Theopista Nsanzugwanko, Dar (CHANZO: HABARILEO) (FS)
0 comments:
Post a Comment