Tuesday, 27 September 2022

SAMIA SCHOLARSHIP KUANZA RASMI KWA WAHITIMU WENYE UFAULU WA JUU MITIHANI YA KIDATO CHA SITA TAHASUSI ZA SAYANSI

...



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda..

Baadhi ya wadau wa  Elimu waliohudhuria  kwenye kikao maalum cha Menejimenti ya Wizara ya elimu nchini Jijini Dodoma .

Na Dotto Kwilasa,DODOMA


WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza rasmi kuanza kwa programu ya ufadhili wa masomo iitwayo 'SAMIA SCHOLARSHIP' utakaosaidia kuchochea ari kwa wanafunzi kuongeza bidii kwenye  masomo ya Sayansi utagharamia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Chuo Kikuu hapa nchini.

 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ameeleza hayo leo Sept 27,2022 Jijini hapa kwenye kikao maalum cha Menejimenti ya Wizara na wadau wa elimu na kueleza kuwa ufadhili huo ni mpya hapa nchini .


Amesema ufadhili  huo utahusisha
 masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2022 iliyoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN).

"SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba,"amesema.  

Akieleza sifa za kupata ufadhili huo Waziri Mkenda amesema utatolewa kwa wahitimu wa kidato cha sita  wenye sifa za uraia halali,ufaulu wa juu kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2022 iliyoendeshwa na NECTA katika tahasusi za sayansi ikiwa ni pamoja  na kupata udahili katika programu za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Tiba katika Chuo Kikuu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali.

"Sifa hizi lazima ziwe ambazo zimetajwa katika kundi la kwanza (Cluster 1) katika Mwongozo wa utoaji mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2022/2023 unaopatikana kupitia www.heslb.go,tz  ambapo mwanafunzi sharti awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa,"amefafanua Waziri Mkenda. 

Sambamba na hayo ameyataja maeneo ya ufadhili huo kuwa yatazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kugharamia ada ya mafunzo,posho ya chakula na malazi,posho ya Vitabu na viandikwa,mahitaji Maalum ya vitivo na mafunzo kwa vitendo.

Maeneo mengine ni utafiti wa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na bima ya Afya ambapo muda wa ufadhili kwa watakaofadhiliwa, watagharamiwa kati ya miaka mitatu (03) hadi mitano (05) kulingana na programu husika walizodahiliwa.

Prof.Mkenda ameeleza pia taratibu za kuomba ya ufadhili wa Samia Scholarship kuwa yatapaswa kuwasilishwa kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao https://ift.tt/3RuzYsB kwa siku 14 kuanzia Septemba 28, 2022.


Ametaja masharti ya ufadhili huo kuwa Mwanafunzi atakaepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atawajibika kuzingatia kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya fedha atakazolipwa moja kwa moja.

"Mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,mnufaika hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika,ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili kabla ya kuanza masomo, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenda kwa Katibu Mkuu,Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mji wa Serikali Eneo la Mtumba ,"Amesema

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amesema uchambuzi huo wa wanufaika 640 wa SAMIA SCHOLARSHIP umezingatia uwiano wa Wasichana 244 na asilimia 38% na Wavulana ni 396 sawa na asilimia 62% na kwamba Wanafunzi kutoka shule za serikali ni 396 sawa na asilimia 62% wakati Wanafunzi kutoka shule za binafsi ni 244 sawa na asilimia 38%.

Amefafanua kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa juu kiwango cha Alama tatu (3) ni 60 (9%)Wanafunzi kutoka  shule za Tanzania Visiwani ni 43 (7%)Wanafunzi kutoka shule za Tanzania Bara 597 (93%)Aidha jumla ya wanafunzi 11 wenye mahitaji maalumu watanufaika na Samia Scholarship.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger