Thursday, 15 September 2022

OJADACT YATOA MAPENDEKEZO KUKOMESHA MATUKIO YA MAUAJI YANAYOENDELEA NCHINI NA KULETA HOFU KWA JAMII

...
 

TAARIFA  KWA UMMA


 MATUKIO  YA MAUAJI  YANAYOENDELEA  NCHINI    NA  KULETA   HOFU  KWA JAMII 


 Septemba 15, 2022


Chama  Cha  Waandishi wa Habari  za Kupiga Vita  Matumizi ya  Dawa za Kulevya  na Uhalifu  Tanzania (OJADACT) kinalaani   mwenendo wa matukio  ya mauaji yanayoendelea kwenye jamii na kusababisha  hofu  kwa jamii  pamoja  na kupoteza nguvu  kazi  ya  Taifa.


OJADACT inasikitika  kuona  matukio  hayo yakiendelea kutokea  na kuchafua  taswira  ya  Taifa  kwenye kulinda  amani  na usalama wa raia wake pamoja na kutumia  rasilimali   nyingi  za Taifa  kwenye  kupambana  na  vitendo  vya  kihalifu.


Baadhi  ya matukio yaliyotokea ni tukio  la  Septemba 14, 2022,  la mauaji  ya Mwanafunzi wa Chuo  Kikuu,  Maria Bosco  lililotokea  eneo  la  Kawe Mzimuni, Jijini  Dar es salaam lililofanywa  na vijana  zaidi  ya thelathini ambao  walitekeleza mauaji , kujeruhi na kupora  vitu mbalimbali  vikiwemo  simu  na fedha.


Tukio  jingine,  tukio  la  mauaji   ya  watu  wanne lililotokea Jijini Mbeya  ambapo Mwalimu wa Shule  ya  Msingi  Bwana Saimon Mtambo (44) alimkata  mapanga   mke wake  na watoto wake wawili  na kisha yeye  kunywa  sumu  na kupoteza Maisha.


Tukio  jingine,  tukio  lililotekea Mkoa wa Mtwara, ambapo Kijana  Kristatus  Victory (23) Mkazi wa Lukuledi Wilaya ya  Masasi anatuhumiwa kumuua  Baba  yake  Mzazi Victory  Milanzi (74)kwa madai ya kushindwa kumtafutia  mchumba wa kuoa.


Tukio jingine, tukio  la  Mkazi wa Kihesa Kilolo Mkoani Iringa Enea Mkimbo (55) aliyefariki  Dunia  baada  ya kujinyonga  kwa kutumia  kitenge  kwa madai  ya  kuzongwa na madeni ya  vikoba.


OJADACT imebainisha  matukio  haya  Machache  ikiwa ni sehemu  tu  ya  matukio  yanayoendelea  kwenye  jamii,  matukio   hayo yamekuwa yakisabishwa na sababu  mbalimbali ikiwemo, tamaa za kujipatia  fedha, wivu wa kimapenzi,  mmomonyoko  wa maadili , hali ngumu  ya maisha na  ushirikina  na mani  potofu  kwenye  jamii.


OJADACT inatoa  mapendekezo  yafuatayo.


1.      Kuundwa kwa mkakati  wa kitaifa wa  kuzuia  uhalifu   ili  kusaidia  kupunguza matukio haya  ya  mauaji  na  uhalifu mwingine kwa kuwaleta wadau pamoja na kuweka mikakati mahususi.


2.      Kuimarisha  maadili  ndani  ya  jamii  ili  kuwa na  jamii yenye  kuheshimu  utu na ubinadamu.


3.      Serikali  kupitia  taasisi zake za kupambana  na uhalifu  pamoja  na ustawi  wa jamii  kufanya  tafiti  za kutosha ili  kugundua chanzo  cha  mauaji  na uhalifu Nchini.


4.      Jeshi  la Polisi kuongeza  kasi  ya  kupambana na matukio  ya  kihalifu  hasa  vikundi  visivyo  rasmi  vinavyofanya  uhalifu.


5.      Vyombo  vya  habari na taasisi  za  kihabari kutengeneza maudhui yenye  kuhamasisha  watu  kutofanya  uhalifu  Zaidi  kuliko  kuripoti  matukio  ya  kihalifu Zaidi.


 *Edwin Soko* 

 *Mwenyekiti* 

 *OJADACT* 

 *15.09.2022*

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger