**************************
Na Mwandishi Wetu,
Cape Town, Afrika Kusini
25 Septemba, 2022
Taasisi 11 zinazotoa mikopo ya elimu ya juu barani Afrika zinatarajia kuanza mkutano wao wa kimataifa wa siku nne utakaoanza kesho Jumatatu Septemba 25, 2022, Cape Town, Afrika Kusini ambapo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki mkutano huo unaojadili uzoefu uliopatikana kutokana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19.
Akizungumza moja kwa moja kutoka Cape Town, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema mkutano huo umeandaliwa na nchi wanachama 11 ambazo ni Shirikisho la Taasisi za kiserikali zinazotoa Mikopo ya Elimu ya Juu Afrika (AAHEFA) na jumla ya washiriki 150 wakiwemo wakuu wa nchi, wajumbe wa bodi na maafisa waandamizi kutoka nchi wanachama wanatarajia kushiriki mkutano huo.
“Mara ya mwisho tulikutana mwaka 2019, Lusaka Zambia…… yapo masuala mengi yanayojitokeza baada ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19 ambao ulizuia mikutano ya ana kwa ana. Tukiwa kama nchi mwanachama, tumefika katika mkutano huu kwa ajili ya kujifunza kutoka kwa wenzetu na kupata uzoefu wa namna tunavyoweza kusimamia mikopo katika taasisi za elimu ya juu”, Mkurugenzi Badru na kuongeza:
“Kama nchi, ushiriki wetu katika mkutano huu umedhihirisha umuhimu wa kuimarisha utendaji wetu hususani matumizi ya teknolojia. Kwa mwaka huu msafara wetu unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Hamisi Dihenga” amesema Badru.
Kwa upande wake, Rais wa AAHEFA ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Kenya (HELB), Charles Ringera akizungumza kutoka Cape Town amesema mkutano huo wa tatu wa AAHEFA utakuwa na kauli mbiu isemayo: Uendelevu wa Mikopo ya wanafunzi na taasisi za mikopo ya Elimu ya Juu – Je kuna fursa zipi baada ya ugonjwa wa UVIKO 19?
Ringera amesema mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Ubunifu wa Afrika Kusini Dkt. Blade Nzimande na utakuwa na jumla ya mada 10 na kutakuwa na maazimio mwisho wa mkutano.
“Kesho tutakuwa na mada kutoka kwa wenzetu wa NSFAS taasisi ya mikopo ya elimu ya Afrika Kusini ikizungumzia kuhusu Sera ya elimu ya juu na itawasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Elimu ya Juu na Mafunzo wa NSFAS, Dkt. Nkosinathi Sishi na mada nyingine itawasilishwa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Vyuo Vikuu vya Kenya Prof. Karuti Kanyinga”, amesema Ringera.
AAHEFA ni Shirikisho lilioanzishwa mwaka 2008 na Taasisi za Serikali zinazosimamia mikopo ya Elimu ya Juu Barani Afrika lililoanzishwa mahsusi kwa ajili ya kubadilishana ujuzi na uzoefu wa masuala ya usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu. Nchi wanachama wa AAHEFA ni Afrika Kusini, Tanzania, Malawi, Botswana, Ghana, Kenya na Lesotho. Nchi nyingine ni Rwanda, Namibia, Uganda na Zambia.
0 comments:
Post a Comment