Hakuna ubishi kuwa mgombea
mteule wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. John Pombe Magufuli ana
ushawishi mkubwa nchini. Hata hivyo, hii si sababu ya wapinzani chini ya Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kumgwaya.
Baada ya
kuteuliwa Magufuli, wengi walisikika wakisema sasa kiatu kimepata mvaaji. Ni kweli,
lakini hata UKAWA wanao wavaaji wa kiatu sawa na Magufuli. Katika kuthibitisha
hilo Dk Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLD kinachounda UKAWA alikaririwa
akisema, “Hatustushwi na (Dk John) Magufuli kwa lolote na mashambulizi yetu
yatakuwa makubwa. Lengo letu la kuiondoa CCM madarakani liko palepale.” Maneno ya
Makaidi yana ukweli. Wale wanaodhani wapinzani wanamgwaya Magufuli wanataka
apitishwe bila kushiriki uchaguzi?
Nadhani Makaidi
ana sababu nzuri tu za kusema hawatishwi na Maguguli. Anasema, “Ajenda na hoja tulizonazo ndizo
zitakazotubeba mbele ya wananchi… tutawapelekea ili waamue wakiwa na taarifa
sahihi. Kama ni kutowajibika au ufisadi ndani ya CCM, suala hilo linaanzia
ngazi ya juu mpaka kwa mwanachama wa kawaida.” UKAWA bado wana imani kuwa
wananchi watawaelewa hasa pale watakapowakumbusha utendaji mbovu wa CCM.
Pia ni vizuri
tukaamini kuwa kwenye siasa lolote linaweza kutokea. Nani aliamini kuwa rais
Uhuru Kenyatta wa Kenya angemshinda waziri mkuu wa zamani Laila Odinga ambaye
hata rais wa zamani Mwai Kibaki alimgwaya kama umeme? Japo siasa za Tanzania na
za Kenya ni tofauti, bado ni mapema kwa yeyote kusema atashinda. Hatujui
wananchi hasa wapiga kura wanafikiri nini na wataamua vipi. Hivyo, ushauri wa
maana hapa ni kwa wagombea wote kutobweteka na umaarufu walio nao bali kwenda
kwa wananchi na kueleza sera zao ili wapate nafasi nzuri ya kuamua.
Japo Magufuli
anajulikana kwa utendaji wake, vile vile chama chake kinajulikana kwa utendaji
mbovu. Hii dichotomy, au ndiyo siyo ni vizuri ikazingatiwa katika kuelekea
uchaguzi ujao. Sidhani kama wananchi ambao bado hawana barabara maji wala umeme
wana wanachoona ni bora kwa Magufuli. Sidhani kama wananchi ambao ardhi yao
imetwaliwa ima na wawekezaji au viongozi wa CCM wanacho cha mno wanachokiona
CCM. Sidhani wajawazito wanaotimliwa na manesi kiasi cha kuzalia vyooni wanacho
cha mno katika CCM.
Kimsingi,
hali ya CCM bado ni ngumu sema unafuu ilio nao ni kuwa na mgombea ambaye hana
tuhuma za ufisadi ua uzembe. Kwa umaarufu, uchapakazi na uzalendo alio nao
Magufuli anaweza kushinda. Lakini CCM
itegemee kuwa na hali ngumu kwenye ubunge. Maana wabunge wengi wanaomaliza muda
walichakachua kiasi cha wengine kuchukiwa vibaya sana kwenye majimbo yao. Sijui
wabunge kama hawa watarudi. Sidhani –kwenye uchaguzi ujao –kama wananchi
wataruhusu uchakachuaji kama ule tulioushuhudia mwaka 2010. Nadhani wananchi
sasa wamechoka na wako tayari kusimamia haki zao kuliko wakati wowote katika
historia ya taifa letu. Hivyo, CCM wanapaswa kulizingatia hili huku na
wapinzani wakizidi kuhanikiza kufichua maovu ya CCM kama taasisi badala ya
kuhangaika na mtu mmoja.
Nadhani Makaidi
anaposema tutabebwa na hoja anatoa onyo kwa CCM kuwa wasibwete na Magufuli. Wanajua
fika kuwa mtu hawezi kuzidi chama. Wana mifano hai ya watu waliongia wakiitwa
Mr Clean wakaondoka wanaitwa Mr Dirt.
Kitu kingine
wanachopaswa kuzingatia wananchi si ukubwa jina la mtu wala umaarufu wake bali
sera anazokwenda nazo kwao na utekelezaji wake.
CCM pamoja na
Magufuli wanapaswa kujifunza toka kwenye mchakato wao ulioisha na kumuibua
Magufuli. Nani alijua kuwa Magufuli angewapiku vigogo waliokuwa wanajiamini
kuwa ndiyo watakao kuwa wao kwenye kupeperusha bendera ya CCM? Nani alitarajia
vigogo kama Edward Lowassa, Bernard Membe na Mark Mwandosya kuangukia pua na
kushindwa na rookie kama Magufuli? Huo ndiyo uchaguzi. Si vyema kuwasemea
wapiga kura au kujaribu kutabiri watafanya nini. Kinachopaswa kufanya kwa pande
zote ni kuheshimu kanuni na kupeleka sera kwa wanachi huku wale walioko
madarakani wakitakiwa kutoa maelezo yanayoingia kichwani pale walipoboronga.
Kama watanzania
watajifunza tokana na makosa yao, tunaweza hata kutegemea maajabu. Jakaya Kikwete
aliingia na sifa nyingi za kweli na za uongo. Je anaondoka na hizo sifa tena? Unategemea
nini kama wapinzani watatumia udhaifu wa Kikwete wakiupambanisha na ahadi na
sifa alizoingia nazo kumbomoa Magufuli? Kwangu mimi ngoma hii bado ni mbichi na
lolote linaweza kutokea kufikia Oktoba.
Mfano mzuri
ni ile hali ya Magufuli kuanza kuona hatari inayokabili chama chake hasa
kuhusiana na ufisadi. Ameanza kuto ahadi za kutomugopa yeyote wala kumuonea. Je
hii inatosha? Atakapokwenda kwa wananchi watamuuliza nini atakachofanya
kuhusiana na mazimwi kama EPA, Richmond na Escrow. Majibu atakayotoa na
usayansi wake vinaweza kuwa vigezo amuzi kuliko mtaji alio nao wa kuwa
mchapakazi bora na kusifika kusimamia ujenzi wa barabara. Je hizo barabara
zinakidhi viwango au kulingana na kiasi cha fedha kilichotumika kuzijenga? Maswali
mbona yapo mengi kuanzia ya barabara hadi nyumba za umma zilizouzwa chini ya
usimamizi wake.
Tumalizie kwa
kuzishauri pande zote kujikita kwenye masuala badala ya personalities.
Chanzo: Dira Julai 23, 2015.
0 comments:
Post a Comment