Friday, 10 July 2015

MKOA WA MBEYA WAGAWANYWA ,ANGALIA HAPA WILAYA MPYA

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY



Serikali imegawanya mkoa wa Mbeya na kupata mkoa mpya wa Sogwe na kuanzisha wilaya mpya sita, halmashauri 25, manispaa 17, tarafa tano na kata 586 nchini.

Akihitimisha Bunge la 10, Mkutano wa 20, mjini Dodoma jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema mgawanyo huo umetokana na Rais Jakaya Kikwete kuridhia kugawanywa kwa maeneo hayo mapya ya utawala.

Alisema lengo la mgawanyo huo ni kusaidia kusogeza utawala na usimamizi na kusogeza shughuli za maendeleo karibu na watu.

Pinda alizitaja wilaya mpya kuwa ni Tanganyika (Katavi), Ubungo, Kigamboni (Dar es Salaam), Sogwe (Mbeya), Kibiti (Pwani) na Malinyi (Morogoro).

Alizitaja halmashauri mpya kuwa ni Buchosa, Malinyi, Madaba, Manyoni, Mpimbwe, Msimbo, Mlele, Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kyerwa, Chemba, Mbogwe, Nyang'wale, Butiama, Momba, Nyasa, Bushetu, Busega, Itilima, Ikungi, Mkalama, Msalala, Kaliua na Bumbuli.

Pinda alitaja miji na manispaa kuwa ni Chalinze, Ifakara, Nanyamba, Newala, Kondoa, Mafinga, Mbulu, Bunda, Mbinga, Tunduma, Handeni, Nzega, Kasulu, Geita, Masasi, Ilemela na Kahama.

Alisema pia kuna tarafa moja katika wilaya ya Newala ambayo ni Mchemwa, nyingine nne zipo wilaya ya Tandahimba, Mchichira, Mwihambwe, Mabamba na Mangombiya.

Alisema serikali itaweka mfumo imara na usimamizi madhubuti ikiwamo maafisa masuhuru kutakiwa kubana matumizi hasa katika ununuzi wa umma, kudhibiti uendeshaji wa semina zisizo za tija, ununuzi wa magari, gharama za umeme, simu na maji.

Alisema rafiki wa serikali ni yule anayelipa kodi ili kuiwezesha kutekeleza shughuli za maendeleo.

UANDIKISHAJI BVR
Kuhusu uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kupitia mfumo wa kielektroniki (BVR), Pinda alisema uandikishaji unaendelea katika mikoa 11 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kupata fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka kupitia uchaguzi mkuu wa madiwani, ubunge na rais utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

MALIPO YA MADIWANI
Alisema malipo ya madiwani yalishawasilishwa Hazina mwaka jana na kutengwa kupitia kifungu cha 21 cha Wizara ya Fedha na tayari maelekezo yametolewa ili stahili zao zisichelewe zilipwe sambamba na malipo ya wabunge.

Waziri Mkuu alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeongezeka kutoka halmashauri 133 mwaka wa 2005/2006 hadi kufikia halmashauri 168 mwaka wa 2014/2015.

"Lengo kuu likiwa ni kupanua na kuimarisha demokrasia na kupeleka madaraka na huduma karibu zaidi na wananchi.

Rasilimali watu katika mamlaka hizo iliongezeka zaidi kwenye sekta za elimu ya msingi na sekondari ili kukabiliana na ongezeko la miundombinu na wanafunzi ambao wamefikia 8,202,892 mwaka wa 2015," alisema na kuongeza:

"Walimu wa shule za msingi waliongezeka kutoka 135,013 mwaka wa 2005 na kufikia 190,957 mwaka 2015. Aidha, wanafunzi wa sekondari waliongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi kufikia 1,704,130 mwaka wa 2015, walimu wa sekondari waliongezeka kutoka 20,754 mwaka 2005 na kufikia 80,529 mwaka wa 2015."

Aidha, Pinda alisema wakati wa kikao cha Bunge la 10, Mkutano wa 20 kilichomalizika jana, jumla ya maswali 336 ya msingi na 879 ya nyongeza yaliulizwa na wabunge na kujibiwa na serikali, huku maswali sita ya msingi na matano ya nyongeza yakiulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu kwa utaratibu wa maswali ya papo kwa papo.

MAONI YA WADAU
Wadau kadhaa walitoa maoni tofauti kuhusiana na uamuzi wa serikali kuongeza idadi ya wilaya zikiwamo za mkoa wa Dar es Salaam kutoka tatu hadi tano.

DK: BANA
Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kimsingi, matatizo hayatatuliwi kwa kuongeza warasimu na gharama za matumizi.

“Kutatua matatizo siyo kuongeza wilaya, bali kupeleka madaraka katika serikali za mitaa ambazo zinajenga barabara zao, vituo vya afya, maji na shule kwa kutumia fedha kutoka Serikali Kuu,” alisema Dk. Bana.

Alisema kwa mfano matatizo ya jiji la Dar es Salaama yanaweza kutatuliwa kwa kuongeza idadi ya halmashauri na mitaa pamoja na kuzipa fedha zaidi kutoka Serikali Kuu.

Hata hivyo, mhadhiri huyo alitofautiana na watu wanaopendekeza kwamba matatizo ya jiji la Dar es Salaam yanaweza kutatuliwa kwa kuundiwa wizara maalum.

Badala yake alisema kinachotakiwa ni kupeleka madaraka zaidi kwa watu na kuwawezesha kwa rasilimali fedha na rasilimali watu.

PROF. BAREGU
Prof. Mwesiga Baregu, alisema kuanzishwa kwa wilaya za Ubungo na Kigamboni, mkoani Dar es Salaam siyo mkakati wa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, bali ni mkakati maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutafuta ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema haiwezekani kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu ndipo serikali iongoze wilaya katika jiji la Dar es Salaam.
“Nadhani huu ni mkakati maalumu ambao unahusiana na uchaguzi mkuu ujao ambao unalenga kuiba kura au kuvuruga uchaguzi ujao,” alisema Prof. Baregu.

Kwa mujibu wa Prof. Baregu, mpango huo umetokana na kuona kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) una nguvu kwa jiji hilo, hivyo watumie nguvu ya ziada kuizima nguvu hio.

BASHIRU ALLY
Mhadhiri wa UDSM, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Bashiru Ally, alisema uamuzi wa kuongeza wilaya katika mkoa wa Dar es Salaam ni mzuri kwa kuwa una idadi kubwa ya watu.

Alisema hiyo itasaidia namna ya kushughulikia shughuli mbalimbali za kijamii, yakiwamo masuala ya usalama, miundombinu na usafi.

“Kwa mkoa wa Dar es Salaam ni sahihi kuongeza wilaya hizo kwani umekua sana na una idadi kubwa ya watu na hata kuhudumia shughuli nyingine za kijamii inakuwa shida, hii itasaidia sana hata katika upande wa kuimarisha huduma hizo hasa usalama,” alisema.

Aidha, alisema suala la kupanga ni kuchagua, hivyo ni vema serikali kama imeamua kuongeza wilaya, inabidi ijipange pia katika kutenga fedha za kuzihudumia.

“Mimi nina amini mpaka serikali inaamua kuongeza wilaya hizo imejipanga, Dar es Salaam siyo kubwa sana, lakini ina matatizo makubwa, inabidi kuwapo na mpango mahususi wa kuziwezesha wilaya hizo zilizoongezeka,” alisema. 

Imeandikwa na Salome Kitomari, Dodoma, Mary Godfrey na Elizabeth Zaya, Dar es salaam 
-Nipashea
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger