Ni siku
nyingine tena tunakutana katika kona yetu ya Vituko Mtaani, leo
tunapata simulizi kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbuyuni,
Kata ya Azimio, Temeke jijini Dar es Salaam, Selemani Mponyo (pichani),
hapa anaanza kusimulia kisa cha kusisimua.
“Mambo mengine ni aibu kuyaongea kwa
umri kama wetu lakini ngoja nisimulie ili watu wajifunze. Ni kipindi
kirefu sasa tangu niamue kesi iliyonishangaza sana.
“Siku moja walikuja mke na mume ofisini,
mume akimtuhumu mkewe kwa kutembea na mwenye nyumba
wao. Alidai kuwa
mkewe ndiye aliyetafuta chumba na baada ya kupata, akamtaka yeye kwenda
kulipia, lakini alifanya hivyo bila kujua kuwa tayari mwenye nyumba
alishampa maneno matamu mkewe.
“Alisema muda mfupi baada ya kuhamia
katika makazi hayo mapya, alianza kuingiwa na wasiwasi baada ya kuona
ukaribu kati ya mkewe na mwenye nyumba unavuka mipaka, maana yule jamaa
alikuwa akimletea zawadi mara kwa mara na kuwasiliana kwa meseji za
mapenzi usiku.
“Mume alidai baada ya uchunguzi wake,
akathibitisha kuwa mkewe anashiriki mapenzi na mwenye nyumba, akampa
kibano kikali akakiri jambo hilo na akaomba msamaha akidai hatarudia.
Mume pia akaenda kwa mwenye nyumba ambako jamaa naye alikiri kitendo
hicho, lakini akadai mkewe ni mwenye tamaa kwani alimtaka awe anampa
hela ya kodi inayotolewa na mumewe.
“Mwanaume huyo alidai baada ya mwenye
nyumba kukubali aliamua kumfukuza mkewe lakini watu walimshauri si
busara ndiyo maana akaamua kuja kwangu nipate kumshauri.
“Kesi hii ilinishangaza sana, nilimshauri kama kweli ameamua kumsamehe ni vyema akahama ule mtaa na wasahau yote yaliyopita.”
Kama una kituko cha kusisimua wasiliana
nami kupitia namba ya simu iliyopo hapo juu, angalizo ni lazima awe
mjumbe wa mtaa, mwenyekiti au afisa mtendaji.
0 comments:
Post a Comment