Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi imemuhukumu Lazaro Charles (35) Mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema katika Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi kutumikia jela kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumpa mimba mtoto wake wa kumzaa mwenye (14) ambaye ni, mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Majengo Manispaa ya Mpanda.
Hukumu hiyo iliyovuta hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya Mpanda, ilitolewa na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Gosper Luoga baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani na upande wa mashtaka.
Awali katika kesi hiyo Mwanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti hapo Januari 1 mwaka 2017 na April 29, 2019.
Mshtakiwa huyo alikuwa akitenda kosa hilo huko nyumbani kwake wakati mke wake ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo alipokuwa amesafiri ndipo alipokuwa akiingia kwenye chumba alichokuwa akilala mtoto wake huyo na kumbaka kwa nguvu.
Mwendesha mashtaka huyo alieleza kuwa baada ya kuwa anambaka alikuwa akimwekea majani kwenye sehemu zake za siri kama dawa ya kienyeji ya kumwondolea maumivu.
Hakimu Luoga amemtaka mshtakiwa kama atakuwa na sababu yoyote ile ya msingi ambayo inaweza kuifanya mahakama iweze kushawishika ili kumpunguzia adhabu basi inatoa nafasi kujijitetea.
Lazaro Charles ameiomba mahakama impatie nakala ya hukumu ya mwenendo wa kesi hiyo tu kwani hana utetezi wowote ule.
Baada ya ombi hilo la mshtakiwa mwanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.
Hakimu Luoga baada ya kusikiliza pande hizo mbili alisoma hukumu na kuiambia Mahakama kuwa mshtakiwa amepatikana na kosa la kifungu cha sheria Namba 158 (1) (a ) SURA YA 16 ya marejeo 2002, hivyo Mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela kuanzia leo Novemba 1, 2019.
0 comments:
Post a Comment