Rais Magufuli amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii na waache kulalamika kwamba hawana fedha wakati hawajitumi.
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Novemba 27, katika eneo la Shelui wilayani Igunga mkoani Tabora akiwa njiani kuelekea Shinyanga baada ya mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Abel Mbinga kumlalamikia maisha magumu.
“Rais unafanya kazi nzuri sana, lakini fedha hakuna mheshimiwa, watu wana hali mbaya, akina mama wananyang’anywa TV, friji kwa ajili ya mikopo midogomidogo, tunaomba uachie fedha, mtaani, hali ngumu, mengine yote hatuna shida na wewe, yakikamilika haya hata ukitawala milele,” amesema Abel.
Majibu ya Rais Magufli: “Usipofanya kazi hela zitaisha tu, ukitaka hela fanya kazi, wapo watu wanalima sasa hivi, baadaye watapata pesa, wewe umekaa kijiweni unataka pesa ikukute hapo? Labda ukaoe mwanamke mwenye pesa. Cha bure hakipo, hata mimi sina, kinachotakiwa ni kuchapa kazi, maandiko yanasema asiyetaka kazi na asile.
“Kalime viazi au matikiti, ukiyaweka hapa barabarani yataliwa tu, ukitaka vya bure hupati, nenda hata machimboni utapata kazi, unataka mkono wako uwe soft (laini)… pesa hakuna, mimi sikuja hapa kuleta hela, nimekuja kuwaambia Watanzania ukweli.
“Serikali inatafuta pesa kwa ajili ya kujenga hospitali, barabara, maji na miradi mingine ya maendeleo. Siwezi kutafuta pesa kwa ajili ya kukulisha wewe na mke wako, na ukikosa (pesa) na mke anakukimbia….. Hata Ulaya wanafanya kazi wasiwadanganye wapo wanaolala kwenye mashimo. Mimi nimekwenda Ulaya wapo wenye shida kuliko huku, bahati mbaya kwao kuna baridi. Ukitaka kutengeneza maisha yako chapa kazi,”
0 comments:
Post a Comment