Wafuasi
22 wa Kundi la ‘Blue Guard’ la Chama cha Wananchi (CUF) wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam
wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kukutwa na silaha za Jeshi
la Polisi.
Washitakiwa
hao ambao ni wakazi wa Zanzibar walifikishwa mahakamani hapo jana na
kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita mbele ya Hakimu
Mkazi, Godfrey Mwambapa.
Mwita
alidai, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kula njama,
kuingilia majukumu ya kipolisi kupitia genge la uhalifu pamoja na
kukutwa na silaha pamoja na zana za Jeshi la Polisi.
Akisoma
mashitaka, Wakili Mwita alidai, kati ya Septemba 20 na 25, mwaka huu
kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, kupitia kikundi cha Blue Guard,
washitakiwa na wenzao ambao hawakufikishwa mahakamani walikula njama za
kuajiri watu, wafanye kazi za kipolisi kinyume cha Sheria ya Makosa ya
Jinai.
Aliendelea
kudai kuwa, washitakiwa wakiwa wanachama wa kundi la Blue Guard
waliwaajiri watu kwa ajili ya kufanya kazi za Kipolisi kinyume na
sheria.
Wakili
Mwita alidai, Septemba 25, mwaka huu katika eneo la Mwananyamala, Dar
es Salaam, wakiwa na lengo la kutenda kosa, washitakiwa walikutwa wakiwa
na silaha kinyume cha sheria , ikiwemo visu vitano pamoja na mabomu ya
machozi 10 kwa ajili ya kuyatumia katika uvamizi.
Aidha,
inadaiwa siku hiyo hiyo, Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wakiwa na
zana za Jeshi la Polisi ambazo ni mabomu ya machozi yanayotumiwa na
jeshi hilo katika majukumu yao.
Baada
ya kusomewa mashitaka washitakiwa hao walikana kutenda makosa hayo,
hata hivyo Wakili Mwita alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika
na kuomba wapangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Upande
wa utetezi kupitia Wakili Hekima Mwesigwa uliiomba Mahakama kuliondoa
shitaka la tatu katika makosa hayo kwa sababu lina upungufu wa kisheria
kwa kutumia baadhi ya maneno kupotosha.
Hata
hivyo, Wakili Mwita aliiomba Mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa
kuwa shitaka hilo halina upungufu wowote badala yake wametumia lugha ya
mkato.
Hakimu
Mwambapa alisema baada ya kupitia vifungu vya sheria, amebaini kuwa
shitaka halina mapungufu kisheria hivyo ametupilia mbali maombi.
Aidha,
alisema washtakiwa hao watapata dhamana endapo watatimiza masharti ya
kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hati ya Sh milioni
mbili kila mmoja, pia wawasilishe vitambulisho vyao mahakamani. Kesi
itatajwa tena Oktoba 20 mwaka huu.
Washtakiwa
ni Hamis Omary Said (49), Said Mohamed Zaharan (57), Hamid Nassor Hemed
(44), Nassor humud Ally (25), Othman Humud Abdlaah (34), Swalehe Ally
Swalehe (30), Hamis Hamis Haji (46), Majid Hamis Juma (58), Mohamed
Hamis Ally (34), Ramadhan Rashid Juma (30), Juma Hamad Seif (21) na
Masoud Iliyasa Fumu (29).
Wengine
ni Jecha Faki Juma (40), Mbaruku Hamis Bakari (31, Mohamed Alli Zuberi
(43), Muhsin Ally Juma (27), Mohamed Amir Mohamed (30), Ally Juma Salum
(35), Juma Hajji Mmanga (26), Ally Nassoro Ally (46), Haji Rashid Juma
(32) na Juma Omary Hamis (28).
Kufikishwa
mahakamani kwa washtakiwa hao kunatokana na mgogoro unaoendelea ndani
ya chama hicho. Septemba 28, mwaka huu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Simon Sirro alitoa taarifa za kukamatwa kwa wafuasi
hao kwa tuhuma za kupanga njama za kufanya fujo na kuchoma ofisi za CUF
zilizopo Buguruni Ilala jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment