Friday, 2 April 2021

VIJANA WA KIUME WADAI UCHUMI WA NG’OMBE UNACHOCHEA NDOA UTOTONI

...

 

Picha ya ng'ombe

Na Deogratius Temba, Kahama

Vijana wameaswa kutafuta vyanzo mbadala vya uwekezaji ili kujukwamua kimaisha badala ya kutegemea kuwaoza wasichana wa shule ili wapate mahari ya ng’ombe. 

Wakizugungumza katika mdahalo wa wanaume  juu kubadili mtazamo na mila na desturi zinazochangia Ukatili wa Kijinsia, katika kata za Shilela na Lunguya , Halmashauri ya wilaya ya Msalala, ulioendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Msalala na Shirika la Kimataifa la  Idadi ya watu (UNFPA),  wanaume kutoka katika vikundi mbalimbali zaidi ya 300 waliokutana katika mdahalo huo, wamesema jamii inahitaji mabadiliko makubwa ya kimtazamo ili kuondokana dhana ya uchumi wa ng’ombe na kuwekeza katika sekta nyingine za uzalishaji mali.

Akizungumza mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, aliwaasa vijana kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana, kujifunza ujasiriamali na kuchukua mikopo ya uwezeshaji vijana ya asilimia nne (4) inayotolewa na Halmashauri ili kuwa na vyanzo vyao wenyewe vya mapato badala ya kutegemea ng’ombe wa wazazi kulipia mahari pindi wanapotaka kuoa.

Katika mjadala huo, vijana walidai kuwa wakati mwingine, wasichana wadogo wanasukumwa kuolewa ili mahari yatakayopatikana yasaidie kumlipia kaka yake mahari kutokana na vijana wa kiume kutokuwa na fedha au kutokumiliki ng’ombe wa kutosha kulipa mahari.

“Unajua hapa kwetu, kama kuna msichana nyumbani, sisi vijana wa kiume tunaomba ajitokeze mtu wa kumlipia mahari ili sehemu ya ng’ombe wake tupewe nasisi tukalipe mahari… sasa kama kijana huna kazi, ajira huna, unategemea utapata wapi mahari?” alisema Fautine Shau (32) mkazi wa kata ya Lunguya.

Kwa upande wake Mtendaji wa kata ya Lunguya, Lusajo Manase, aliwaasa vijana kuhakikisha wanasimama imara katika kubalidili mtazamo, kuacha kurithi mila na desturi ambazo zinasababusha vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.

“Tunayo bahati ya kipekee kukutana na nyie vijana wa kiume wa kata yetu. Hawa wenzetu wamekuja ili tubadilishane mawazo, tuboreshe mahusiano yetu ili tukitoka hapa tuwe na mkakati unaotekelezeka wa kutokomeza kabisa Ukatili wa Kijinsia”, alisema Lusajo.

Shabaha za kiutendaji kwa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia (MTAKUWWA), ni Kuongeza uwiano wa halmashauri zenye programu za  kijamii za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake kutoka asilimia 0 hadi asilimia 20,  Kuongeza uwiano wa wanakaya wenye umri kati ya miaka 15-49 waliopata taarifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake,  kutoka asilimia 0 hadi asilimia 55 (iv) Kupunguza ukatili wa kingono kutoka asilimia 17.2 hadi asilimia 8.

Aidha ni  kupunguza ukatili wa kimwili dhidi ya wanawake wenye umri kati ya miaka15-49 toka asilimia 39 hadi asilimia 10 na  kupunguza ukatili wa kihisia kutoka asilimia 36.3 hadi asilimia 18. 

 Sambamba na kupunguza ukatili dhidi ya Watoto unaosababishwa na mila na desturi  kama mimba za utotoni kutoka asilimia 27 hadi asilimia 5, Kupunguza kiwango  cha ukeketaji kutoka asilimia 32 hadi asilimia 11 na  Kupunguza ndoa za utotoni kutoka asilimia 47 hadi asilimia 10. 


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger