Friday, 30 April 2021

MANISPAA YA SHINYANGA KUANZISHA MASHINDANO YA USAFI WA MAZINGIRA

...

 

Mkuu wa idara ya Usafi na Mazingira Manispaa ya Shinyanga Kuchibanda Snatus, akisoma taarifa ya mpango wa kuanzisha mashindano ya usafi wa mazingira kwenye Baraza la Madiwani kwa niaba ya Mkurugenzi. Picha zote na Marco Maduhu
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akizungumza kwenye Baraza la Madiwani.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila, akizungumza kwenye Baraza la Madiwani.

***
Na Marco Maduhu, Shinyanga.
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, inatarajia kuanzisha mashindano ya usafi wa mazingira, kwa ajili ya kuuweka mji huo katika hali ya usafi, pamoja na kupambana na magonjwa yatokanayo na uchafu kikiwemo kipindupindu.

Akisoma taarifa ya mpango huo leo wa kuanzisha mashindano ya usafi wa mazingira, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga, Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira Manispaa hiyo Kuchibanda Snatus, kwa niaba ya Mkurugenzi, alisema lengo la mashindano hayo ni kuhakikisha mji unakuwa safi muda wote.

Alisema mashindano hayo yatajumuisha kata zote 17 za Manispaa ya Shinyanga, Mitaa 55, vijiji 17, Taasisi zote za umma, na binafsi, zikiwamo Shule za Msingi na Sekondari, Masoko, viwanda, ambayo yanatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

“Maeneo yatakayokaguliwa kwenye mashindano hayo ni usafi wa Kaya, Shule, Masoko, Mitaro, Barabara, Viwanda, na Maeneo ya wazi na utekelezaji utasimamiwa na viongozi wa Serikali za vijiji, mitaa na Kata, kwa kufanya ukaguzi wa usafi wa mazingira kwenye maeneo yote,”alisema Snatus.

“Mshindi wa mashindano haya ngazi ya Kaya na Shule atapewa zawadi ya vifaa vya usafi, Kiwanda na Kata itakayo ongoza watapewa Ngao, Mtaa utapewa Cheti, na watakaofanya vibaya watapewa Kinyago,”aliongeza.

Aidha alisema faida za mashindano hayo ni kuboresha hali ya usafi wa mazingira kwenye maeneo mbalimbali ya Manispaa, kupunguza madharia ya Mbu, pamoja na kutokomeza magonjwa ya kuhara na kipindupindu.

Naye Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Nkulila, alisema mpango huo ni mzuri na utasaidia kuondoa kero za uchafu mjini Shinyanga, ambapo mji utakuwa msafi pamoja na kuzolewa uchafu wa kwenye Maghuba kwa wakati, huku akitoa wito kwa madiwani wakatoe elimu ya usafi kwa wananchi.

Nao Madiwani wa Manispaa hiyo ya Shinyanga, walipongeza mpango huo wa mashindano ya usafi wa mazingira kuwa utaleta hamasa kubwa ya kuufanya mji huo kuwa msafi huku kila mmoja akijingamba kupata ushindi.

Pia Baraza hilo la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, limefanya kikao cha siku mbili kujadili ajenda mbalimbali, kwa ajili ya mstakabali wa maendeleo ya Manispaa hiyo.

Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza.
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza
Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza

Na Marco Maduhu- Shinyanga.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger