Thursday, 29 April 2021

TAKUKURU MARA YAOKOA MIL. 689 BAADA YA KUDHIBITI MIANYA YA RUSHWA

...

 

Na Dinna Maningo,Musoma

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) mkoani Mara imefuatilia na kudhibiti mianya ya rushwa na kuokoa sh Milioni 689,317,212.00 wakati wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh.Bilioni 8.188 katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi,2021.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Mkuu wa Takukuru mkoa wa Mara Hassan Mossi alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kilikuwa kifanyiwe ubadhilifu na kingelipwa kwa wakandarasi na wazabuni mbalimbali ambao walikuwa wakitekeleza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya majengo na barabara kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na.11 ya mwaka 2007.

Mossi alisema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2021 TAKUKURU mkoani humo imefanya uchunguzi wa malalamiko yanayohusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kadhaa iliyotekelezwa kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani yenye jumla ya sh. 891,288,244.00.

"Tulifanya uchunguzi dhidi ya mkopeshaji mmoja aliyemkopesha fedha mama ambaye kwa sasa ni marehemu aliyekuwa akimiliki nyumba, baada ya mkopeshaji kusikia mama mmiliki wa nyumba kufariki, alitengeneza nyaraka kuonyesha kuwa walifanya mauziano,mpaka sasa mkopeshaji huyo anamiliki nyumba hiyo ya marehemu kwa kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kinyume na sheria,tunaendelea na uchunguzi ukikamilika taratibu za kumfikisha mahakamani zitafanyika",alisema Mossi. 

Alisema kuwa ofisi hiyo imesaidia Kanisa la Mennonite Serengeti kuokoa sh milioni tatu fedha ambazo zilitokana na mauzo ya gari aina ya Toyota Cruiser yaliyofanyika kinyemela na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo.

Aliongeza kuwa TAKUKURU imefanya uchunguzi wa makusanyo ya mapato yanayofanyika kwa kwa kutumia mashine ya POS na kubaini mianya ya rushwa iliyosababisha ubadhilifu wa sh.milioni 220,000,000 kinyume na sheria,ubadhilifu uliofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Serengeti.

"Baada ya kuanza uchunguzi watuhumiwa tayali wamerejesha fedha sh. milioni 13,00,000 ikiwa ni miongoni mwa makusanyo ambayo yalikuwa hayafiki kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo. 

Alisema kuwa ofisi inaendelea na uchunguzi wa mkopeshaji mwingine ambaye alimkopesha mwalimu mstaafu sh. 1,400,000,baada ya mafao yake kutoka alichukua kiasi cha sh.66,000,000 na tayari mkopeshaji amerejesha sh.30,000,000 baada ya TAKUKURU kuingilia kati na bado anatakiwa kumrudishia mstaafu huyo shilingi 34,600,000.

"Mwalimu mwingine alikuwa amechukuliwa fedha zake shilingi 20,000,000 na bwana mmoja aliyedai kuwa amemsaidia mwalimu huyo kulipwa mafao yake haraka lakini kwa uhalisia hakuna kazi aliyoifanya,baada ya uchunguzi alimrejeshea kiasi chote cha fedha", alisema Mossi. 

Alisema kuwa ofisi hiyo imeokoa fedha milioni 1.474,800 ambazo ni fedha za NSSF ambazo zilichukuliwa na wananchama wa MUSOMA SACCOS walizokopeshwa, nakwamba TAKUKURU imepokea malalamiko 189 yanayohusu vitendo vya rushwa ikilinganishwa na malalamiko ya mwezi Octoba -Desemba, 2020.

"Tumefanikiwa kushinda kesi nne na kufungua kesi tatu mpya na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, tuna program ya TAKUKURU inayotembea na imeweza kufika katika kijiji cha Bwitego,na Nyinchoka wilayani Serengeti nakuzungumza na wananchi na kutatua migogoro katika vijiji hivyo", alisema Mossi.

Aliongeza kuwa TAKUKURU ina mikakati katika kipindi cha mwezi Aprili -Juni,2021 kuhakikisha inazuia rushwa na kudhibiti mianya ya rushwa kwenye miradi ya maendeleo pamoja na uelimishaji umma juu ya madhara ya rushwa katika jamii na kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani hivyo alitoa rai kwa watumishi wa umma na wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger