Friday, 22 March 2019

Waziri Mkuu Azindua Kiwanda Cha Kuchakata Muhogo......Awataka wakulima kuchangamkia fursa kwa kulima kwa wingi

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi katika mikoa ya Lindi na Mtwara watumie fursa ya uwepo wa kiwanda cha kuchakata muhogo katika kijiji cha Mbalala, kata ya Nyengedi mkoani Lindi kwa kulima zao hilo kwa wingi ili waweze kujiongezea kipato.

“Kama unataka pesa nenda kalime muhogo kwani kuna soko la uhakika na pia zao hili ni la muda mfupi na kilimo chake ni rahisi. Kwa sasa hatuna muda wa kukaa vijiweni vijana jiungeni katika makundi na muanzishe mashamba ya mihogo soko lipo tena mwenye kiwanda atawafuata hukohuko shambani.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 22, 2019) wakati akifungua kiwanda cha kuchakata muhogo cha Kampuni ya Cassava Starch of Tanzania Corporation Limited (CSTC) kilichopo katika kijiji cha Mbalala, kata ya Nyengedi mkoani Lindi.

Amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli la kuhamasisha ujenzi wa viwanda ni kusaidia katika kuongeza thamani ya mazao mbalimbali yanayolimwa na wakulima nchini kabla ya kuuzwa.” Mbali na kuongeza tija kwa wakulima pia viwanda vinatoa ajira nyingi”.

Kadhalika, Waziri Mkuu amekipongeza kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara kwa kazi nzuri ya utafiti wa mbegu za mazao mbalimbali wanayoifanya. Amesema kituo hicho ndicho kilichotafiti mbegu bora za muhogo zenye uwezo wa kuzalisha tani 20 hadi 50 kwa hekta.

Kwa upande wake, Balozi wa ufaransa nchini, Balozi Frederic Clavier amesema Serikali ya Ufaransa ipo tayari kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli katika mkakati wake wa kukuza uchumi hadi kufikia uchumi wa kati kwa kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025.

Amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni ushuhuda tosha wa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa na kilimo ni miongoni mwa mikakati ya kuinua uchumi wa Tanzania.

Nae, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewashukuru wawekezaji hao kwa uamuzi wao wa kujenga kiwanda cha kuchakata muhogo nchini kwa kuwa wamewezesha wakulima wa zao hilo kupata soko la uhakika na vijana wengi kupata ajira.

Kwa upande wake,Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa msukumo alioutoa wa kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini kwa kuwa umechangia kuboresha maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali.

Mbunge huyo amesema uwekezaji katika sekta ya viwanda umesaidia kupunguza changamoto ya ajira hususani kwa vijana. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa juhudi zake, kwani hatukutarajia kuwa na kiwanda katika eneo hili”.

Awali,Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CSTC, Christophe Gallean alisema kiwanda hicho ambacho kilianza kujengwa mwaka 2012 kinazalisha unga wa muhogo wenye kiwango cha juu cha ubora na kinauza unga huo katika nchi za Afrika Mashariki, Kusini, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani.

Alisema kiwanda hicho chenye wafanyakazi zaidi ya 420 ambapo Watanzania ni asilimia 97 kina uwezo wa kuchakata tani 60 za muhogo mbichi kwa siku, ambao ni sawa na tani 25 za unga bora wa muhogo kwa siku.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger