Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Kondoa, mkoani hapa imewafikisha mahakamani mafundi umeme, Ally Manyundo na Ibrahim Seleman kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh 100,000.
Kati ya fedha hizo tayari walipokea Sh 60,000 ili waweke nguzo za umeme karibu na nyumba ya mtoa taarifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo, Manyundo ni fundi umeme na mwajiriwa wa Kampuni ya MF Electrical Engineering Company Limited na Selemani ni kibarua kwenye kampuni hiyo.
Akiwasomea mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kondoa, Lucas Jang’andu baada ya kufunguliwa kesi ya jinai Namba 56/2019, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Haule aliiambia mahakama hiyo kuwa washtakiwa wametenda kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na Kifungu cha 15 (1) (a) na (2) ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007.
Mwendesha Mashitaka huyo alidai kuwa washtakiwa hao kati ya Machi 8 na Machi 10 mwaka huu, wakiwa katika Kijiji cha Kiteo Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma waliomba Sh 100,000 na kupokea kiasi cha Sh 60,000 kama rushwa kwa ajili ya kuweka nguzo ya umeme karibu na nyumba ya mtoa taarifa.
Alisema washtakiwa hawakukidhi masharti ya dhamana, hivyo walipelekwa rumande hadi Machi 22 mwaka huu kesi hiyo itakaposikilizwa.
0 comments:
Post a Comment