Dar Es Salaam,Tanzania.
MWAMUZI Martin Saanya aliyechezesha mechi ya watani wa
jadi, Simba na Yanga Oktoba 1, mwaka huu amefungiwa miaka miwili kwa
pamoja na Msaidizi wake, namba moja, Samuel Mpenzu.
Habari za ndani kutoka Bodi ya Ligi ya Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF),zimesema kwamba maamuzi hayo yamefikiwa leo katika
kikao cha Kamati ya Masaa 72 ya shirikisho hilo.
Na pamoja na kuwafungia waamuzi huo kwa makosa ya kutoa
maamuzi ya utata, pia Kamati imefuta Kadi nyekundu ya mchezaji Jonas
Mkude baada ya kubaini hakufanya kosa.
Maamuzi ya utata ya Saanya yalisababisha vurugu Uwanja
wa Taifa Jumamosi baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na
mshambuliaji Mrundi,Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania bara.
Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi
ndefu ya beki Mbuy Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba,
Novaty Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
Bao hilo lilizua kizaazaa,wachezaji wa Simba wakimvaa
refa Martin Saanya wakidai mfungaji,Tambwe aliushika mpira kabla ya
kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha
wa Simba SC Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari
wa mbele.
Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika
tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na
kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi
kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba
SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
Na Mpenzu naye anadaiwa kukataa bao safi la Simba lililofungwa na Ibrahim Hajib mapema kipindi cha kwanza akidai aliotea.
Pamoja na hayo, Simba na Yanga zote zimeadhibiwa kwa
kutozwa faini na kutakiwa kufidia gharama za uharibifu mbalimbali ambao
mashabiki wake walifanya uwanjani.
0 comments:
Post a Comment