WITO umetolewa kwa wananchi kuongeza uelewa na utayari kabla na baada ya majanga huku wakijua namna ya kujikinga nayo ikiwemo mafuriko kwa kupunguza au kuondokana na athari za kijamii na kiuchumi.
Wito huo umetolewa jana na Mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka Asasi ya kitaifa inayohusika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi (ForumCC Tanzania) Rebecca Muna wakati akizungumza na waathirika wa mafuriko wa kata za Lukobe na Kihonda Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuwapatia elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya mafuriko na hatua za kuchukua.
“Mabadiliko ya tabia nchi ni athari moja iliyoleta athari nyingine ya mvua za Elnino na hatimaye mafuriko katika maeneo ya Manispaa ya Morogoro na maeneo mengine ya nchi na dunia kwa ujumla, mafuriko yametokea zaidi ya mara moja na kusababisha hasara kubwa ya kuharibika kwa mali sambamba na vifo”,alisema Muna.
Muna aliongeza kuwa, moja ya njia ya kujikinga na majanga ya mafuriko ni wananchi kusikiliza na kuzichukulia hatua taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini ikiwemo mvua kubwa, upepo na vimbunga.
Alisema kwa kushirikiana na ActionAid, Plan International, CAN Tanzania kwa ufadhili Start Fund wameweza kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo mablanketi na vyakula na kuwaondoa kwenye maeneo yaliyoathirika hasa kwa waathirika wa maeneo mengine ya manispaa ya Morogoro, Malinyi, Ifakara, Lindi na Rufiji.
Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro Winfred Kipako aliwataka wananchi waliokumbwa na mafuriko kwenye maeneo hayo kuwa watulivu wakati serikali ikijipanga kujenga mitaro itakayotoa maji kwenye njia za reli ya SGR na kuyapeleka kwenye mto Ngerengere ili mafuriko yasijirudie tena kwenye maeneo yao.
0 comments:
Post a Comment