Jamaa mmoja amenusurika kifo kwa tundu la sindano baada ya mti kuangukia choo cha rununu alimokuwa akijisaidia.
Jamaa huyo alikwama ndani ya choo cha rununu siku ya Ijumaa, Aprili 30,2021 baada ya kuangukiwa na mti.
Mwanamume huyo alikuwa anajisaidia kwenye choo hicho kilichoko katika Hifadhi ya Gettysburg wakati upepo mkali uliangusha mti na kumuwacha na majeraha madogo.
Maafisa wa usalama eneo hilo walisema tukio hilo lilisababishwa na upepo mkali, kama ilivyoripoti vyombo vya habari vya Marekani Jumamosi, Mei 1,2021.
Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa jamaa huyo alinusuriwa mwendo wa saa kumi jioni na Idara ya Wazima Moto ya Barlow.
Chifu msaidizi Joe Robinson alisema kuwa walipata mti umeangukia gari lakini hakuna yeyote aliyekuwa ndani.
Kisha baadaye maafisa waligundua kulikuwa na mtu aliyekwama ndani ya choo na kuanza shughuli ya uokoaji.
“Alikuwa na bahati. Ulikuwa mti mkubwa, na ulikwepa kumgonga. Ingelikuwa mbaya zaidi,” alisema Robinson ambaye amekuwa mzima moto wa kujitolea kwa miongo mitatu.
Robinson alisema jamaa huyo aliokolewa kwa kukata mti huo wakitumia msumeno na kisha kukata sehemu ya choo hicho.
Maafisa hao walimuweka ndani ya ambulensi na kumpeleka katika Hospitali ya Gettysburg kwa sababu ya kupata majeraha madogo.
Wahudumu wa masuala ya dharura walipokea simu nyingi ya miti kuangushwa na upepo, nyaya na moto.
0 comments:
Post a Comment