Sunday, 30 May 2021

ASKARI WA UHAMIAJI WALIOMTESA ALEX WAKIDAI NI TAPELI WASIMAMISHWA KAZI

...

Kamishina Jenerali wa Uhamiaji Dkt.  Anna Makakala
***
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Uhamiaji imewasimamisha kazi wafanyakazi wake watatu kutokana na tukio la askari wa Uhamiaji kutumia nguvu dhidi ya Alex Raphael Kyai kama video fupi ilivyoonekana katika mitandao ya kijamii.
Video hiyo inayosambaa mtandaoni inamuonesha Alex akipewa mateso mbalimbali ikiwemo kulowanishwa maji kwa kutumia bomba la maji huku akiwa amelala kwenye maji, kuruka kichura pamoja na kugaragara kwenye mchanga.

Akizungumza na wandishi wa habari leo Mei 30, 2021 Kamishina Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala amesema Mei 27 mwaka 2021, Idara ya Uhamiaji ilimkamata mtuhumiwa wa utapeli anayefahamika kwa jina Alex Raphael Kyai katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini, Dar es salaam ambaye aliongozana na mteja wa huduma za pasipoti, aliyemtambulisha kama mkewe.

Aidha Dkt. Makakala amesema baada ya mahojiano, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kuwalaghai na kupokea fedha kutoka kwa wateja mbalimbali ili waweze kupata pasipoti kwa haraka, pia mtuhumiwa huyo amekuwa akijitambulisha kama Mtumishi wa Taasisi nyeti ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

" Idara ya Uhamiaji inakiri kutokea kwa tukio hilo na pia inalaani kitendo kilichofanywa na askari wa Uhamiaji kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao, hata hivyo Idara ya Uhamiaji tayari imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari hao" ,Dkt.Makakala.

Idara ya uhamiaji inatoa wito kwa wananchi wote wanaohitaji huduma za kiuhamiaji kufika wenyewe katika ofisi za Uhamiaji, pia Uhamiaji wanawahakikishia kwamba idara itaendelea kutoa huduma zake kwa weled, uwazi na bila kutumia mtu wa kati ( Vishoka) Na Idara hiyo ya Uhamiaji inaomba kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo.

Aidha Idara ya uhamiaji imetoa onyo kwa yeyote ambaye atajaribu kujifanya kuwa Afisa wa Uhamiaji au Afisa wa Serikali ili kumsaidia mtu mwingine kwa maslahi yake binafsi hatua kali dhidi yake zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria.

 Chanzo - Michuzi Blog

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger