Thursday, 27 May 2021

“Kujikosoa Ni Kujisahihisha” Bashungwa

...


Na Judith Mhina Maelezo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, amesema kujikosoa ni kujisahihisha maneno aliyoyanukuu kutoka kwa muasisi wa Taifa la Tanzania Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Maneno hayo ameyatamka wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha 14 cha mwaka huu kwa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kilichofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia Mbeya (MUST) hivi karibuni.

Waziri Bashungwa amenukuu maneno hayo kutokana na hali halisi ya Maafisa Habari wa Serikali hapa nchini ambao wana wajibu wa kujikosoa na  kujirekebisha  katika kutimiza majukumu yao kama kaulimbiu ya Kikao Kazi hicho inavyosema, “Taarifa kwa Umma ni Takwa la Kisheria, Viongozi wa Umma na Maafisa Habari Tuwajibike.”

Aliongeza kuwa, ili kutimiza takwa hilo  wote kwa pamoja wana wajibu wa kuhakikisha  wanasimamia kama viongozi ili walengwa ambao ni Mafisa Habari wa Serikali  watangaze na kusemea kazi zote za Serikali ikiwemo miradi ya kimkakati, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“Tuna taarifa kuwa baadhi ya  Maafisa Habari walioko  katika utumishi wa Umma ni watu ambao hawataki kujituma na kuwa wabunifu  ingawa wanawezeshwa kwa kupewa vifaa vya kazi  na kushirikishwa ndani ya  menejimenti husika, pamoja na kushirikishwa katika  ziara zote  lakini hawatimizi wajibu wao.” alisema Waziri Bashungwa.

Aidha, katika dhana nzima ya kujikosoa na kujisahihisha kama alivyosema Mwalimu Nyerere, upo wajibu  wa kukitendea haki Kikao Kazi  hicho, ambacho ni cha siku tano kuanzia Mei 24-28, 2021 ili kuwa  chachu ya kuleta mageuzi makubwa katika kuhakikisha  Maafisa Habari wanaisemea na kuitangaza Serikali ili Umma wa Tanzania wajue kile ambacho Serikali yao  inafanya.

Katika suala zima la wajibu wa mwajiri, Maafisa Habari wengi wapo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma na Wizara. Kuna changamoto kadhaa zinazowakabili maafisa hao kama vile kuwa chini ya mtumishi wa Kitengo cha TEHAMA, au kuonekana kama mpiga picha tu wakati wa matukio mbalimbali na kutoshirikishwa katika maamuzi ya Menejimenti husika.

Amesema kuwa Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016 na kanuni zake za Mwaka 2017 pamoja na Sheria ya Haki ya kupata Taarifa Na. 06 ya mwaka 2016 ndivyo vinavyomfanya Afisa Habari kutambulika na kutimiza wajibu wake. Sheria hizi zinajenga taaluma ya Habari na kuifanya kutambulika rasmi.

Waziri Bashungwa amebainisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, zikiwepo za Maafisa Habari kuchanganywa na Watumishi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao wakati mwingine huweza kukorofisha mawasiliano ya kimtandao na hivyo kukwamisha kazi za maafisa habari.

Kuhusu suala la kutokuwa na vitendea kazi pamoja na kupewa majukumu ambayo si yao na kushirikishwa tu pale yanapotokea matukio Waziri Bashungwa alitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuangalia suala hilo na kuona umuhimu wa kuwashirikisha maafisa Habari katika vikao vya maamuzi  ili kuwa na uelewa mpana utakaowasaidia kutangaza na kusemea kazi nzuri zinazofanywa na Serikali.

Kuokana na changamoto mbalimbali zilizoainishwa na Waziri Bashungwa, Idara ya Habari (MAELEZO) ilipata fursa ya kufanya mahojiano na baadhi ya  Maafisa Habari Grace Gwemagobe wa Mkoa wa Songwe ambaye alisema “Maafisa Habari walio wengi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini wana changamoto ya utendaji wa kazi, kwa kuwa inategemea kiongozi anayemkuta katika sehemu husika ana utashi gani juu ya kada ya Afisa Habari. Aidha, mara nyingi inakuwa  kama ni hisani, au  kujuana na kiongozi wako badala ya kusimama kwenye mfumo halisi ulivyo wa kiutumishi  au kulingana na taratibu za kusimamia utumishi wa umma.

Gwemagobe  ameongeza kuwa yeye yupo chini ya  Idara ya Utawala na Rasilimali watu  ambapo kiongozi wake ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu, na Maafisa Habari wengi hawajui  miongozo ya uendeshaji  (PMG)  katika Sekretarieti ya Mkoa. Hatua hiyo inasababisha Maafisa Habari wengi wa Mkoa kuishia kuwa Katibu  wa  Wakuu wa Mikoa  badala ya kufanya kazi za Afisa Habari kama ilivyoelekezwa  katika taratibu za utumishi wa umma.

Naye Afisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Mufindi Ndimiyake Mwakapiso amesema “ Ofisi za Serikali ni za umma  kwa hiyo  kama Mkuu wa Kitengo au idara ni Afisa Habari au  Mtumishi wa TEHAMA haina tatizo lolote kwani tunafanya kazi kwa kushirikiana  na  mambo yanaenda tu”.

Mwakapiso pia ameongeza kuwa  kuna baadhi ya Halmashauri Maafisa Habari ndio wakuu  wa vitengo na wanawasimamia watumishi wa TEHAMA, kwa nia njema tu na kusisitiza kuwa wanafanya bila tatizo lolote.

Naye Afisa Habari ambaye hakutaka jina lake litajwa amesema “Mimi binafsi katika ofisi yangu sina vitendea kazi wala hakuna kitengo cha habari tunawekwa mahala popote kiongozi wetu anapodhani tunaweza kuwa hapo. Pia  hatuna bajeti ya kitengo, vilevile mara nyingi wakuu wa idara wenye miradi mbalimbali hawatushirikishi kwa kuhofia tukienda kwenye miradi tutadai kulipwa fedha na wao hawako tayari kulipa posho ya Afisa Habari badala ya yeye na wahusika katika ofisi yake”.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger