Tuesday 30 March 2021

Wataalamu wa mazingira wasio waaminifu kudhibitiwa

...


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imepitisha kanuni itakayowadhibiti washauri wa mazingira ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wawekezaji.

Ummy amesema wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma  Machi 28, 2021.

Alisema baadhi ya wataalamu hao kutokuwa waaminifu na kuwatoza kiwango kikubwa cha fedha watu wanaotaka kuwekeza hususan katika viwanda na kukwamisha maenndeleo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti lipo tatizo kwa hawa environmental experts (wataalamu wa mazingira) sasa tumepitisha kanuni kama ambavyo wanafanya wafamasia, manesi, madaktari ambayo itasaidia kuwa na viwango na tutakuwa, wataalamu hao watapaswa kujisaili upya,” alisema.

Alisema Serikali inawalinda wawekezaji na kuwa kamwe haiwezi kuwa kikwazo kwao na kuwa suala la kulinda mazingira pia linachukua nafasi yake katika viwanda vinavyojengwa.

Aidha Waziri Ummy alibainisha kuwa Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 katika migodi na viwanda kwa kufanya ukaguzi katika maeneo hayo.

Aliongeza kuwa elimu itaendelea kutolewa kwa wenye viwanda hapa nchini kuhusu kuweka mifumo ya kutibu majitaka kabla ya kuyatiririsha katika mazingira hali inayoweza kuhatarisha afya za wananchi.

Katika hatua nyingine alisema kuwa Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango-kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini.

“Tutaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala wa zebaki na pia Ofisi kwa kushirikiana na Mamlaka husika itaimarisha usimamizi wa uingizaji wa zebaki nchini. Pia tutashirikiana na Mamlaka husika kuandaa Mkakati wa udhibiti wa athari za zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa kuandaa Mkakati wa Nishati Mbadala ya Kuni na Mkaa kwa ajili ya kupikia.

“Tutaomba mamlaka husika ziondoe tozo kwenye mashine za kutengenezea mkaa mbadala kama ilivyo sola na pia kuomba gesi iuzwe kwa rejareja ili wananchi waweze kumudu,” alisema.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger