Monday, 29 March 2021

Serikali Kuendelea Kuzipatia Ufumbuzi Changamoto Za Muungano

...


 Na Lulu Mussa
Serikali itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano kadiri zinavyojitokeza na kuhakikisha Hoja za Muungazo ambazo zimepatiwa ufumbuzi maazimio na makubaliano yake yanatekelezwa na pande zote mbili za Muungano.

Hayo yemesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kuwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Amesema kupitia vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya uenyekiti wa Mhe. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jumla ya hoja 25 zilisajiliwa na kati ya hizo hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi, 10 ziko katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

“Mhe. Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, changamoto za Muungano haziwezi kuisha azma ya Serikali zetu mbili ni kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi mapema kwa mustakabali endelevu wa Muungano wetu” Mhe. Ummy alisisitiza.

Waziri Ummy ameyataja mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 kuwa ni pamoja na Kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambapo kikao cha kusaini Hati Tano (5) za Makubaliano ya kuondoa kwenye orodha ya hoja za Muungano hoja zilizopatiwa ufumbuzi kilichofanyika tarehe tarehe 17 Oktoba, 2020 Jijini Dar es Salaam.

Aidha, katika kuratibu Masuala ya Kiuchumi na Kijamii  jumla ya Taasisi kumi na mbili (12) zilitembelewa Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Muungano na Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa pande mbili za Muungano; Kuratibu masuala yasiyo ya Muungano ili kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Vikao saba (7) vya Ushirikiano vilifanyika.

Amesema katika mwaka ujao wa fedha Ofisi yake itaweka mkazo katika kutatua changamoto za Muungano hususan masuala ya fedha, kuimarisha ushirikiano kwa taasisi zisizo za Muungano zenye sekta zinazoshabihiana na kutolea mfano sekta za Afya, Elimu na Mawasiliano.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kushirikiana katika kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo hufadhiliwa na Washirika wa Maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa pande mbili za Muungano. Miradi ambayo imewasaidia wananchi wa pande zote mbili za Muungano kushiriki na kuinua hali zao za kiuchumi pamoja na kuongeza ajira kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria Mhe. Mohammed Mchengerwa ameishauri Serikali kuendelea kutoa elimu hususan kwa vijana waliozaliwa baada ya Muungano ikiwa ni pamoja na kuelezea fursa na faida za Muungano.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger