Saturday 28 December 2019

Zingatieni mfumo wa rufaa wa huduma za afya nchini – Waziri Ummy

...
Watanzania hususan wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wametakiwa kuhakikisha wanazingatia na kufuata mfumo wa rufaa wa utoaji huduma za afya nchini uliowekwa na Serikali.

Rai hiyo imetolewa  na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala.

Akiwa hospitalini hapo, Waziri Ummy alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliowasindikiza ndugu zao kwenda kujifungua, kwamba wanalazimishwa kulipia gharama ingawa Sera ya Serikali inaeleza huduma ya kujifungua ni bila malipo.

Hata hivyo, ilibainika kwamba idadi kubwa ya wajawazito wanaofika hospitalini hapo kujifungua hawafuati mfumo wa rufaa badala yake huenda wenyewe hospitalini hapo.
 
Kutokana na hali hiyo, wananchi hutakiwa kuchangia huduma ingawa wengi wao walilalamika kwamba hawapewi maelezo ya kina hasa kuhusu huduma ya kujifungua kwa haraka (fast track) iliyoanzishwa hospitalini hapo.

“Kwa kutokufuata rufaa ndiyo maana kunakuwa na mrundikano wa wagonjwa. Taarifa za madaktari zinaeleza wajawazito 85 kati ya 100 wanaweza kujifungua bila changamoto yoyote na wanaweza hata kuzalishwa na wakungwa wa ngazi ya cheti au diploma.

“Ni asilimia 15 hupata changamoto za uzazi na hao ndiyo wanaopaswa kupewa rufaa kwa mfano waje huku Mwananyamala,” amesema Waziri Ummy.

Ameongeza “Hivyo, nimewaeleza wazi uongozi kwa hawa wanaokuja bila rufaa wasione aibu kuwapiga penati, lakini wale wanaokuja kwa kufuata mfumo wa rufaa wapewe huduma bila malipo inavyostahili.

Sambamba na hilo, ameuagiza uongozi huo kuhakikisha unaweka uwiano sawa wa madaktari katika upande wa huduma hiyo ya fast track waliyoainzisha na isiwe kichocheo au kisababishi cha watu kukosa huduma.

“Hii itawezesha hospitali kujiendesha ili itoe huduma bora, wameweka kiasi cha Sh. 75,000 badala ya Sh. mil 1.5 ambazo wanalipia kule hospitali binafsi, muhimu kutoa maelezo sahihi kwa wananchi,” amesema.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu amesema walianzisha huduma hiyo ya fast track ili kuwezesha wananchi wenye kipato cha chini wanaohitaji huduma ya haraka kujifungua nao waweze kuimudu.

“Watu wanakuja hapa Mwananyamala kwa sababu ya huduma zetu ni bora, zaidi ya asilimia 90 tunaowahudumia ni wanawake na watoto na asilimia 15 pekee huhitaji huduma ya dharura kujifungua.

“Hapa tuna madaktari bingwa 22, tulianzisha huduma hii ili hawa mabingwa waweze kutoa huduma hapa hapa badala ya kwenda kule hospitali binafsi, lakini hakuna mwananchi ambaye hatukumpa huduma na kumlazimisha alipie kwanza gharama,” amesema.

Ameongeza “Hatulazimishi mwananchi kulipia huduma, tunatoa huduma kwa wote, lakini ukichagua kuja Mwananyamala badala ya sisi kukurudisha tunakuambia kuna njia mbili, upate huduma kwa ‘fast track’ au ufuate mfumo wa rufaa.

MWISHO


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger