Sunday, 29 December 2019

Waziri Mkuu Atoa Agizo Zito Kwa Wakuu Wa Mikoa kote Nchini

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati ili wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kusoma kwa pamoja kwa sababu wakipishana muda wa kuanza masomo baadhi yao wanashindwa kufanya vizuri jambo ambalo si sahihi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Desemba 29, 2019) wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020 kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Ruangwa.

Jumla ya watahiniwa  933,369  sawa  na  asilimia  98.55 ya  waliosajiliwa  walifanya  mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 na kati yao watahiniwa  759,737  wamefaulu ambao ni sawa na asilimia 81.50.

Kati  yao  wasichana  ni  395,738  ambao  ni  sawa  na  asilimia  80.87  na wavulana  ni  363,999  sawa  na  asilimia  82.20.  Mwaka  2018  watahiniwa waliofaulu  walikuwa  asilimia  77.72,  hivyo  kuna  ongezeko  la  ufaulu  kwa asilimia  3.78.

“Wakuu wa Mikoa hakikisheni vyumba vya madarasa vinakamilika ili wanafunzi wote waliofaulu waanze masomo kwa pamoja. Kitendo cha wanafunzi kupishana kuanza masomo kinawafanya waliochelewa kutofanya vizuri katika mitihani yao.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia vizuri elimu kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwakatisha masomo iwe kwa kuwaoa, kuwaozoesha au kuwapa ujauzito.

Amesema Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.

“Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa au kumpa ujauzito.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona idadi kubwa ya watoto wa kike wanatimiza malengo yao kielimu, hivyo ni lazima wakaondolewa vishawishi  kwa kuboresha mazingira yao ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mabweni.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo na wilaya ya Ruangwa ambayo imepewa sh. bilioni 38 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kubuni mradi wa kimkakati wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao na pembejeo linalojengwa katika kijiji cha Lipande. Ujenzi huo unaogharimu sh bilioni 5.45.

Ghala hilo ambalo limeanza kutumika lina uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 litaiwezesha halmashauri kujiongezea mapato ya ndani na kusaidia kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu na wafadhili. Pia litapunguza gharama za usafirishaji wa korosho walizokuwa wanatozwa wakulima wakati wa kusafirisha mazao.

Amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa nchini ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga, uboreshwaji wa viwanja vya ndege, ununuzi wa rada na ununuzi wa ndege mpya.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, kipaumbele chake kilikuwa ni kukuza kiwango cha uchumi kutoka cha chini kwenda cha kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, DESEMBA 29, 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger