Mbowe-Tumalize mjadala kwa maridhiano badala ya vijembe
Baada
ya mvutano mkali ndani ya Bunge Maalum la Katiba, Mwenyekiti wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe, ameshauri wajumbe kumaliza
mjadala kwa maridhiano badala ya kulumbana na kurushiana vijembe.
Mbowe
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, alitoa ushauri huo
juzi wakati akichangia mjadala wa mabadiliko ya kanuni ya 37 na 38 ya
bunge hilo, yalipendekezwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge hilo kuwa kila
mbunge awe huru kupiga kura ya wazi au ya siri.
Alisema
mjadala unaoendelea hautafika mwisho kutokana na pande mbili
zinazokinzana kila moja kushikilia msimamo wake, hali ambayo
inasababisha baadhi ya wabunge kutoka kwenye mada ya msingi na kuanza
kudhalilishana.
“Mimi
sitaki kujikita kwenye kura ya siri wala kura ya wazi, isipokuwa
napenda kushauri kuwa suala hili ili lipate ufumbuzi tulipeleke kwenye
kamati ya maridhiano badala ya kuendelea kulumbana kwani naamini kuwa
tunaweza kuzungumza kwa muda mrefu na hatutafikia uamuzi,” alisema
Mbowe.
Aliwaambia
wajumbe kuwa yapo mambo mengi na mazito ambayo tayari yamekwishaamuliwa
na bunge hilo kwa maridhiano, haoni sababu ya kuendelea na mjadala
usiokuwa na mwisho badala ya kutumia njia hiyo ya maridhiano ambayo
tayari imekwishaonyesha njia kwa baadhi ya mambo.
Wazo hilo liliungwa mkono na baadhi ya wajumbe hilo akiwemo Teddy Ladislaus, ambaye anawakilisha wanafunzi wa elimu ya juu.
Katika
kuonyesha kuwa mawazo ya Mbowe yalizingatiwa na Mwenyekiti, kabla ya
kuahirisha kikao hicho, Mwenyekiti Samwel Sitta aliteua baadhi ya
wajumbe kuingia kwenye kamati ya muda ya maridhiano na kuwataka wakutane
usiku huo.
Baadhi
ya wajumbe kamati ya Muda ya Maridhiano ni Profesa James Mwandosya,
Anne Kilango Malechela, Profesa Ibrahim Lipumba, Mbowe, Peter Mzirai,
James Mbatia, Anna Abdallah, Dk. Asha Rose Migiro , Askofu Dornald
Mtetemela, Amon Mpanju, Fredrick Werema na Hamad Rashid.
Kamati
hiyo ilitakiwa kujadili suala hilo na kuwasilisha mapendekezo yake kwa
Mwenyekiti kabla ya kupelekwa bungeni ili kutoa uamuzi wa mwisho.
Kanuni
ya 37 na 38 ziliwekwa kiporo mwezi uliopita wakati wa kupitisha kanuni
nyingine kutokana na wajumbe kushindwa kufikia mwafaka baada ya baadhi
yao kutaka itumike kura ya siri wakati wa kufanya maamuzi huku wengine
wakitaka iwe ni kura ya wazi.
Licha
ya kanuni hizo juzi kuletwa bungeni kwa mara ya pili, bado wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba waliendelea kuvutana na kutofikia makubaliano,
hali iliyomlazimu Freeman Mbowe kupendekeza suala hilo liamuliwe kwa
maridhiano.
0 comments:
Post a Comment