MVUA ZALETA MADHARA MAKUBWA JIJINI DAR ES SALAAM
Mvua zinazoendelea
kunyesha jijini Dar es Salaam, zimeleta adha kubwa, huku baadhi ya
wakazi wakilazimika kuhama baada ya makazi yao kukumbwa na mafuriko.
Gazeti la Mwananchi lilitembelea sehemu mbalimbali jijini jana na
kushuhudia mafuriko makubwa, huku baadhi ya nyumba kuta zake zikiwa
chini baada ya kuzidiwa na maji.
Katika maeneo ya Tanesco Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Msasani Bonde la
Mpunga na Mikocheni A Mtaa wa Vyura, hali ilikuwa mbaya zaidi, pamoja na
nyumba nyingi hasa za Msasani kuwa nzuri na za ghorofa, lakini zilikuwa
zimejaa maji eneo la chini kiasi cha kutoingilika.
Msasani:
Eneo la Msasani ndilo lililoathirika kwa kiasi kikubwa na mafuriko,
kwani barabara nyingi hazikupitika kirahisi kutokana na kujaa maji na
kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Maeneo ya Hospitali ya TMJ, Ofisi za Tanesco na Jengo la Biashara la
Shoperz Plaza, hali ilikuwa mbaya kutokana na maeneo hayo kujaa maji kwa
kiasi kikubwa.
Katika Mtaa wa Vyura Msasani, ambako kuna kliniki maalumu inayotoa
matibabu ya figo, maji yalikuwa yamejaa kiasi cha kuwekwa mashine za
kunyonya kuyatoa nje.
Tabata:
Katika eneo la Tabata hali ilikuwa mbaya zaidi kwani kuna baadhi ya
maeneo magari hayakuweza kupita kabisa kutokana na barabara nyingi kujaa
maji.
Daladala zinazofanya safari zake kati ya Tabata Segerea-Mnazi Mmoja,
zililazimika kuishia Buguruni kutokana na barabara ya Uhuru kujaa maji
na kushindwa kupitika.