Wednesday, 1 January 2025

BENKI YA CRDB YAFUNGUA MATAWI MAPYA MUGANGO, SIRARI MKOANI MARA

 

Katika kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma Vijijini na Sirari wilayani Tarime.


Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya ‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa taifa pia.
“Mkoa wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema Raballa.


Kabla ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime na 35 Musoma Vijijini.
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa.


Kutokana na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti, Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote nchini.
Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.

“Tawi hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema Mheshimiwa Gowele.

Licha ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele.

Kwenye uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
“Ufunguzi wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,” amesema Kusaya.

Sambamba na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime.
Share:

MBUNGE WA TARIME MJINI ACHUKIZWA NA MBUNGE WA NCHINI KENYA KUHAMASISHA KATIBA MPYA AOMBA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUCHUKUA HATUA

 

Na Helena Magabe - Tarime

MBUNGE wa Jimbo la Tarime mjini Michael Kembaki amesema ulinzi na usalama Tarime uko vizuri licha ya kuwa amekerwa na Mbunge wa Kurya Magharibi Nchini Kenya Matias Rhobi kuhamasisha katiba mpya nchini katika Jimbo lake na kuleta uchochezi kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kitendo cha mbunge huyo kuchocheo wananchi kudai katiba mpya  akiwa kwenye sherehe aliyoalikwa na moja ya mtia nia ,akihoji kwanini Mbunge hakufika na kudai kuwa hakuna maendeleo Tarime ,hakuna barabara za lami ni kitendo ambacho kimemkera na ni uvunjifu wa sheria za nchi.

Amesema Mbunge  huyo anatakiwa kufanya maendeleo Nchini kwake hasa kwenye Jimbo lake ambalo yeye si mgeni anazijua barabara za jimboni kwake zilivyo mbovu hasa njia ya Kehancha ambayo ilijengwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita hakuna maendeleo aliyofanya na  Jimboni kwake ni Mbunge Bubu ambaye haongelei Jimbo lake na hayuko kwenye rekodi ya vyombo vya habari .

Akiendelea kuzungumza amesema Katiba mpya sio kipaumbele cha wananchi wa Tarime bali wananchi wanahitaji maendeleo kama vile ,maji,umeme elimi,afya barabara na mahitaji muhimu hiyo katiba mpya anayowahamasisha wadai haitawasaidia kwani hata huko jimboni kwake  katiba haijaleta majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi wake hivyo aache  kuzungumzia vitu ambavyo haviingii akilini.


Ameiomba Serikali ya Kenya kumchukulia hatua mbunge huyo kwa sababu nchi ya Kenya ni jirani na ndugu hivyo asingependa kuona anasababisha mgogoro wa kudai  katiba na kusababisha uvunjifu wa amani   baina ya nchi mbili ambazo zina mahusiano mazuri.


" Kwanza sisi utamaduni wetu ni tofauti na wa nchi yao sisi tuna  heshima si rahisi kutukana  Kiongozi Kila mtanzania ana wajibu wa kuilinda heshima ya Nchi yake  kule  kwao wanatukana viongozi kwanza kura wanapiga  kwa ukabila,huku sisi tunafata sifa  asilete mambo yake ya kisiasa every day nikutia kauli ambazo hazina tija "alisema Kembaki.


Aidha amesema hakuna mtia nia ayemnyima usingizi kwani maendeleo amefanya na wananchi wanamkubali na katika sekta zote amezitendea haki kwa upande wa barabara ambayo alisema Bomani hakuna lami amesema itapata lami karibia maeneo yote na kwamba mbali na kilometa 6 za lami zilizo kwenye mpango zimeongezwa nyingine 18 ambapo kata ya Nyamisangura na Bomani zitapewa kipaumbele.



Share:

Tuesday, 31 December 2024

MBUNGE RWEIKIZA ALIVYOLIPAMBA JIMBO LAKE

Abainisha miradi mikubwa ya maendeleo kupitia kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba yake mzazi

Na Lydia Lugakila - Bukoba

MBUNGE wa jimbo la Bukoba vijijini Dkt. Jasson Rweikiza amebainisha miradi mikubwa ya maendeleo iliyofanyika na inayoendelea kufanyika jimboni kwake huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, kwa kuwapatia zaidi ya shilingi Bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni lango la kutoka na kuingia ndani ya mkoa wa Kagera.

Mbunge Rweikiza ametoa ufafanuzi huo  wakati akiongea wananchi mbalimbali pamoja na viongozi wa Mkoa wa Kagera waliofika katika viwanja vya Rweikiza vya shule ya Rweikiza iliyopo  Kyetema Wilaya ya Bukoba  kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba yake mzazi aliyekuwa akiitwa Samsoni Rweikiza. 

Rweikiza amebainisha kuwa,Dkt. Samia Suluhu Hassan amelipendelea Sana Jimbo lake kwani ametoa Mabilioni ya fedha kwa ajili ya maendeleo jimboni humo.

Akieleza miradi hiyo Mbunge huyo amesema kuwa pamoja na Daraja la Karebe ambalo limetengewa kiasi cha shilingi bilioni 9.3 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kutokana na daraja hilo kuchoka kwasababu limejengwa muda mrefu.

Amesema Daraja hilo ambalo lipo Barabara kuu inayounganisha kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba,Misenyi na Karagwe  Wananchi hulitumia katika kusafirisha mazao na bidhaa nyingine.

Akitaja Daraja lingine amesema ni la Chanyabasa ambapo wananchi hutumia kivuko kuvuka toka kata zaidi ya nane kuja hospitali ya Wilaya ya Bukoba Vijijini na wengime wanaovuka kwenda Bukoba mjini kwa shughuli za kujiingizia kipato jambo linalosababusha  watumie muda mrefu wakisubiri kivuko kwasababu kinavusha watu wachache na mizigo kidogo.

Aidha amesema ujenzi huo unaotarajiwa kuanza muda wowote kuanzia hivi sasa unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 kutokana na maagizo ya Serikali awamu ya sita.

 Ametaja daraja jingine ambalo limeingizwa kwenye mpango wa kufanyiwa ukarabati mkubwa na fedha yake italetwa wakati wowote kuwa ni Kyetema, linaunganisha

Barabara kuu kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine kuingia Bukoba na nchi jirani ya Uganda.

"Nitumie fursa hii kwa niaba ya Wananchi wa jimbo la Bukoba vijijini nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa kwetu ametoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo yetu"alisema Dokta Rweikiza.

Ameongeza kuwa kuna mradi mkubwa wa maji Kemondo ambao umekamilika na wananchi wanatarajia kupata maji mwezi mmoja ujao.

Naye askofu wa Dayosisi ya kaskazini magharibi (KKKT)  Abedinego Keshomshahara amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inafanya maendeleo makubwa kwa Wananchi pia mbunge Rweikiza amekuwa kiungo kizuri kati ya wananchi,Serikali na viongozi wa dini zote.

Kwa upande wa katibu mkuu mstaafu wa chama cha Mapinduzi (CCM),katibu mkuu kiongozi mstaafu,Balozi na mbunge Dkt .Bashir  amesema Mbunge huyo ameonyesha mfano mzuri kwa Wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

"Maombi ya miradi hiyo ililetwa kwenye chama wakati wa Serikali ya awamu ya tano na mbunge Rweikiza ambapo tuliingiza kwenye Ilani ila kutokana na maono mema ya Rais Dokta Samia  ameamua kutoa fedha nyingi ili ikajengwe na kunufaisha Wananchi" alisema Dokta Bashir.

Share:

BONANZA LA MICHEZO DR. SAMIA - JUMBE HOLIDAY LA KUFUNGA MWAKA 2024 NA KUUKARIBISHA MWAKA 2025 LAPAMBA MOTO SHINYANGA


Na Marco Maduhu,SHINYANGA

BONANZA la Michezo Dr. Samia/Jumbe Holiday limeendelea kushika kasi katika viwanja vya CCM Kambarage Mjini Shinyanga, kwa kuchezwa michezo mbalimbali.
Jackline Isaro (kulia) akicheza bao mara baada ya kuzindua bonanza hilo.

Mratibu wa bonanza hilo Jackline Isaro akizungumza juu ya bonanza hilo amesema linafanyika leo Desemba 31,2024 na kutamatika Januari Mosi 2025 majira ya saa 7 usiku katika viwanja vya mpira wa kikapu Risasi huku washindi wakipewa zawadi zao.
Jackline akizungumza kwa niaba ya James Jumbe ambaye ndiyo muandaaji wa bonanza hilo, amewataka majaji watende haki ili washindi wapatikane kwa uhalali.

Aidha, michezo ambayo inachezwa kwenye bonanza hilo ni mbio za baiskeli, mchezo wa bao,drafti,karata,ususi,Ps Game,Mpira wa pete,kikapu,kufukuza kuku kwa jinsia zote,kushindana kula,Polltable,kucheza mziki.
Michezo mingine ni mpira wa miguu, ambapo itakuwa kati ya bodaboda dhidi bajaji,bingwa wilaya ‘Ranges’ dhidi ya ngokolo, pamoja na DERBY ya upongoji.

Zawadi za washindi ni kwamba katika mbio za baiskeli mshindi katika makundi manne zawadi ni sh.milioni 2.1,mchezo wa bao mshindi wa kwanza sh.100,000,drafti mshindi wa kwanza sh.100,000, karat ash.100,000,msusi sh.100,000, Ps game mshindi wa kwanza sh.200,000 wapili sh.100,000, watatu sh.50,000.
Mpira wa pete, washindi wa kwanza watapewa sh.500,000, kleti za soda 7, mchele kilo 50, washindi wa pili sh.300,000, mchele kilo 50 na soda kleti 7.

Mpira wa kikapu kwa njinsia zote, mshindi wa kwanza atapa sh.500,000 na wapili sh.300,000.
Mchezo wa kufukuza kuku kwa jinsia zote washindi wa kwanza watapa kuku na sh.20,000, na mchezo wa kushinda kula washinda wakwanza watapata sh.20,000, huku mchezo wa polltable mshindi wa kwanza ataibuka na kitita cha sh.100,000, wapili sh.50,000.

Kwa upande wa mpira wa miguu timu ya bodaboda dhidi ya bajaji, mshindi wa kwanza atapata sh.500,000, Ng’ombe mmoja,kleti 7 za soda na mchele kilo 100, wapili sh.300,000, ng’ombe mmoja na mchele kilo 100.
Zawadi zingine bingwa wa wilaya Rangers dhidi ya Ngokolo, mshindi wa kwanza atapata 500,000,Ng’ombe mmoja, mchele kilo 100 na kleti 10 za soda, wapili atapata sh.300,000,Ng’ombe mmoja na soda kleti 10.

DERBY ya upongoji kwamba mshindi wa kwanza atapata sh.1,000,000, Ng’ombe mmoja,mchele kilo 100 na kleti 10 za soda, huku mshindi wa pili akipata sh.500,000,Ng’ombe mmoja, mchele kilo 100 na soda kleti 10.

TAZAMA PICHA👇👇
Mratibu wa bonanza la michezo Dr.Samia/ Jumbe Holiday Jackline Isaro akizindua bonanza hilo.
Mratibu wa bonanza la michezo Dr.Samia/jumbe Holiday Jackline Isaro akicheza bao.
Michezo mbalimbali ikiendelea kuchezwa kwenye bonanza hilo.
Share:

RAIS SAMIA AMLILIA JAJI WEREMA

 

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa familia ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Frederick Werema, huku akiwataka kuwa na subira na imani kufuatia kifo cha nguli huyo wa sheria nchini.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha

Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, mheshimiwa Jaji mstaafu Frederick Werema. 

Ninatoa pole kwa familia, mheshimiwa Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Majaji, ndugu, jamaa na marafiki”

“Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra na imani katika kipindi hiki cha kuomboleza msiba huu, na ailaze roho ya mpendwa wetu huyu mahali pema peponi,”- amesema.

Rais Samia ametuma salamu hizo kupitia mitandao yake ya kijamii leo Jumatatu, Disemba 30, 2024, muda mchache tangu kutolewa kwa  taarifa za kifo cha Jaji mstaafu  Werema zilipoanza kusambaa mitandaoni.

Share:

Monday, 30 December 2024

SERA YA MADINI NGUZO MUHIMU KUIMARISHA SEKTA YA MADINI – MBIBO


⚪  Yasaidia Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali zaidi ya Trilioni 1.93 kati ya 2021 na 2024

 📍 Morogoro, 

Imeelezwa kuwa Sera ya Madini ya 2009 imekuwa nguzo muhimu katika kuimarisha Sekta ya Madini, japokuwa kuna haja ya kuhuisha sera hiyo ili kuendana na mabadiliko ya sasa pamoja na matarajio ya baadaye katika maendeleo ya Sekta ya Madini na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa leo, Desemba 30, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo wakati akiongoza Kikao cha Mapitio ya Sera ya Madini ya mwaka 2009, kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro na kuhudhuriwa Wataalam wa Sera, na Wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa lengo la kufanya mapitio ya Sera hiyo na kuandaa mapendekezo ya maboresho.

Amesema kuwa mchakato mapitio ya Sera ya Madini ya mwaka 2009 katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi nchini. 

“Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na Sera ya Madini inayoendana na viwango vya kitaifa na mahitaji ya sasa ya kiuchumi na kijamii. Tunahitaji sera itakayotoa mwongozo thabiti wa usimamizi endelevu wa rasilimali za madini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Mbibo.

Mbibo ameongeza kuwa, Wizara ya Madini hivisasa inaongozwa na Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inalenga masuala mahsusi yakiwemo kuimarisha ushirikiano wa Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi; kuboresha mazingira ya kiuchumi kwa uwekezaji; kuongeza faida kutokana na uchimbaji madini; kuboresha masuala ya kisheria; kuendeleza wachimbaji wadogo; pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira.

Akitoa wasilisho kuhusu Manufaa ya Sera ya Madini 2009, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Angelo Haule, amesema kuwa, ukuaji wa Sekta ya Madini umeimarika na Mchango wake kwa Taifa umeongezeka ambako kati ya Machi 2021 na Mei 2024, Tume ya Madini ilikusanya shilingi trilioni 1.93 kama Mapato ya Serikali, ikionyesha ufanisi mkubwa wa usimamizi wa sekta hiyo.

“Ukuaji wa sekta uliongezeka kwa kiwango cha asilimia 7.3 hadi 10.9 kati ya mwaka 2020 na 2022, huku mchango wake kwenye Pato la Taifa ukiongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020 hadi asilimia 9.1 mwaka 2022. Aidha, masoko 42 na vituo 100 vya ununuzi wa madini vimeanzishwa, na kusaidia mauzo ya madini zenye thamani kubwa ikiwa ni pamoja na dhahabu, almasi, na tanzanite” amesema Haule

Haule amesisitiza kuwa, kwa upande wa ununuzi wa bidhaa na huduma, Kampuni za Kitanzania zilishiriki kwa asilimia 82 mwaka 2021 na asilimia 86 mwaka 2023, ikidhihirisha ongezeko la mchango wa wazawa kwenye sekta hiyo kwa kutoa huduma na kusambaza bidhaa migodini.

Ameongeza kuwa, zaidi ya leseni 23,924 za Uchimbaji Madini ya aina mbalimbali zilitolewa kati ya Mwaka 2021 na 2024, hatua inayolenga kuimarisha uwekezaji na ufanisi wa Sekta ya Madini nchini.

Share:

NYOTA MPYA YA TANZANIA: RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AONGOZA MAGEUZI YA KIUCHUMI

Tanzania, ambayo kwa muda mrefu imeonekana kama moja ya nchi zenye viwango vya juu vya kiuchumi katika Afrika Mashariki, sasa inavuma kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Tangu kuchukua madaraka mnamo Machi 2021, Rais Samia amejitokeza kama mtu wa mageuzi, akiiongoza nchi kuelekea utulivu, usawa, na ukuaji wa kiuchumi. Uongozi wake haujatu tu kuamsha matumaini ndani ya nchi, bali pia kuipa Tanzania nafasi muhimu katika mazingira ya kiuchumi ya kanda hii.  

Zama Mpya ya Uongozi  

Rais Samia Suluhu Hassan alifanya historia kwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania, akivunja vikwazo katika eneo la kisiasa ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiongozwa na wanaume. Kuongozwa kwake kulifuata baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, John Magufuli, ambaye wakati wa uongozi wake ulionyesha maendeleo makubwa ya miundombinu lakini pia sera zinazozua mabishano. Hata hivyo, mtindo wa uongozi wa Samia umekuwa unaojulikana kwa uhalisi, mazungumzo, na juhudi za kukuza umoja.  

Mtazamo wake umeonekana hasa katika juhudi zake za kurekebisha uhusiano wa kidiplomasia na kuvutia uwekezaji wa kigeni. Tofauti na sera za mtangulizi wake zilizokuwa za kujitenga, Samia amekubali msimamo wa wazi na wa kushirikiana, akishirikiana na washirika wa kimataifa na majirani wa kanda ili kuimarisha matarajio ya kiuchumi ya Tanzania.  

Mageuzi ya Kiuchumi na Ukuaji  

Chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeona mwelekeo mpya wa kuzingatia mageuzi ya kiuchumi na utofautishaji. Uchumi wa nchi, ambao kwa muda mrefu umetegemea kilimo, sasa unaona ukuaji katika sekta kama vile madini, utalii, na nishati. Uwiano wa kimkakati wa Tanzania, rasilimali asilia nyingi, na miundombinu inayoboreshwa vimeifanya kuwa mahali pazuri pa wawekezaji wanaotafuta fursa katika Afrika Mashariki.  

Moja ya mafanikio makubwa ya Samia imekuwa uwezo wake wa kurejesha imani katika mazingira ya biashara ya Tanzania. Serikali yake imeweka kipaumbele uwazi, kurahisisha michakato ya kiserikali, na kutekeleza sera zilizolenga kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI). Juhudi hizi hazijaenda bila kutambuliwa, huku waangalizi wa kimataifa wakisifia mwelekeo mzuri wa kiuchumi wa Tanzania.  

Miundombinu na Ushirikiano wa Kanda  

Maendeleo ya miundombinu ya Tanzania yamekuwa msingi wa mkakati wake wa kiuchumi. Bandari za nchi, hasa Bandari ya Dar es Salaam, hutumika kama milango muhimu kwa nchi zisizo na pwani kama vile Zambia, Malawi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Chini ya uongozi wa Samia, uboreshaji unaoendelea wa bandari na mitandao mingine ya usafiri unaimarisha jukumu la Tanzania kama kitovu cha biashara ya kanda.  

Zaidi ya hayo, ushiriki wa Tanzania katika Eneo la Biashara huru la Afrika (AfCFTA) unaonyesha juhudi zake za kushirikiana kiuchumi na nchi jirani. Kwa kukuza uhusiano wa karibu wa kiuchumi na nchi jirani, Tanzania iko tayari kufaidika na fursa kubwa zinazotolewa na soko la watumiaji linalokua la Afrika.  

Maendeleo ya Kijamii na Ushirikiano  

Rais Samia pia amechangia maendeleo ya kijamii, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na usawa wa kijinsia. Serikali yamechukua hatua za kushughulikia masuala kama vile elimu, afya, na uwezeshaji wa wanawake, kwa kutambua kuwa maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila kuwekeza katika mtaji wa binadamu.  

Uongozi wake umewahimiza kizazi kipya cha Watanzania, hasa wanawake na wasichana, ambao wanamwona kama kioo cha matumaini na ushahidi wa uwezekano wa kuvunja vikwazo vya kijamii.  

Changamoto na Njia 

Licha ya maendeleo, changamoto bado zipo. Tanzania bado inakabiliana na masuala kama vile umaskini, ukosefu wa ajira, na hitaji la kuendelea na utofautishaji wa kiuchumi. Zaidi ya hayo, kupungua kwa uchumi wa kimataifa na athari za mabaki ya janga la COVID-19 vinaweza kuwa hatari kwa mwelekeo wa ukuaji wa nchi.  

Hata hivyo, mtazamo wa Rais Samia wa kimazoea na wa kutazamia mbele umejenga matumaini miongoni mwa Watanzania na waangalizi wa kimataifa. Uwezo wake wa kusuluhisha changamoto ngumu huku akizingatia maendeleo ya muda mrefu unaashiria mwendo mzuri wa Tanzania.  

Kimulimuli cha Matumaini Afrika Mashariki  

Tanzania inapoendelea na safari yake ya kuwa nguvu ya kiuchumi katika Afrika Mashariki, Rais Samia Suluhu Hassan anajitokeza kama kimulimuli cha matumaini na maendeleo. Uongozi wake haujatu kuibadilisha Tanzania ndani ya nchi, bali pia kuimarisha nafasi yake kama mchezaji muhimu katika kanda hii.  

Kwa mtazamo wazi, juhudi za kushirikisha wote, na mwelekeo wa maendeleo endelevu, Rais Samia anapisha njia kwa mustakabali mkavu wa Tanzania na watu wake. Nchi inapoendelea kuinuka, dunia inatazama, na hadithi ya mageuzi ya Tanzania chini ya uongozi wake bado haijakwisha.

Share:

Sunday, 29 December 2024

KUNYWA FURAHA GINGER LIFE SWEET - KINYWAJI CHA MAAJABU! , FURAHA TANGAWIZI IPO PALE PALE!!


Furaha Ginger Life Sweet: Kinywaji kilichojaa furaha, afya, na nguvu.

Furaha Limited maarufu kwa utengenezaji wa Kinywaji  Furaha Tangawizi imekuletea kinywaji kingine cha asili Furaha Ginger Life Sweet  ambapo pia kina nguvu ya Tangawizi (Ginger)  kukufanya ujivunie afya bora na nguvu za asili.

Kinywaji kipya cha Furaha Ginger Life Sweet ni kinywaji cha asili kilichojazwa nguvu za ginger (Tangawizi), na manufaa mengi kwa afya yako. 

Ongeza Nguvu na Kuondoa Uchovu: Furaha Ginger Life Sweet inakuwezesha kutawala siku yako bila uchovu! Huupatia mwili wako nguvu ya asili.

Kinga ya Mwili Imara: Imarisha kinga yako dhidi ya magonjwa ili upate afya bora kila wakati.

Tengeneza Tumbo Lako: Furaha Ginger Life Sweet ni msaidizi mzuri katika mmeng’enyo wa chakula, kuondoa gesi tumboni na kuzuia sumu mwilini.

Afya Bora ya Magoti (Joint): Ikiwa unakutana na maumivu ya goti, Furaha Ginger Life Sweet itakusaidia kuondoa maumivu haya na kuimarisha afya ya viungo vyako.

Furaha Ginger Life Sweet

Kunywa furaha, pata afya! 🌱🍃

Tupigie 
0627460413 - Kahama
0757485153 - Mwanza
0713217634 - Dar es salaam
0713773001- Suppliers

Pia Kunywa Furaha Tangawizi kwa ajili ya Afya ya Asili kwa Mwili Wako!

👉 Inasaidia Mmeng'enyo wa Chakula
Furaha Tangawizi husaidia kuboresha utendaji wa mmeng’enyo wa chakula na kuondoa maumivu ya tumbo.

👉 Inaondoa Sumuvu Mwilini
Husaidia kuondoa sumu mwilini, ukiacha mwili wako ukiwa safi na wenye afya.

👉 Inaimarisha Kinga ya Mwili
Inasaidia kuimarisha kinga yako dhidi ya magonjwa, ikikufanya kuwa na afya bora kila wakati.

👉 Inasaidia Kupunguza Uzito
Furaha Tangawizi ni nzuri kwa wale wanaotaka kupunguza uzito, huku ikichoma mafuta kwa asili.

👉 Inakata Shinikizo la Damu na Magonjwa ya Moyo
Husaidia kupunguza shinikizo la damu na inazuia magonjwa ya moyo kwa njia ya asili.

👉 Inazuia Saratani
Furaha Tangawizi ni nzuri kwa kuzuia saratani kwa asili.

👉 Anti-Aging 100%
Furaha Tangawizi inasaidia kupambana na dalili za kuzeeka na kukuacha ukiwa na ngozi nyororo na afya nzuri.

Tupigie 
0627460413 - Kahama
0757485153 - Mwanza
0713217634 - Dar es salaam
0713773001- Suppliers




Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger