Sunday, 5 January 2025

KATIBU MKUU WIZARA YA NISHATI; UMEME NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA

...


Na Regina Ndumbaro Ruvuma 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu Dkt. Khatibu M. Kazungu, amesema kuwa umeme ni muhimu kwa uchumi, uhai, na maendeleo ya kisiasa na kijamii hivyo ni jukumu la Wizara kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika.

Ametoa kauli hiyo Januari 4 2025,
alipotembelea kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu Mkoani morogoro, kinachozalisha megawati 204 za umeme Dkt. Kazungu amesisitiza  kuwa Wizara ya Nishati ina jukumu muhimu la kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. 

Ameongeza kuwa ni muhimu kusimamia miradi ya uzalishaji umeme ili kuwa na usambazaji wa nishati kwa ufanisi na kuhakikisha kwamba maendeleo ya uchumi na jamii yanaendelea. "Wizara ya Nishati inajukumu kubwa kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika kwa ajili ya kusukuma mbele shughuli mbalimbali za maendeleo", amesema Kazungu.

Katika ziara hiyo,  amebainisha kuwa kituo cha Kidatu kilianza kuzalisha umeme tangu mwaka 1975 na kwa sasa kinatimiza miaka 50 ya huduma ambapo ameonyesha changamoto za usafirishaji wa umeme kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere kwenda Dodoma  changamoto hii inahitaji kutatuliwa haraka ili kuhakikisha usambazaji wa umeme unafanyika bila vikwazo.

Akiwa kwenye kituo hicho, Dkt. Kazungu amezungumzia mtambo namba mbili unaofanyiwa ukarabati ulioanza  mwezi  Mei mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025 huku akitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa mkandarasi anasimamiwa kwa karibu ili kazi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na mtambo huo uweze kuungana na mitambo mingine ambayo itaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme.

Dkt. Kazungu amefafanua kuwa ukarabati huo utasaidia kuzalisha umeme mwingi zaidi, ukilinganisha na umeme unaopatikana sasa, hii itasaidia kukidhi mahitaji ya umeme ambayo yanazidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu amesisitiza kuwa usimamizi mzuri wa miradi ya nishati utawezesha maendeleo endelevu na kuleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza Meneja wa mradi wa Kidatu HPP Mhandisi Manfred Lucas Mbyalu ameeleza huduma zingine zinazotolewa na kituo  hicho cha kufua umeme ni kinatoa huduma ya zahanati pamoja na elimu kwa wafanyakazi na wategemezi wao pamoja na wakazi wa vijiji jirani ili kuisaidia jamii kupata huduma bora za kijamii.

Kipekee ameeleza namna ambavyo TANESCO  itaendelea kuhakikisha kituo cha kufua umeme cha kidatu mitambo yake inakuwa katika hali nzuri na inapatikana muda wote (plant availability) ili kuhakikisha wanachangia umeme wa kutosha kwenye gridi ya Taifa kufanikisha adhma ya serikali ya awamu ya sita ya kukuza uchumi wa wa wananchi na nchi kwa ujumla.

Imeelezwa kuwa  ili kuendeleza maendeleo ya umeme nchini, ni muhimu kwa Serikali na wadau wa sekta ya nishati kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme, Hii itasaidia kupunguza changamoto za upungufu wa umeme na kuongeza uzalishaji wa umeme kwa ufanisi, hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger