Friday, 19 July 2024

BONANZA LA MICHEZO NA MAZOEZI KUFANYIKA PEMBA JULAI 20 - 28, 2024

...

Katika kuadhimisha miaka 10 ya klabu ya mazoezi ya Gombani (Gombani Fitness club), klabu hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) na Shirika ka Bima la Zanzibar wameandaa bonanza la mchezo wa mazoezi lenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika mazoezi na michezo.

Bonanza hilo litakaloshirikisha michezo ya aina mbali mbali litafanyika kisiwani Pemba kuanzia tarehe 20 hadi 28, Julai mwaka huu. Viongozi mbali mbali wa serikali na taasisi binafsi wanatarajiwa kushiriki siku ya Jumapili ya tarehe 28 ambayo ndio itakua kilele cha maadhimisho hayo kwa kuanza na matembezi kutoka Madungu na kumalizikia katika Uwanja wa Mpira wa Gombani, kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Jumla ya michezo mitatu itachezwa siku hiyo ikiwemo mazoezi ya viungo, mchezo wa magunia na mchezo wa kuvuta kamba ambayo jinsia zote zitashiriki kwa kuonesha vipaji na uwezo wao.

Katika shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho hayo waandaaji wa bonanza hilo watapita skuli na shehia mbali mbali kuhamasisha kuhusu usawa wa kijinsia katika mazoezi na michezo, pamoja na kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kujikinga na ukatili wa


kijinsia (GBV) kupitia michezo maalum inayojulikana kama (S4D acitivities).

Aidha jumla ya washiriki 500 kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja, Pemba na Tanga wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambapo kauli mbiu ni "Wekeza katika mazoezi na michezo kwa jinsia zote". Kauli mbiu hii inabeba lengo la bonanza hili kwa kuhakikisha watu wote wanahamasika kushiriki katika michezo bila kujali jinsia zao.

Kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Zanzibar tunahamasisha Wanamichezo kujikatia bima ya 'Group Personal Accident' (Bima ya ajali kwa Wanakikundi) ambayo itakuwa inawakinga dhidi ya maumivu ya mwili na/au vifo vitakavyosababishwa na ajali wakati wakiwa katika mazoezi na harakati zao za michezo za kila siku.

Wakati Gombani Fitness Club inatimiza miaka 10 tokea kuanzishwa kwake, mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa afya za wana klabu, bado kuna changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwepo kwa miundombinu rafiki ya kufanyia mazoezi kisiwani Pemba hususani kwa wanawake, dhana potofu dhidi ya mazoezi ya viungo, na kukosekana kwa taarifa sahihi juu ya umuhimu wa mazoezi na michezo katika vyombo vya habari.

Kwa sasa TAMWA ZNZ inatekeleza programu ya michezo kwa maendeleo yenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia katika michezo ambayo inatekelezwa kwa pamoja na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD) kwa ushirikiano mkubwa na Taasisi ya Maendeleo ya kimataifa ya Ujerumani (GIZ).

Imetolewa na;

Kamati ya maandalizi,

Bonanza la Michezo na Mazoezi Pemba.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger