Monday, 22 May 2023

NIT KUJENGA MAJENGO 8, IKIWA 5 KAMPASI YA MABIBO DSM NA 3 UWANJA WA NDEGE KIA KWA AJILI YA MAFUNZO YA MARUBANI

...
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa akisoma hotuba wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24 leo Mei 22,2023 Bungeni Dodoma.

****************

NA EMMANUEL MBATILO

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeendelea kutekeleza mradi wa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Mradi huo utaimarisha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia ambapo unajumuisha ujenzi wa majengo nane (8) ikiwa majengo matano (5) yanajengwa katika Kampasi ya Mabibo Dar-es-Salaam kwa ajili ya kufundishia Wahandisi wa Ndege na Wahudumu wa Ndani ya Ndege na majengo matatu (3) yatajengwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya mafunzo ya Marubani.

Aidha, ujenzi wa majengo matano (5) unaendelea ambapo umefikia hatua ya kusimamisha nguzo za jengo hilo na ujenzi wa majengo matatu (3) upo katika hatua za kumpata Mshauri elekezi wa usanifu.

Hayo yameelezwa leo Mei 22, 2023 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24.

Amesema kupitia kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga na operesheni za usafirishaji kilichoanzishwa chini ya mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, NIT imenunua vifaa vya mafunzo ambavyo ni Aircraft Engineering System Trainers; Virtual Maintenance Trainer kwa ajili ya mafunzo ya Uhandisi wa Matengenezo ya Ndege; na Fixed Cabin Crew Mock – Up kwa ajili ya mafunzo ya Wahudumu wa ndani ya Ndege.

"Katika kuimarisha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga, Serikali kupitia NIT imenunua Ndege mbili (2) zenye injini moja (1) kwa ajili ya kufundishia Marubani pamoja na Full Motion Cabin Crew Mock-Up yaani kifaa maalum cha kufundishia Wahudumu wa ndani ya Ndege". Amesema Prof. Mbarawa

Pamoja na hayo amesema NIT kupitia Kituo cha Kikanda cha Umahiri cha Mafunzo ya Usalama Barabarani kilichoanzishwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kimeendelea kutekeleza majukumu yake ambapo hadi kufikia Aprili, 2023, tathmini ya kumpata Mshauri Elekezi ambaye ataandaa mitaala na miongozo ya kufundishia pamoja na kupata ithibati ya kimataifa ipo kwenye hatua za mwisho.

Hata hivyo amesema Kituo kupitia ufadhili wa AfDB kinaendelea na hatua za ununuzi wa vifaa vya kufundishia mafunzo ya Usalama Barabarani ikiwemo Teleconferencing System pamoja na Geographic Information System (GIS) and Remote Sensing.

Amesema NIT imeendelea kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaalam na machapisho kwa lengo la kufundisha wataalam katika njia za usafirishaji ambazo ni Barabara, Anga, Reli, Maji na Bomba (Pipeline).

Ameeleza kuwa katika mwaka wa masomo 2022/23, Chuo kilitoa mafunzo ya kozi ndefu 34 ikilinganishwa na kozi 33 zilizotolewa katika mwaka wa masomo 2021/22 ikiwa ni ongezeko la kozi moja (1) sawa na asilimia 3. Kwa sasa Chuo kina wanafunzi wa kozi ndefu 14,920 ikilinganishwa na wanafunzi 12,942 katika mwaka wa masomo 2021/22 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,978 sawa na asilimia 15.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa akisoma hotuba wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa Mwaka 2023/24 leo Mei 22,2023 Bungeni Dodoma.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger