Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa Kijana Nahodha unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID), Jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Mradi Kijana Nahodha kutoka T- MARC Tanzania, Dkt.Tuhuma Tulli, akifafanua jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (kushoto) akizungusha mfano wa uskani wa meli kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri (kulia) kuashiria uzinduzi wa mradi wa Kijana Nahodha, hafla iliyofanyika jijini Dodoma ambapo viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Taasisi ya T-MARC wakishuhudia uzinduzi huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Masoko wa T- MARC Tanzania Bw. Alpha Joseph (kulia) alipotembelea maonesho katika uzinduzi wa Mradi wa Kijana Nahodha unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID). Kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Bi. Kate Somvongsiri.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
Na: Mwandishi Wetu - DODOMA
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amezindua mradi wa Kijana Nahodha unaolenga kuwafikia vijana 45,000 watakaonufaika na masuala ya elimu ya uongozi, ujasiriamali, afya na ujuzi.
Akizungumza Mei 24, 2023 kwenye uzinduzi huo wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la T-MARC Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID), Mhe. Katambi amesema mradi huo ni muhimu katika kuwezesha maendeleo ya kiuchumi hasa katika kuwajengea vijana uwezo wa kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kuleta maendeleo katika jamii.
“Aidha, miradi ya aina hii ni uthibitisho wa ushirikiano thabiti na dhati uliopo baina ya serikali ya Tanzania na Marekani, tunatambua mradi huu wa kijana nahodha utasaidia kufikia malengo tuliyokusudia ya kukwamua kijana wa kitanzania azione fursa na kuwa na mchango kwa Taifa lake,”amesema.
Naibu Waziri Katambi amewataka vijana wa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na mikoa yote mitano ya Zanzibar kuchangamkia fursa ya mradi huo.
“Niwaombe pia viongozi na maafisa mliopo wa Wizara zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huu kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia Sera na Miongozo ya Nchi iliyopo ili kuweza kuleta toja kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana nchini,”amesema.
Naye, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, amepongeza serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa jitihada za kuwainua vijana.
“Mradi huu utaleta manufaa kwa Tanzania na ni muhimu vijana wakatumia fursa ya mradi huu, nchi inayowekeza kwa vijana inapiga hatua kimaendeleo,”amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la T-MARC Tanzania, Charles Singili, amesema mradi utainua vijana kufikia ndoto zao na unatekelezwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya nchi.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa mradi huo, Dkt.Tuhuma Tulli, amesema utatekelezwa kwa miaka minne (2022-2026) na unalenga kusaidia vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 25 hususan vijana ambao hawana elimu ya shuleni, vijana wasio na ajira, vijana wenye ulemavu, wasichana waliozaa katika umri mdogo na wenye maambukizi ya VVU.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na USAID kwa Dola za Marekani Milioni 10.6 na utaenda kuboresha upatikanaji wa elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya ufundi stadi, afya, uraia, ujasirimali na uongozi.
0 comments:
Post a Comment