NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imesema inaendelea na utaratibu wa kujenga na kukarabati vyuo vya watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwasaidia wenye ulemavu kupata ujuzi ili kujikomboa kiuchumi.
Akizungumza Jijini Dodoma baada ya kupokea msaada wa vifaa visaidizi kwa ajili ya wenye ulemavu vyenye thamani ya shilingi milioni 13.9 ambavyo ni viti mwendo 55 na fimbo nyeupe 50 za wasioona kutoka kwa Taasisi ya kutoa huduma ndogo za kifedha (ASA Microfinance Company Limited), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anapata haki yake bila vikwazo.
Aliongeza kuwa ipo mikakati madhubuti ya kuhakikisha masuala ya wenye ulemavu yanapewa kipaumbele ikiwemo uboreshwaji wa vyuo ikiwemo Chuo cha Mwanza ambacho ujenzi wake unatarajiwa kukamilika kuanzia mwezi Januari mwakani kuwawezesha vijana kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kufanya shughuli zao za uzalishaji na kushiriki katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Kwasasa Wizara inaratibu kwa kasi ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu na ufufuaji wa vile ambavyo vipo.Tunaendelea kufanya hivyo katika Chuo cha Yombo Dar es salam, tumezindua Chuo kingine Tabora ambacho kilikuwa kimefungwa kwa miaka 10 na kumalizia ujenzi wa chuo cha kisasa Mkoa wa Tanga,” alisema Naibu Waziri Ummy.
Pia Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuendelea kutoa fedha ya elimu bila malipo ambapo watu wenye ulemavu nao hunufaika na mfumo huo huku akieleza kuwa Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
“Serikali kupitia bohari kuu ya dawa inaendelea kuagiza mafuta ili kuwakinga dhidi ya saratani ya Ngozi kwa watu wenye ualbino sambamba na kuzitaka Halmashauri kuendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kupitia asilimia 10 inayotolewa na kila Halmashauri kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa sababu hii inawasaidia kupambana na umasikini,”alieleza.
Hata hivyo aliishukuru kampuni hiyo kwa moyo wake wa kujitoa na kuiunga mkono serikali katika juhudi za kuwaletea ustawi wananchi wake na kuwahimiza wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuwasaidia watu wenye ulemavu hatua itakayofanya kujiona wana thamani na kutambulika ndani ya jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ASA Microfinance Limited , Muhammad Shah Newaj alieleza kwamba wametoa msaada huo wenye thamani ya Sh. milion 13.9 kama sehemu ya kutambua mchango wa watu wenye ulemavu katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa akisema wana uwezo wa kufanya kazi kama watu wengine endapo watapewa fursa na kuhudumiwa katika mahitaji yao wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanaisaidia jamii kuepukana na umaskini.
Naye Afisa Sheria kutoka ASA Microfinance Limited, Zephania Paul alifafanua kwamba vifaa hivyo ni sehemu ya kutoa huduma kwa jamii na awamu hiii ni yapili kufanyika akisema awamu ya kwanza ilifanyika jijini Dar es salaam huku akibainisha kuwa taasisi hiyo ipo katika Mikoa nane ya Tanzania Bara na Zanzibar na hadi sasa wamewafikia wanawake 1,600 na kutoa ajira .
Akitoa shukrani zake mama wa mtoto mwenye ulemavu Martha Mshama aliishukuru serikali kwa kushirikiana na wadau kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu akieleza kuwa kiti alichopewa kitamsaidia kufanya kazi zake kwani awali alikuwa akitumia muda mwingi kuwa karibu na mtoto akihofia kuanguka na kupata madhara.
” Tunaishukuru serikali kwa kutupatia viti mwendo ambapo ni msaada mkubwa kwangu maana nilikuwa nikihofia usalama wa mtoto wangu kuna wakati anaweza kuanguka natakiwa kuwa naye karibu sana lakini sasa walau nitaweza kufanya kazi zangu nawashukuru sana Mungu awabariki,”alishukuru Martha.
Naye Selina Nigangwa (mwenye ulemavu wa miguu) mkazi wa Swaswa aliishukuru serikali kwa kuwapatia msaada huo na kushauri wakati mwingine kutoa viti vya kuendesha kwa kutumia mikono.
“Tunashauri serikali wakati mwingine watoe viti vya kuendesha kwa mikono ili tuweze kuendesha wenyewe bila kumtegemea mtu,” alieleza Selina.
0 comments:
Post a Comment