Na Mwandishi wetu – Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, Jasinta Mboneko amewataka wanafunzi wote wa kidato cha sita katika shule zilizoko wilayani kwake kuacha hofu badala yake wasome kwa bidii na kutumia muda mchache uliosalia kuhitimisha masomo yao na kujiweka sawa kwa ajili ya mitihani ijayo.
Mboneko ametoa kauli hiyo Juni mosi, 2020 mjini Shinyanga wakati akikagua na kuzungumza na wanafunzi mbalimabli kutoka shule tano zilizoko manispaa hiyo na Shinyanga Vijijini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kuwataka wanafunzi wote wa kidato cha sita na vyuo kurejea huku suala la usalama wa afya na tahadhari ya ugonjwa wa covid 19 ukizingatiwa.
Akizungumza na wanafunzi wa kidato cha sita shule ya Sekondari Old Shinyanga, Jasinta amesema kuwa kwa sasa wanapaswa kubadili fikra zao na kurejea katika masomo kutokana na muda uliosalia kuwa mchache kwao kwani wana uwezo wa kuhimili na kujiandaa vizuri.
“Niwaombe nyinyi kidato cha sita hapa Shuleni Old Shinyanga mpo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hakikisheni mnasoma na mnaacha kulala kwani muda siyo rafiki sana maana msipofanya bidii ya kupitia yale mliosoma mapema kabla ya COVID 19 kwa sasa mtashindwa kufanya vizuri katika mtihani wenu wa mwisho,” amesema.
Akiwa shule za Sekondari Buluba,Savannah Plains na Don Bosco Mkuu huyo wa wilaya ameendelea kuwakumbusha na kuwasihi wanafunzi kusoma kwa bidii kipindi hiki kilichosalia akiwataka kuondoa hofu kwani hofu ni ugonjwa mkubwa kuliko tatizo lenyewe.
Aidha amewataka wamiliki wa shule binafsi mkoani Shinyanga kuacha kuongeza gharama za aina yoyote kwa kisingizio cha ugonjwa wa COVID 19 huku akiwasisitiza walimu kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni na kuendelea na masosmo kwani muda umebaki siku 27 pekee.
Katika hatua nyingine Mboneko amewaomba wazazi nchini wenye watoto wanaosoma shule zilizoko wilayani Shinyanga ambao hawajafika wahakikishe watoto wao wanafika shule kwani muda unazdi kusonga hali itakayowafanya washindwe kufanya vyema.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tinde iliyopo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Pendo Matonange amesema kuwa shule hiyo ina idiadi ya wanafunzi mia 415 huku wanaotarajia kuhitimu kidato cha Sita wapo 204 tayari wamewasili wanafunzi 173 kati ya 204 wanaotarajia kufanya mitihani yao ya mwisho Juni 28, mwaka huu.
Mwalimu Matonange amesema kuwa suala la usafi na usalama kwa wananfunzi wote juu ya kuchukua tahadhari ya Corona limepewa kipaumbele kutokana na tahadhari zinazotolewa na watalaam wa afya ikiwemo kuweka vitakasa mikono, sabuni na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari binafsi ya Savanah Plains, Yona Ludomya na Wiliam Makenge wa Sekondari ya Buluba wamesema kuwa tahadhari ya ugonjwa wa COVID imechukuliwa kwa hali ya juu kwa kuandaa mazingira rafiki kuhakikisha kuwa kila mwananfunzi anafanya mtihani wake akiwa na afya njema.
Wameongeza kuwa kwa sasa jitihada na nguvu kubwa zimeelekezwa kwa wanafunzi hao ili waweze kukamilisha na kufanya mitihani yao kwa kzingatia kanuni na maagizo ya Serikali.
Ziara hiyo ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga imefanyika ikiwa ni kukagua na kujionea utekelezaji wa maagizo ya serikali iwapo shule zimezingatia maagizo yake kwa kuchukua tahadhari mbalimbali dhidi ya virusi vya Corona ikiwemo kuandaa vitakasa mikono na maji, ambapo amezitembelea shule za Sekondari Old Shinyanga, Tinde wasichana za Serikali na Buluba, Don Bosco na Savannah Plains zinazomilikiwa na watu binafsi.
Wa Pili Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akitoa maelekezo kwa Mkuu wa shule ya wasichana Tinde Pendo Matonange
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta mboneko akiongea na wanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Savannah plains
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari ya wasichana Tinde wakiendelea kumsikiliza mkuu wa wilaya.
Wanafunzi wa kidato cha sita shule ya wasichana Tinde wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko wakati akikagua utekelezaji wa maagizo ya Serikali dhidi ya Ugonjwa wa Corona
Wanafunzi wa shule ya sekondari Old Shinyanga wakismikiliza mkuu wa wilaya wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa usalama wakiwa darasani
Wa Kwanza Kulia ni Mkuu wa wilaya Shinyanga Jasinta Mboneko akisisitiza jambo
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akihitimisha ziara yake shule ya Sekondari Don Bosco Didia
0 comments:
Post a Comment