Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa mara ya kwanza amewafanyia usaili wahitimu wa taaluma ya Sheria kwa ajili ya kuwapokea na kuwakubali kuwa Mawakili kwa njia ya Mtandao ‘Video Conference’.
Akizungumzia kuhusu usaili huo, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Messe Chaba, alisema usaili huo unafanyika baada ya wahitimu hao, kufanya maombi ya kukubaliwa kuwa mawakili kwa mtandao na kukidhi vigezo vinavyotakiwa na Baraza la Elimu ya Sheria.
‘‘Tumetumia njia hii ya mtandao ili kuendena na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuliishi agizo la Jaji Mkuu alilolitoa katika hotuba yake ya kilele cha Siku ya Sheria nchini Februari Mosi, mwaka 2018, ambapo aliwataka Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kubadili fikra na mtazamo ili kujiandaa na kujiimarisha kwenye matumizi ya TEHAMA katika karne hii ya 21, ikiwa ni hatua ya kurahisisha utendaji kazi wetu. Tumefanikiwa kutumia njia vizuri kwa siku na tuna wahitimu takribani 80 wanaofanyiwa usaili, ’’ alisema Mhe. Chaba.
Alisema usaili huo, umeanza kufanyika Juni 23, mwaka huu na utamalizika Julai 3, mwaka huu.
Chaba ambaye pia Katibu wa Baraza la Elimu ya Sheria, alisema njia hiyo ina faida kwa wanataaluma hao, kwa kuwa inawapunguzia gharama za usafiri, malazi, muda na usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa wa kusafiri Jijini Dar es Salaam ili kufika kwenye ofisi za Jaji Mkuu kwa ajili ya kufanyiwa usaili huo.
Aliongeza kuwa usaili huo umekuwa ni fursa kwa Mahakama kwa kuwa umeongeza matumizi ya TEHAMA hususan kipindi ambacho dunia na nchi ya Tanzania inakumbwa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu, COVID 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, ikiwa ni hatua mojawapo za kuepuka maambukizi dhidi ya tatizo hilo.
‘‘Mchakato wa kuwapata wanataaluma hao ulifanyika mwezi Aprili na Mei, lakini hufanyika mara mbili kwa mwaka, ambapo utafanyika tena Novemba na Desemba mwaka huu. ‘‘Wanataaluma hawa walituma maombi katika baraza hili, kuanzia Aprili Mosi mwaka huu hadi Mei 14, mwaka huu kwa ajili ya kuomba kuwa mawakili, hivyo jumla yao walikuwa 651 na waliokidhi vigezo ni takribani 613 ambao ndio tunawafanyia usaili,’’ alisema Mhe. Chaba.
Alivitaja baadhi ya vigezo vya kukubalika katika usaili huo ni kuleta maombi, kumaliza Shule ya Sheria (Law School), kuwasilisha vyeti, kupitia elimu ya Diploma ya Sheria, Elimu ya Sheria ya Chuo Kikuu, kuleta matokeo ya taaluma hiyo, kuwa na tabia njema, hati ya kiapo cha majina, na barua ya utambulisho wa kazi.
Wanataaluma hao baada ya kumaliza usaili na kufaulu,wanatarajiwa kukubaliwa na kupokelewa kuwa Mawakili kwenye Sherehe ya 62 itakayofanyika Julai 10, mwaka huu. Aidha, mawakili hao wakishakubaliwa wataingizwa katika Mfumo wa Kusimamia Mawakili (TAMS). Sherehe hizo zilianzishwa rasmi mwaka 1986.
Maeneo yanayotumika kufanya usaili huo ni Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam watahiniwa (438), Arusha (46), Tanga (watano), Tabora (16), Mtwara (watatu), Dodoma (23), Mbeya (27) na Mwanza (44). Awali wanataaluma wa fani ya Sheria walikuwa wakikutana na Jaji Mkuu ana kwa ana kufanyiwa usaili.
picha namba 1.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa ofisini kwake Jijini Dar es Salaam akimfanyia usaili mhitimu wa Shule ya Sheria kwa njia ya mtandao maarufu kama ”Video Conference” ikiwa ni maandalizi ya kuapishwa kuwa Wakili .
0 comments:
Post a Comment