Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imewatoa hofu wanafunzi wa kidato cha sita walioanza masomo June Mosi mwaka huu katika shule sita zilizopo wilayani humo kuhusiana na ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.
Pia imewataka kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya wataalamu wa afya yaliyotolewa na Wizara ya Afya katika kipindi hiki ambacho wanajiandaa na mitihani ya mwisho ya Taifa inayotarajia kufanyika hivi karibuni.
Wanafunzi nikutoka shule za sekondari, Busoka, Anderleck, John Paul, Mwendakulima, Mwalimu Nyerere na Dakama na kuwataka walimu wa shule hizo kuhakikisha kila darasa linakuwa na ndoo za kunawia mikono,Vitakasa mikono pamoja na matumizi ya Barakoa wakati wa masomo.
Anamringi Macha ni mkuu wa wilaya ya Kahama, aliyabainisha hayo June 2 Mwaka huu katika ziara ya kukagua maandalizi ya Mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha sita kuhusiana na namna viongozi wa shule hizo walivyotekelza maagizo ya serikali ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 kwa wanafunzi.
Aidha Macha alisema kuwa Ugonjwa wa Corona bado upo lakini hapa nchini maambukizi yameshuka ukilinganisha na hapo awali,na kuwataka wanafunzi kutokuwa na hofu juu ya ugonjwa huo na badala yake wajikite na maandalizi ya mitihani yao ya Mwisho.
“ Wanafunzi wangu msiazimane barakoa na muache tabia za kutembeleana katika mabweni nyakati za usiku,kumbukeni moja ya sababu ya kuambukizana kwa ugonjwa huu ni kuazimana,nguo,barakoa,kugusana na kutonawa mikono,”alisema Macha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege alisema kuwa,watahakikisha wanawapatia wanafunzi huduma zote katika kipindi hiki cha mitihani ikiwemo, chakula na malazi ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya Mwisho.
“Walimu wapo tayari kuwasaidia kwa masomo yote na hakuna mwanafunzi ambaye ataruhusiwa kwenda kuzurura nje ya maeneo ya shule tumejipanga vizuri na ndoo,vitakasa mikono na sabuni zipo kwa wingi hivyo tunaamini watamaliza mitihani yao salama,”alisema Berege.
0 comments:
Post a Comment