Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Benard Membe, ameendelea kutia mkazo mpango wake wa kuwania urais kupitia chama chochote cha siasa nchini.
Membe ambaye mwaka 2015 alitia nia kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema kama chama chake hicho kitamsafisha kuhusu tuhuma zinazomkabili, atachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Membe alivuliwa uanachama na Kamati ya Maadili ya CCM, Februari mwaka huu, baada ya sauti yake na makada wengine wa chama hicho kuvuja kwenye mitandao ya kijamii, wakielezea namna chama hicho kilivyokosa mwelekeo.
Alitangaza msimamo wake huo kupitia mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya DW, kijijini kwake Londo, mkoani Lindi na kurushwa jana.
Membe alisema CCM kikimsafisha, ni wazi kuwa atawania urais kupitia chama hicho kwa sababu ni haki yake ya kikatiba kufanya hivyo na kwamba siyo dhambi kugombea.
“Ni kweli kabisa mwaka huu nitagombea, lakini sijui nitagombea kupitia chama gani kwa sababu moja kama CCM 'itani-clear' (itanisafisha), ninaweza kugombea kupitia CCM kwa sababu ni haki yangu na furaha yangu ni furaha ya watu pia kuona watu wakishindana na wala siyo dhambi kugombea.
Kuhusu kupitishwa na chama hicho, alisema anaweza asiwe na nafasi ya kupitishwa, lakini anaweza kuwa na haki.
Membe alisema ana uhuru wa kugombea kupitia chama kingine cha siasa kwa sababu kukosa haki ndani ya chama, kunampa uhuru kutafuta haki kupitia chama kingine.
Alisema siyo lazima kuwania nafasi ya urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo wala Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) isipokuwa chama chochote kitakachompendeza anaweza kutumia kuwania nafasi hiyo.
“Mimi ninakuambia uwanja upo mezani, chochote kinaweza kuja kitakachonipendeza ninaweza kufika,” alisema Membe.
Alisema yeye pamoja na wanachama wengine sita wa CCM wana msimamo kama wake, lakini hawezi kuwataja kwa sasa kwa sababu wanaweza kufukuzwa chama wakati wowote kuanzia sasa.
“Siwezi kuwasema kwa sababu watafukuzwa chama, nakuapia leo kama tusingekuwa tunafukuzana, ningekupa majina yote sita mimi wa saba, lakini watafukuzwa kesho asubuhi," alisema.
Credit: Nipashe
0 comments:
Post a Comment