Monday, 4 May 2020

Bodi Ya Tumbaku Tanzania Kusimamia Zoezi Laulipaji Madeni Ya Wakulima Ushetu

...
SALVATORY NTANDU
Bodi ya Tumbaku Tanzania imesema itahakikisha inasimamia zoezi la ulipaji wa Madeni ya wakulima wa zao hilo ya msimu wa mwaka 2018/19 ambayo walikuwa wanaidai kampuni ya Magefa katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa kabla ya kufunguliwa kwa masoko mapya ya Mwaka 2020/21.

Kauli hiyo imetolewa leo na Meneja wa Bodi ya Tumbaku katika mkoa wa Kitumbaku Kahama, Albert  Charles wakati akizungumza na Mpekuzi blog kuhusiana na namna zoezi hilo litakavyofanyika na kuwatoa hofu wakulima kuwa watapatiwa stahiki zao.

 “Kampuni ya Magefa imetuhakikishia kuwa watalipa fedha hizo kwa vyama vya Msingi, Ilomelo, kangeme na Tumaini Amcos ambazo walinunua tumbaku katika masoko yaliyofanyika mwezi Marchi 2019 zinazokadiriwa kufikia milioni 80,” alisema Charles.

Alifafanua kuwa malipo hayo yalichelewa kutokana na Kampuni hiyo kutolipwa baada ya kuuza tumbaku hiyo nje ya nchi sambamba na uwepo wa Ugonjwa wa Covid 19 ambao umesababisha nchi nyingi kufunga mipaka na kukwamisha kufanyika kwa masoko hayo.

“Katika msimu wa 2018/19 wakulima wote  waliofunga mikataba na kampuni za ununuzi wa Tumbaku katika mkoa huu za TLTC, Allience One na JTI walilipwa fedha zao kwa asilimia 100 lakini baadhi yao walibainika kulima tumbaku nje ya mkataba ambazo serikali ilitafuta mnunuzi(Magefa)ambaye hivi karibuni ataanza kuwalipa,”alisema Charles.

Sambamba na hilo Charles amewatahadharisha wakulima kuwa  katika msimu ujao wa masoko ya tumbaku hakuna mkulima atakayeruhusiwa kuuza kwa zaidi ya asilimia 110 na wameandaa daftari maalumu ambalo litatumika kwa wakulima wote ili kudhibiti biashara ya Kangomba na ulanguzi wa Tumbaku ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima .

 “Msimu uliopita kunavyama vya Msingi viliuza tumbaku kwa asilimia 110 hadi 146 kinyume na sheria namba 24 ya mwaka 2001 ya Tumbaku na kanuni zake inayomtaka mkulima kulima zao hilo bila mkataba ama mnunuzi,”alisema Charles.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) Emmanuel Charahani amewataka wakulima kuwaepuka walanguzi wa zao hilo katika msimu mpya wa mwaka huu  ili kuondokana na tatizo la kukosa masoko na kusababisha serikali kuanza kutafuta wanunuzi kwa tumbaku iliyozalishwa nje ya Mkataba .

“Tunzeni tumbaku zenu vizuri, zingatieni Usafi na pangeni Madaraja kama inavyotakiwa haipendezi kila mwaka tunakamata tumbaku chafu na safi ikiwa imechanganywa sokoni ”alisema Charahani.

Sambamba na hilo pia, Charahani amezitaja kampuni zilizofunga Mkataba wa kununua zao hilo katika mkoa huo kwa mwaka 2020/21, kuwa ni  Petrobena east africa L.t.d, Jespany Company L.t.d, Magefa, Grand Tobbaco, Allience one, JTI na kufafanua kuwa kampuni ya JESPANY COMPANY L.T.D  haihusiki na deni hilo kwani ndio mara yake ya kwanza  kufunga mkataba wa ununuzi wa na wakulima katika mkoa wa kitumbaku Kahama.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger