KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Chritopher Kadio, ameitaka Idara ya Huduma za Uangalizi kuhakikisha wafungwa wenye vifungo vya nje wanafanya kazi zinazoonekana kwa wadau.
Alisema kutekelezwa kwa agizo hilo, wadau wataona faida ya wahalifu kutumikia adhabu zao nje ya Magereza badala ya kufanya usafi kwenye maofisi.
Kadio aliyasema hayo Mjini Morogoro jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili unaoshirikisha Maafisa Wafawidhi wa idara hiyo kutoka mikoa 23 nchini.
Alitoa wito kwa idara hiyo kuandaa mpango mkakati ambao utaiwezesha Serikali kupunguza mzigo wa kuwahudumia wahalifu waliopo gerezani.
Alisema baadhi ya wahalifu wanaweza kutumikia adhabu zao nje ya Magereza hivyo ni wakati muafaka kwa idara hiyo kuwa na suluhisho ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi.
“Lipo tatizo kubwa ambalo linaukabili mpango huu hasa fikra za kizamani kuwa adhabu ya kila mhalifu ni kwenda jela, dhana ya adhabu mbadala bado haijakolea katika fikra za wengi.
“Fikra hizo zipo kwenye sekta zote za jamii yetu kuanzia katika mahakama, baadhi ya Mahakimu wana kigugumizi cha kutoa adhabu za kutumikia jamii nje ya jela,” alisema.
Alifafanua kuwa, pia kwenye jamii vijijini na mitaani bado hawajaona umuhimu wa kutekeleza jukumu la kuwarekebisha na kuwalea jamaa zao wnaojiingiza katika uharifu.
Kadio alisema viongozi wa kisasa nao hawajalichangamkia jambo hilo na kulipigia debe kwa nguvu zote.
“Ni imani yangu kuwa idara pamoja na Wizara tunalo jukumu la kuhamasisha na kutoa elimu kwa wadau tukianzia mikoani, kila kiongozi wa Mkoa awe na mpango kazi wa kuelimisha.
“Mbali ya kuhamasisha matumizi ya adhabu mbadala pia ni jukumu letu kuhamasisha jamii ijiepushe na vitendo vya uhalifu, kuheshimu utawala wa sheria unaozingatia haki,” aliongeza.
Alisema pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili idara hiyo katika utendaji kazi wao, aliwataka wakuu wa idara watafute ufumbuzi wake badala ya kuitegemea serikali izitatue.
Kadio alisema Wizara hiyo itaendelea kuwawezesha kadri inavyoweza ndio maana kila mwaka inaboresha bajeti yao.
“Ni vema mkafahamu kuwa, dhamira na dira ya Wizara yetu ni kudumisha utulivu, usalama na amani kwa Watanzania na ili dhamira hii ikamilike, idara imepewa jukumu la kusimamia utekelezwaji wa adhabu mbadala ya kifungo gerezani.
“Mnalo jukumu la kuchangia mafanikio ya Wizara iweze kufikia dhamira yake kwa Taifa,” alifafanua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara hiyo, Aloyce Musika, alisema lengo la mkutano huo ni kufanya tathmini ya shughuli zilizofanyika mwaka mzima, kupanga mipango ya mwaka ujao.
Alimshuruku Kadio kwa kufungua mkutano huo ambao unashirikisha Maafisa Wafawidhi kutoka mikoa 23 ambayo wameifikia nchini isipokuwa mikoa mitatu ya Katavi, Lindi pamoja na Ruvuma.
“Miaka yote tumekuwa tukifanya mkutano kama huu kwa mafanikio makubwa mbali ya ugumu wa bajeti lakini Wizara imekuwa karibu na sisi, kukaa pamoja,” alisema.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment