Thursday, 26 March 2020

RAIS MAGUFULI : UCHAGUZI MKUU WA TANZANIA 2020 HAUTAAHIRISHWA LICHA YA KUWEPO KWA CORONA

...
Na Peter Elias, Mwananchi 
 Rais John Magufuli amesema uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu hautaahirishwa licha ya kuwepo kwa mlipuko wa virusi vya corona.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Machi 26,2020 Ikulu ya Chamwino, Dodoma wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ripoti ya Takukuru.

Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri kwamba kazi hazifanyiki na hakuna kukutana kwa sababu ya corona. Amesema hata nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo, bado mabunge yao yanakutana kama kawaida.

"Sisi tunaendelea kukutana, ndiyo maana hata Bunge linaendelea na vikao vyake, hata huko kwenye nchi zilizoathirika kabisa, mamilioni ya watu wamekufa kwa corona, bado mabunge yao yanakutana. Kazi lazima ziendelee.

"Na uchaguzi tutafanya, wapo wanaofikiri kwamba tutaahirisha, nani anataka kukaa kwenye maofisi haya muda wote huo," amesema Rais Magufuli wakati akizungumza kwenye hafla ya kupokea ripoti hizo.

Rais Magufuli ameeleza kushangazwa na mwandishi mmoja kuandika habari kwamba "Baraza la madiwani lafanya mkutano licha ya corona" na kuhoji kama mikutano ya aina hiyo imezuiwa.

Amesisitiza kwamba kazi lazima ziendelee kufanyika licha ya uwepo wa virusi hivyo na mikutano ya baraza la madiwani, Bunge na hata ile anayoifanya yeye itaendelea kufanyika kwa sababu ni sehemu ya kazi zao.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger